Tuesday, February 10, 2009

Tanzania yangu niipendayo. Barabarani

Kama kuna miundombinu muhimu katika nchi (na pengine niseme nchi nyingi duniani) ni barabara. Hiki ni chanzo cha mawasiliano, chanzo cha mahusiano na hata mzunguko wa pesa katika nchi nyingi na hasa zinazoendelea unategemea zaidi aina hii ya miundombinu ambayo ni Barabara.

Ukweli huu unajidhihirisha nchini Tanzania ambapo barabara ni njia kuu ya usafiri kwa walio wengi. Ni namna ya kutumia katika kusafiri kwenda kujuliana hali, kufanya tafiti, kusambaza huduma mbalimbali kama za afya, kusambaza mazao na biashara na kugusa maisha ya walio wengi iwe ni kwa maombi ama mahubiri ama kuwajulia hali ama hata wanasiasa wanaokwenda kueleza nia zao za kutaka kuchaguliwa. Na pengine ndio njia pekee ya usafiri ambayo kila mwananchi wa Tanzania atakwambia kuwa ameshawahi kuitumia.

Lakini bado umuhimu wake hauonekani miongoni mwa viongozi wetu. Wameamua kuukana ukweli wa manufaa yake na wameamua kutokubali kuwa kuboresha barabara ni njia kuu ya kuboresha maisha maisha ya kujitegemea ya watanzania walio wengi. Bado hawaonekani kukubali ukweli kuwa wakiwekeza kwenye miundombinu kama barabara kutawawezesha wananchi kujiweza katika biashara na kilimo, katika kusambaza huduma mbalimbali na hata kupunguza tamaa ya wengi kukimbilia mijini

Nakumbuka mwanzoni mwa miaka ya 2000 serikali ilisamehe kodi kwa wananchi. Hii ilionekana kama jambo bora maana watu walikuwa wakikimbizana na mgambo na wengine kuvunjika na hata kufa kwa ajili ya kukwepa kukamatwa kwa kukosa kulipa Shs 5,000 za kodi. Msamaha ulipambwa na ukaonekana wawafaa wananchi. Mwaka 2003 nikabahatika kwenda wilaya ya Karagwe mkoani Kagera ambapo pia nilipata bahati ya kuhoji watu (kwa ajili ya kipindi cha Kazi kilichokuwa kikirushwa na Redio Times Fm) na kwa mshangao wangu na wa wengi nikakutana na kilio ambacho sikutegemea.

Watu walinionesha rundo la ndizi ziiviazo maeneo ya gulio kwa kuwa hakuna hata wa kubadilishana nao kwa paketi ya chumvi ya sh 50/= na kwa kuwa kuna nyingine zinazoiva shambani basi hakuna haja ya kurejesha hizo maana ni "kazi mara mbili". Nilipouliza sababu ya yote wakasema MVUA ZIMEANZA NA BARABARA HAZIPITIKI

Walichoniambia ni kuwa kama Dar mkungu unauzwa makumi ya maelfu na wao wanashindwa kupata hata wa kubadilishana naye kwa chumvi, basi hata msamaha wa kodi haufai. Wao (na mimi pia) tuliamini kuwa wa kama barabara zingekuwa nzuri, ina maana wangeweza kuuza bidhaa, kupata pesa, kununua chumvi na mengine wahitajiyo na hata kama kodi ingekuwa Sh 10,000 wangeweza kumudu. Nikaona kweli barabara mbaya ni kero.

Lakini nikakumbuka mara nyingi na tumekuwa tukishuhudia kilio cha wenye barabara mbovu na nzuri na vyote ni juu ya uhai. Unakumbuka El Nino ilipotenganisha mawasiliano ya nchi na hasa barabara na ni wakati huo ambako watu walikuwa wanaozewa na mazao yao ghalani ilhali wengine wanakufa kwa njaa. KISAAA?? Mawasiliano na hasa barabara

Kisha nikakumbuka "utamu" wa barabara nzuri ulivyo mchungu kwa wengine maana kila kukicha wanaona wenzao wanavyopukutika kwa ajali zitokanazo na uzembe wa madereva wanaokimbiza magari kuliko kawaida kwa kuwa tu BARABARA INARUHUSU.

Ni barabara hizo hizo ambazo kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu zimeshakatisha maisha ya mamia ya watu katika ajali ambazo zinasikitisha hata kuangalia taswira zake.

Na viongozi wetu KAMA KAWAIDA YAO WANATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI, WANATOA MAAGIZO WASIYOFUATILIA na KISHA WANASONGA kama hakuna lililotokea.

Ni wakati wa kuamka, ni wakati wa kujali maisha ya wasioweza kuendesha maisha yao kwa kuwa barabara ni mbaya na kutetea na kuokoa uhai wa wale wanaopoteza maisha kwa kuwa
barabara ni nzuri

Rise Up, Wise Up, Wake Up and Shake Up

No comments: