Saturday, October 18, 2008

Remembering Philips Lucky Dube.


Lucky katika onesho lake la Aug 25, 2007 Crossroads Entertainment Complex Bladensburg MD
Lucky na Back Up singers tar 25 Aug 2007 Crossroads Complex

Nilipomaliza kuangalia show yake usiku wa tarehe 25 Agosti 2007, niliwaeleza rafiki zangu kuwa sitakosa show ya Lucky Dube bila sababu ya msingi. Sababu ya kusema hivyo ni namna nilivyojivunia na kuvutiwa na onesho zima la Lucky. Kuanzia matumizi ya muda, ala, jukwaa (akiwa pamoja na back up singers wake) na hata uvaaji wao na namna alivyoiimbisha hadhira na kuifanya kuwa kitu kimoja japo ulikuwa ni mchanganyiko wa watu wa asili na imani tofauti.
Lakini wiki 7 baadae nikiwa bado nina kumbukumbu ya show ile nikapata habari za kuuawa kwake. Ilikuwa ngumu kuamini lakini ulikuwa ukweli kuwa mtu aliyetumia muda wake mwingi kupigania haki na usawa na upendo miongoni mwa jamii na kukemea maovu kama uporaji na mauaji, anajikuta akiwa mhanga wa yale aliyojaribu kuisaidia jamii kuondokana nayo.
Lucky alikuwa ASKARI anayepigania haki za kinamama na watoto, akipinga ubaguzi na ukandamizaji, akisimamia imani, kuelimisha kuhusu mfumo wa maisha upumbazao wengi, kutetea misingi ya muziki wa Reggae, Mapenzi, kuburudisha kwa hadithi za kusadikika ambazo ukweli wake upo katika jamii zetu na pia alikuwa mume kwa Zanele na baba kwa watoto wake 7. Ukisikiliza nyimbo zake nyingi, Lucky alikuwa ni msanii anayeelezea hadithi halisi tangu mwanzo wa nyimbo na unapomaliza kusikiliza wimbo unatambua alichokuwa akikisisitiza ama kukanya, ama kuelimisha. Ukisikiliza PRISON anaanza kwa kusema "somebody told me about this when i was still a little boy. He said to me crime does not pay, education is the key. As a little boy i thought i know what i was doing. But today here i am. I'm a Prisoner". Sikiliza wimbo wake wowote utaweza kuona mpangilio wa mashairi katika kueleza atakacho na hicho kilimtofautisha saana na wasanii wengine.
Sikiliza pia uhusiano wa midundo na ujumbe katika nyimbo zake utatambua kuwa alikuwa na uwezo wa kuiweka hadhira katika utayari wa kupokea ujumbe kwa mirindimo iendanayo na ujumbe katika wimbo
Lucky Dube katika miaka 25 aliyoshiriki katika sanaa hii ya muziki aliweza kutoa jumla ya albamu 23 ambazo 6 kati yazo alitoa katika mahadhi ya Mbaqanga, 1 katika mahadhi ya Afrikaans na 16 katika mahadhi ya Reggae. Ni mahadhi ya Reggae yaliyompa nafasi ya kutambulika, kuheshimika na kuelimisha jamii kwa upana wake ambako katika albamu hizo ameimba kuhusu mambo mengi yanayoathiri maisha yetu ya kila siku miongoni mwao ikiwa ni pamoja na Haki za wanawake na watoto (Hold On, Little Heros, God Bless the women), Mahusiano na Mapenzi (Romeo, Never Leave You, I've got you babe, Big Boys Dont cry, Lovers in a dangerous time, How will i know, Release Me) , Siasa (Political Games, Monster, Is This Freedom, Guns and Roses, The Way It Is, Together as one,) Maisha ya kufikirika (My World, Divorce Party,), Ubaguzi (Together as One, Trinity), Maovu (Crime and Corruptions, War and Crime, Crazy World, mfumo wa maisha upumbazao watu (Other side, Shut Up, Affirmative action, Love Me the way i am), ya kale na ya sasa (Changing world, Money Money), Imani (Take it to Jah, Shembe, Rastas,) na hata muziki ( Reggae is strong, Back to my roots, We Love It, Seriouss Reggae Bussiness).
Lucky Dube aliuawa na watu wanaodhaniwa kutaka kupora gari lake mbele ya nyumba ya nduguye alipotoka kuwapeleka wanawe usiku wa tarehe 18 Oktoba 2007. Ni kama alivyoimba katika wimbo wake wa CRIME AND CORRUPTON kuwa "do you ever worry about leaving and coming back in a coffin, with bullets in your head" ndivyo haswa ilivyokuwa hatima ya maisha yake. Kama alivyoimba katika Reggae Is Strong kuwa "Nobody can stop reggae" ndivyo kazi zake zinavyoendelea kuielimisha jamii kila kuikicha licha ya maisha yake kusimamishwa.
Kazi zake zitaendela kuburudisha, kuelimisha na kuikomboa jamii kutoka utumwa wa kiakili bila kikomo.

REST IN PEACE LUCKY

No comments: