Monday, March 9, 2009

Kizazi kipya. Kizazi kinachorithishwa ushujaa wa ujinga na kashfa

Shuleni tumesoma makala ya mchunguzi na mwandishi Peter Gibbon aliyoiita "End of Admiration: The Media and The Loss of Heroes" ambayo alisema kuwa kizazi cha sasa kimeweka kando heshima kwa mashujaa na kutukuza mambo na watu wa ajabu watendayo mengi yasiyoinufaisha jamii. Amezungumza juu ya vyombo vya habari vinavyochangia kutothaminisha mashujaa na kuendekeza kuwatukuza nyota wanaofanya mambo yasiyofaa jamii.
Japo swali laweza kuwa NANI AFAAYE KUITWA SHIJAA, na japo naamini kuwa shujaa huonekana na kuthaminiwa kulingana na jamii, bado naamini katika alilosema Bwn Gibbon. Hata kwa ushujaa na mashujaa wa sehemu mbalimbali, bado twaona baadhi ya vyombo vya habari yakiwemo "majamvi" yetu haya "yanavyoenda nje ya ukawaida na majukumu yake" na kuandika habari za ajabu ambazo zitaweza kuwapa "attention" ya wengi.
Siku hizi habari ya mpiganaji anayetetea haki za wanyonge, haina maana kama ilivyo ya nyota aliyefanya upuuzi na kupelekwa jela.
Habari ya mwelimishaji anayekwenda kuielimisha jamii kuhusu mambo mbalimbali yaisibuyo jamii hiyo haipewi uzito kama ambavyo atakuwa supastaa fulani anayedhaniwa kuchukua mke wa mtu.
Hoja za waelimishaji kuhusu namna ya kuishi katika uchumi huu unaoyumba hazionekani kuwa za maana kuliko za "concert" ya msanii fulani mahala fulani.
Siku hizi hata wasanii wanaopenda kujulikana kama "kioo cha jamii" wanapanga na kufanya yasiyotendeka ili mradi waweze kuwa kwenye habari. Inasikitisha kuona sasa hivi hata watoto ambao wanatakiwa kufunzwa namna njema za kufanikiwa wanaona kuwa ujinga na kashfa ni njia ya mkato ya mafanikio (hasa kwa wale wanaotafsiri mafanikio kama kuandikwa kwenye magazeti na kuonekana kwenye vyombo vya habari)
Na katika kudhihirisha hili, unaweza kuona kuwa hata wasanii wanaanza kujiingiza katika uimbaji wa nyimbo za ajabu zenye kuwawezesha kujibizana hali itakayowapa "air time" ambayo inawapatia maonesho na "interviews" nyingi na kuwafanya wawe wanavyotaka kuwa.
Cha kujiuliza ni kuwa ni nini twarithisha wanetu juu ya ujasiri na ushujaa?
Ni kwanini wale maBIBI na maBABU wanaoachiwa watoto na watoto wao wasionekane mashujaa kwa yale watendayo?
Vipi kuhusu wale ambao kwa moyo mweupe wanasaidia kufanya kazi ngumu kufanikisha usalama na uhai wetu?
Na wale ambao kwa mshahara mdogo na ambao unachelewa kila mwezi bado wanaendelea kutuelimisha mashuleni na kututibu mahospitalini?
Na wale ambao kupitia nafasi na taaluma walizonazo wanajitolea bila kikomo kuwekeza katika kuwasaidia wengine ili nao wawe msaada kwa jamii nzima?
HAWA HAWAONEKANI, HAWAANDIKWI NA WENGI HAWATHAMINIKI jambo ambalo sio tu lasikitisha, bali laonesha ni nini twajitahidi kufanya na kizazi cha aina gani twataka kuwa nacho.
Ni kweli twaelekea kwenye kizazi kipya alichozungumzia Kaka Kissima ambacho hakina utambuzi wa Mashujaa halisi waliotenda na kuishi kwa utaratibu wa P.U.G.U ambao Kaka Makulilo Jr amekuwa akiuhimiza mara zote. Kizazi cha sasa kinakueleza wazi juu ya umuhimu wa kusoma ili urejee nyumbani "kufisadi" kwa namna nafasi yako itakavyokuruhusu.
Tunaona tofauti kubwa ya namna ufujaji na ukatili ulivyoongezeka miaka ya karibuni na kushuka kwa heshima na thamani ya mashujaa wetu wengi ambao walijitolea kwa hali na mali kutenda yaliyo mema kwa jamii na sasa wanataabika bila hata uwezo wa matibabu. Tumeona baadhi ya watumishi waliolitumikia taifa katika awamu ya kwanza wakiendesha maisha yao kwa taabu na hawa ndio waliojitolea kuwezesha kuwa tulipo na kujinyimba licha ya nafasi walizokuwa nazo wakati huo kufanya ufujaji. Lakini hakuna ajaliye hali zao, bali kila siku ni habari za mfujaji fulani anayedhuria mahakama kwa ufujaji aliofanya na hakuna wa kumjali SHUJAA anayeganga njaa huko kijijini. Na kizazi chaiga nini cha kufanya kuepuka aibu iwakumbao hawa MASHUJAA WETU WA KWELI
Hiki ni kizazi chetu. Kizazi kipya. Kizazi kinachorithishwa ushujaa wa ujinga na kashfa badala ya kutenda yaliyo mema na yaifaayo jamii
Labda tumsikie Lucky Dube alivyowapa heshima mashujaa katika wimbo wake Hero




3 comments:

Jimy said...

You are right kabisa. Tupo pamoja kaka!

Putri Erdisa Januarti said...

hey you know! i really love your subtitle! could i copy it to my blog? :D

nyahbingi worrior. said...

samahani fungua kurasa ya kuchangia mawazo kuhusu jumuiya ya wanablogu tanzania.

http://blogutanzania.blogspot.com/

www.ringojr.wordpress.com