Friday, October 24, 2008

Them, I & Them: JUSTINE KALIKAWE .......Kitendawili

Marehemu Justine Kalikawe alipotwaa tuzo ya msanii bora wa ReggaeSafari ya mwisho ya Justine, nyumbani kwake Kitendaguro Bukoba

Nikiwa na baadhi ya wasanii walioshiriki wimbo ulioitwa HAKUNA (urejee hapa). Hapa ni ndani ya Bacyadr Studio kurekodi Video ya wimbo huo uliokuwa maalum kumuenzi Justin Kalikawe

Tukiwa Idara ya Habari Maelezo (2003) na Ras Pompidou, Jah Kimbuteh, Ras Inno, Bi Georgia (Mjane wa Justine) na meneja wake wa zamani Allen Mbaga kuzungumzia Tamasha la HAKUNA lililomuenzi Justine
Jana ni kati ya siku nilizokumbuka meengi saana kuhusu nyumbani. Na ni katika kuwaza huko nikajikuta nawaza SAFARI YANGU YA MAISHA na kujiuliza msururu mzima wa matukio ya maisha yangu. Nikawaza nimetoka wapi, niko wapi na pengine ninaenda wapi. Kama ilivyo kwa wengi wetu, tunaweza kuwa na majibu ya maswali ya tulipotoka na pengine tulipo (kwa mtazamo wetu0 lakini tuendako bado ni KITENDAWILI. Na ni kitendawili hicho tunachojiuliza ambacho kina meeengi yanayohitaji muda zaidi ya tujipao katika kusaka majibu. Nilipofikiria tulikotoka na kilichonileta huku na ninavyosonga ki-umri na kuwaza mustakabali (future) ya maisha yangu na familia, nawaza mengi. Lakini ni jana hiyohiyo ambapo Kaka Gotha Irie alinitumia picha ambayo tulipiga mwaka 2003 wakati tukirekodi video ya wimbo HAKUNA wake Justine Kalikawe. Hivyo nikaenda kumsikiliza Justine na kukutana na wimbo huu ambao nimeona nishirikiane nanyi kwa mara nyingine.

"nilikuja kutafuta ugenini, nikazoea pakawa ni nyumbani, sasa ninaelekea uzeeni, nibaki huku au nirudi nyumbani. Nilioa nikazaa na watoto, na nilipotoka kwao ni kama ndoto; lakini najiuliza siku nikirudi kwetu, niende nao au wabaki huku"
Hayo ni maneno anayoanza nayo mwanamuziki aliyepata kufanya vema saana katika miondoko ya Reggae nchini Tanzania Marehemu Justine Kalikawe katika wimbo wake Kitendawili. Kama ilivyo kwa nyimbo nyingi ambazo zinakuwa na UJUMBE HALISI wa maisha kwa hadhira, wimbo huu bado unaendelea kuwa na maana na mguso uleule kwa wale walio mbali na nyumbani na hasa wale walioanzisha familia ambapo ikifika suala la maisha baada ya kustaafu unarejea kujiuliza kama alivyojiuliza Kalikawe.
Haijalishi alitunga wimbo huu akiwa wapi, ama akijifikiria kama aliye wapi, lakini kwa kuwa alifanya kile afanyacho vema zaidi kwa kutunga nyimbo zenye uhalisia kwa jamii, bado sasa hivi ndugu wengi tulio mbali na nyumbani tukiusikiliza wimbo huu tunapata hisia halisi ya alichoeleza Justine na kuweza kujiuliza maswali ambayo naye aliuliza kwenye utunzi wake huu, bado ujumbe wake unawagusa wengi ambao kwa bahati mbaya kutokana na mfumo wa maisha ya sasa wameelekea popote duniani kwa namna yoyote kusaka chochote ili kuweza kurejesha uwekezaji nyumbani, na kama ilivyo kwa binadamu yoyote, unapofika mahali ndio unapoanzisha urafiki na "udugu" na uliokutana nao, na wakati muafaka ukifika unaanzisha familia na kwa majaaliwa ya Mungu unapopata watoto inakuwa baraka, lakini baadae waweza kujiuliza kama aliyojiuliza Kalikawe kuwa "nilikotoka niliishi na wazazi, babu na bibi, mjomba na shangazi, lakini huku mimi na familia, ndugu wengine ni eneo la kazi eeeee; katikati kuna bahari, tena ni mbali elfu kumi maili, nikisafiri nafika alfajiri tena ni mbali natumia utajiri eee"
Sijui la kusema, lakini namkumbuka Justine kama moja ya nguzo za muziki wa Reggae mkoani Kagera na Tanzania kwa ujumla. Alitumia lugha zake za Kihaya na Kiswahili kufikisha ujumbe aliokusudia kwa jamii husika na mara zote ALIELIMISHA, AKIBURUDISHA NA AMA KUIFUNZA JAMII KUJIKOMBOA KUTOKA KATIKA UTUMWA WA KIAKILI.
Justine alifariki ghafla mwezi wa nane mwaka 2003 katika Hospitali Kuu ya Mkoa wa Kagera mjini Bukoba miezi michache baada ya kurejea kutoka ziara ya kimuziki nchini Denmark. Aliacha mjane Georgia na watoto wawili Abayo na Niwe na mpaka mauti yanamkuta alikuwa ndiye msanii mwenye albamu nyingi zaidi za Reggae nchini Tanzania (8 za audio na 3 za video katika miaka 16 aliyodumu katika muziki wa Reggae). Katika kumuenzi, wasanii nyota wa Reggae nchini walitunga wimbo wa HAKUNA na kuandaa Tamasha maalum la kuenzi kazi na maisha ya Justine lililofanyika Don Bosco. Tulishapata kujadili FIKRA PEVU / MAONO ya Justine Kalikawe katika wimbo wa HAKUNA kwa kuhusisha na uchaguzi ujao HAPA
RIP Justine Kalikawe
Bofya player kusikiliza KITENDAWILI hiki


2 comments:

EDWIN NDAKI (EDO) said...

NDUGU yangu nimependa sana uandishi wako katika blog yako.


Kila jema nakutakia siku njema endelea kulete mitazamo yako ..kazi nzuri

Mzee wa Changamoto said...

Thanx alot Edo. Karibu sana na naamini tuko pamoja katika changamoto zetu hizi.
Blessings