Thursday, February 19, 2009

Kilichomliza Waziri Mkuu ni kipi? Na waliomliza wanafanya nini?

(Bofya hapa kwa Taswira. ONYO. INATISHA )
Nafikiria saana jinsi HAKI ZA BINADAMU zinavyowakingia kifua wale ambao kwa namna moja ama nyingine wameamua kuzivuruga haki hizo kukamilisha nia na matakwa yao. Na si matakwa yao tuu, bali matakwa hayo yanajumuisha kutoa uhai wa wengine kwa sababu za kishirikina.
Na hapa nazungumzia mauaji ya albino (Bofya hapa kusoma ama hapa kwa kali zaidi ) ambayo yanaendelea kushamiri nchini kiasi cha kuonesha wasiwasi wa utekeleza wa ukomeshaji wake kwa njia ya sheria. Ndugu zetu hawa wanauawa kikatili, wanapoteza viungo vyao na kuishi maisha ya hofu kwa kuwa tu wamezaliwa katika hali waliyozaliwa nayo. Wanakuwa wahanga wa matatizo ya imani potofu kwa kuwa tu hawakuwa na uchaguzi wa vipi ama ni aina gani ya ngozi wawe nayo na hata ni ulemavu gani wasiwe nao. Bado imani za kishirikina zinaonekana kuwabagua na kuwatala.
Nakumbuka Waziri Mkuu alipowahi kutoa "suluhisho" kuwa wanaofanya hivyo wakikamatwa wauawe ikawa shughuli. Na mimi pia sikutegemea kama angeweza kutoa onyo la namna ile na sikudhani kama lilikuwa muafaka kwa wakati ule. LAKINI NASIKITIKA SAANA kuona tuliokuwa tukidhani twatakiwa kuongozwa na utawala wa sheria tunaona ukishindwa kufanya kazi yake na watu wenye ulemavu huu wakipukutika kila siku. Kwanini mtu afikie hatua ya kuua mtu kwa kumkatakata na kuondoka na vipande vyake? Ni nini yule anayeuawa anakuwa akisema wakati akikatwa? Anaomba asiuawe? Anaomba asamehewe? Anaomba sala ya mwisho akijua kuwa wakati wake umefika?
Nakumbuka Martin Luther King aliwahi kusema kuwa "human beings are capable of calculated cruelty as no other animal can practice" na sasa tunaona namna watu wanaojua kuwa si haki kuua wenzetu wakifanya hivyo tena kwa makusudi na lengo la kujinufaisha. Tumeshuhudia Smba anayekula mtu akidhani ni chakula chake akiuawa na wananchi kujipongeza, lakini mtu anayetambua kuwa sheria na imani haimruhusu kuua, anafanya hivyo na anaendelea kukata mitaa.
Pengine kilichokuwa kinamliza Waziri Mkuu si tulichodhania. Pengine kilichomliza Waziri Mkuu ni kile kinilizacho sasa. Pengine Waziri Mkuu alilia kwa kuwa aliona namna watu wasivyotambua machungu yaliyo katika mioyo ya wenzetu ambao licha ya kuondokewa na ndugu zao, wamebaki na taswira za ajabu na kutisha na pia hofu inayotanda kila sekunde za maisha yao.
KWANI WAO WANA KOSA GANI? KUWA KATIKA ANGUKO LA KIMAUMBILE kuzaliwa na mapungufu hayo ya ulemavu wa ngozi?
Sidhani kama Waziri Mkuu anaweza kurejea alichosema, lakini nadhani waliompinga na kumfanya alie mbele ya bunge wana wajibu wa kuja mbele na kusema ni kipi wanachofanya kuahidi kukomeshwa kwa mauaji haya. Kwa maneno mengine ni kuwa kama wanatetea haki za binadamu za wale ambao wanazivunja na kudhamiria kuendelea kufanya hivyo, basi kuna haja ya wao KUWAJIBISHWA.
MAUAJI YA ALBINO NI YA KUPIGWA VITA KWA NAMNA ZOTE.

NAMAANISHA ZOTE

1 comment:

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Mulangira. Hata mimi hizo picha zimenisikitisha saaaana! Watanzania tunaelekea wapi lakini? Ni nini kilichotufikisha hapa? Ni umasikini, ujinga, wendawazimi - ni nini? Watu wanaofanya unyama kama huu wakikamatwa wanapewa adhabu gani? Je, mbali na kulia, serikali imefanya nini? Waziri wa mambo ya ndani (naamini misukosuko yake ya kupigania vitambulisho vya taifa) sasa imeshaisha, anayaonaje mambo haya? Huu ni wakati ambapo wananchi wenyewe inabidi waamke na kusema sasa yatosha. Nilisoma Sengerema na picha hizi zimenishtua na kunisikitisha sana. Binadamu - kwa jina la kisayansi eti HOMO SAPIENS!!!