Thursday, October 2, 2008

Ndio maana wasanii wana washauri.

Sanaa ya muziki ni kazi ambayo kwa wanaoitumia kuendesha maisha yao wanawekeza mengi kuhakikisha kuwa kila kitu (pamoja na maamuzi) yanakwenda sawa na mipango yao ya maisha. Ni kuanzia namna ya kujidhihirisha kwa mashabiki, katika nyumba za ibada, katika mahojiano, katika kutambua ni muda gani ulio muafaka kutoa wimbo na ama albamu na wimbo upi utoke kulingana na wakati na dalili za mauzo na hata uwekezaji mwingine kwa ajili ya maisha yajayo. Pia kuna suala la nini cha kuvaa unapokuwa wapi na kina nani kuhakikisha kuwa unawakilisha kazi na wewe mwenyewe pia imani na misimamo yako bila kwenda kombo.
Tumeshuhudia baadhi ya wasanii wetu wakiongea mambo ya ajabu wafanyiwapo mahojiano na hata kutojitokeza vema ama katika mwonekano utakiwao watakiwapo kuhudhuria baadhi ya matukio. Na hii ni tofauti na zile nguo za ajabu ambazo baadhi yao hujitokeza nazo kwenye matamasha na maonesho yao.
Na sasa nimeguswa na hili la msanii ambaye amepata matamasha mengi katika kipindi cha mwezi uliopita pengine kuliko msanii mwingine yeyote wa "kizazi kipya" nchini Ali Kiba ambaye kwa sababu azijuazo yeye na "mshauri" wake ametokea katika Baraza Tando na vyombo vingine vingi akiwa na hii T-Shirt yenye kuhamasiaha kuachiwa na TID.
Ikumbukwe kuwa TID amefungwa mwaka 1 baada ya kukiri kumpiga mlalamikaji Ben Mashibe kwa trei ya chupa ya bia. Kwa mujibu wa http://www.jambonetwork.com/blog/?p=13225 "baada ya kusoma maelezo,Hakimu alimpa nafasi mtuhumiwa kujitetea,ambako alisema kwamba alikuwa amepitiwa siku ya tukio kutokana na pombe alizokuwa amekunywa,hivyo akaiomba mahakama iahirishe kutoa hukumu hiyo.Mtuhumiwa alijitetea kuwa anayo familia inayomtegemea katika kuwalea, isitoshe mama yake mzazi hana kazi, naye pia anamtegemea kwa kila kitu"
Kama TID ambaye ni mtuhumiwa kakiri kosa na kusema ni sababu za ulevi, sijui Ali Kiba anataka aachiwe kwa kuwa alihukumiwa isivyo halali ama ni sababu gani inayomfanya msanii aonekanaye kama kioo cha jamii kutetea maovu ambayo mtendaji ameyajutia.
Narudia niliyowahi kusema kuwa MUZIKI NI KAZI NA WASANII WANATAKIWA KUTAMBUA KUWA KWA LOLOTE WAFANYALO WANAJENGA NA AMA KUHARIBU OFISI ZAO.

Ni Changamoto tuu

No comments: