Wednesday, April 8, 2009

Huwezi kuwashukuru wote, waombee tu!!!


Nakumbuka niliwahi kuandika na kuuliza kama umemshukuru ama kumuombea adui yako (bofya hapa kuirejea) na lengo hasa lilikuwa kuonesha ama kukumbushana umuhimu wa mitazamo yetu.
Namna ambavyo mtu unayeamini anaweza kuwa adui yako alivyo na nafasi kubwa katika kukuendeleza.
Unadhani ni wangapi wanajitahidi kuwa makini waandikapo makala / matoleo yao bloguni wakihofia kuna "watakaowaponda?"
Hudhani kama hiyo ni nafasi chanya iliyochezwa na woga wa yule ambaye anaweza kuwa kama adui kwako?
 Ni katika hali hiyohiyo ninapopenda kusema kuwa ukiangalia jinsi binadamu tutegemeanavyo, utashangaa kujua undani wa waliokuwezesha kuwa hapo ulipo. Na mara nyingi wanaokuwezesha ni wale ambao wewe huwajui na kuna uwezekano pia kuwa wakawa watu ambao hawakukutakia mema katika hilo.
Mfano ni pale ambapo mimi ninapojua kitu kinachonifanya niweze kuishi na kusaidia wengine, lakini nilijifunza kitu / kazi hiyo toka kwa mtu. Na mtu huyo amejua vema na kuweza kunifunza kwa kuwa alijifunza mwenyewe na kwa taabu na sababu ya yeye kufanya hivyo ni kwa kuwa waliokuwa kwenye nafasi ya kumfunza walikataa kufanya hivyo kwa sababu wazijuazo wao.
Pengine hujui hilo, lakini unajifunza vema toka kwa yule aliyeamua kujifundisha kukwepa kadhia za "maadui" zake.
Hata malezi na maisha kwa ujumla yako hivyo. Wazazi wanawalea watoto maisha wanayosema "sitaki apitie nilikopitia". Huko alikopitia pengine alipitishwa na waliokuwa wakimtakia mabaya, lakini akaweza kujikwamua na sasa anakupa njia muafaka. Hivi waliompitisha huko mzazi wako ni wa kushukuriwa pia?
Kuna watu wamependa ku-blog kwa kuwa wamevutiwa na baadhi ya blogs, lakini wenye blogs hizo walianzisha kwa kuwa hawakupata nafasi ya kutosha kueleza hisia zao kwenye sehemu nyingine, kisha wakajifungulia njia huko ulikopenda wewe.

Hebu fikiria kama utaanza kumshukuru kila aliyekuwezesha kufikia hapo ulipo, utaweza kutaja wangapi? Na hao uwatajao wamezeweshwa na nani na nani na nani?
Kwangu suluhisho ni kutojaribu kuwataja wote maana hutowakumbuka. WAOMBEE TU!!!

2 comments:

Unknown said...

Kaka Nimepita kuchota hekima zako.
Ahsante kwa ujumbe maridhawa.

Yasinta Ngonyani said...

amen! Ujumbe mzuri sana Asante