Tuesday, March 17, 2009

Ni kweli kuwa twawaandaa vema wazazi watarajiwa?

Nikiwa nyumbani nakumbuka kusikia juu ya habari za watu kupata matatizo ya ujauzito kutoka kwa kile kilichoaminika kuwa "kutopatana kwa damu". Hiyo haikuwa mbaya zaidi kama ile ambayo watu walihisi "wanarogwa" na ndio maana ama mimba zinatoka ama watoto wanazaliwa na kasoro. Hali ilizidi kutisha pale ambapo mzazi mmoja ama wa upande mmoja kutokubaliana na uamuzi wa wenza fulani kuwa pamoja, na ambao baada ya kuamua kuwa pamoja wanajikuta wakipata matatizo ya kizazi, uzazi ama uzao wao na kwa imani potofu wanahisi ni yule aliyewakataa anayesababisha hayo.
Katika harakati za ukuaji kimaisha, katika kusoma hili na lile na kuelimika kuelekea maisha mengine, nimekutana na somo kuhusu damu na ndani yake kukawa na hii topiki kuhusu RH. Japo si mtabibu na wala sielewi mengi kuhusu utabibu, nimeona niwasilishe hapa kibarazani kuondoa utata wa kile ambacho hutokea pale ambapo mwanamke mwenye damu yenye u-hasi wa Rh (RH Negative) anapobeba mtoto mwenye damu zeny RH Positive na madhara yake.
Nimeisoma na kugundua kuwa ni kati ya mada ambazo kama zingeweza kuelezwa vema kwa wazazi watarajiwa nyumbani na kwingine kote, wakaelezwa hatari na namna ya kujikinga na ama kupunguza uwezekano wa athari zake, basi tusingeishia kuwa na familia zenye watoto wenye utegemezi na ama kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na mchanganyiko huu wa damu.
Japo kuzuia watu kutokuwa pamoja kwa kuwa tu damu zao zinaweza kuleta uzazi wenye ukinzani baina ya mama na mtoto ni kitu ambacho kinaweza kisiwezekane, lakini kupunguza idadi ya waathirika wa tatizo hilo kwa ku-limit uzazo mmoja (ambao kwa mujibu wa wataalam unakuwa na nafasi ndogo ya kuathiriwa na tatizo hili) kunaweza kuwa msaada mkubwa kwa kinamama.
Naamini watabibu wetu kina Da Subi, Dr Baraza na wengine wanaweza kunyambulisha mengi kwa undani zaidi kulingana na hali ilivyo. Na kwa wewe mwenzangu na mimi waweza kujisomea kwa undani kwa kubofya hapa.
Twatambua kuwa kuna mambo yanayozuilika na mengi yanaweza kueleweka kwa jamii kama wahusika watakuwa wameelimishwa na kuandaliwa vema. Hili laweza kupunguza "kushikana uchawi" pamoja na mengine mengi yanayoweza kuleta MPASUKO katika familia na jamii kwa ujumla. Na haya yote yataweza kuepukika ikiwa tu tutawaandaa vema wazazi watarajiwa. Na ndio maana nikajiuliza kuwa NI KWELI KUWA TWAWAANDAA VEMA WAZAZI WATARAJIWA? Maana kwa kufanya hivyo tutaokoa maisha na uhusiano baina ya jamii.
Amani kwenu

2 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Nakubaliana nawe kwa sisi waafrika kila jambo linapokwenda kama isivyotakiwa basi inakuwa/semekana ni ushirikina yaani amerogwa. Kwa hiyo ni kweli akina mama watarajiwa inabidi waandaliwe na pia ikibidi si akina mama tu hata akina baba watarajiwe inabidi wawekwe mstari wa mbele.

Mzee wa Changamoto said...

Na ndio maana nikasema wazazi watarajiwa. Nikimaanisha wote kinamama na kinababa waelezwe hali ilivyo, athari na hatari za kufanya wafanyacho na namna ya kuweza kuzuia matatizo kama yapo.
Asante Da Yasinta