Thursday, April 9, 2009

Labda sisi si maskiniUMASKINI; ni neno nisilopenda kutumia kwa kuwa laonekana kutimiza matakwa ya wanaolisema kuendelea kutudharau na kutudhalilisha. Ninaona hivyo kwa kuwa tunakuwa maskini pale tusipokuwa na kile walichonacho, na wao wanakuwa wahitaji pale wanapokosa tulichonacho ambacho wanakihitaji. Kwa bahati mbaya hata viongozi wetu wanapokutana na hao ma-global sheriffs wanapandikizwa mbegu hizi za kujidhalilisha na kujidharau na bila kujua wanarejea nazo na kuendeleza propaganda za wakandamizaji hawa.
Kaka Msangi Jr aliuliza kwa Da Koero kuwa kwanini wafanyabiashara wa kizalendo wanaitwa wajasiriamali wakati watokao nje wanaitwa wawekezaji? Pia Kaka Matondo aliwahi kuuliza kuwa TUTATUKUZA VYA WENGINE NA KUDHARAU VYA KWETU MPAKA LINI? Na hata Kaka Kamala pia amekuwa akizungumzia saana tatizo la watu kutoitambua nguvu iliyo ndani mwao na kuendekeza kila kitokacho nje ya wewe na kudhani kitakupa amani utakayo.
Dunia sasa iko kikaangoni. Uchumi umeporomoka kila mahala na kila mwenye uwezo wa kumnyooshea mwenzake kidole anafanya hivyo. Wengi wanasema kuwa kuporomoka kwa uchumi duniani ni kutokana na kuanguka kwa uchumi wa Marekani. YAONEKANA KUKUBALIKA KWA WENGI lakini najiuliza hivi ni kiasi gani cha utendaji kazi kinahitajika ili kuifanya nchi kama Marekani isitetereke? Kwa sasa kiwango cha wasio na ajira kimepita 8% ambayo inaonekana kuiathiri saana nchi. Hapo ina maana kuwa zaidi ya 91% bado wana kazi na nchi inahaha kujaza nafasi za kazi. Nimesaka takwimu za Tanzania lakini hakuna nizipatapo japo hata nilizozipata zinaonesha kuwa hali ni mbaya zaidi. BOFYA HAPA KUZISOMA.
Ninafikiria kama na Tanzania ingekuwa na kiasi hiki kidogo cha ukosefu wa ajira tungekuwa wapi? Kwanini haya matatizo yasiwe funzo kwetu kuwa wenzetu tunaowaona wameendelea wanafanya kazi kuhakikisha wananchi wao wanakuwa na ajira na kiwango cha kazi kinakuwa kikubwa ambacho kitasababisha mzunguko mkubwa wa pesa na kuimarisha uchumi? Hebu fikiri kama namba za takwimu hizo zingegeuzwa na za Marekani zikawa za Tanzania na za Tanzania zikawa za Marekani, kungekalika? Unadhani nchi na ulimwengu ungekuwa kama vilivyo?
TATIZO
Ni kwamba viongozi (ama niseme watawala) i wabunifu. Wnatoa ahadi ambazo wanajua fika kuwa hazitimiliki.
Wananchi hawaonekani kuwa na subira na pia imani na mipango yoyote isiyotimilika ndani ya muda mfupi.
Viongozi hawaonekani kujali matatizo halisi ya wananchi na wawekezaji ambayo hayaonekani machoni pa wengi (kama mifumo ya maji na majitaka) ambayo ikiwa ya uhakika kunakuwa na mfumo bora zaidi wa maisha
Njaa na urho vinawagawa na kuwaathiri wananchi ambao husikiliza na kufuata kila waambiwacho na wale waliopewa "uchache" na wagombea.
TUJIULIZE
Tuna rasilimali ngapi ambazo zikisimamiwa vema zinaweza kuwa MKOMBOZI kwa jamii?
Rasilimali hizo zina thamani gani na thamani hiyo ni sawa na sehemu gani ya hitaji la bajeti ya serikali kwa mwananchi?
Zinatumika vipi na kwa uwazi kiasi gani? Kama huna kichefuchefu cha haraka soma taarifa hii juu ya kiasi wanachovuna na kile wanacholipia kodi kwa kubofya hapa
Tujiulize kuwa viongozi wetu wamejitoa vipi kwa jamii wanazozitumikia?
Tujiulize kuna usawa na uwazi kiasi gani katika kuyashughulikia matatizo na mikataba ya nchi yetu kwa manufaa ya wananchi walipo sehemu husika?
TUNA RASILIMALI NYINGI AMBAZO ZIKIPANGWA NA KUSIMAMIWA SAWASAWA, TUTAWEZA KUWA MBALI ZAIDI YA HAPA TULIPO.
Nikitazama yote najikuta nikiamini kuwa labda sisi si maskini, bali "tunamaskinishwa" na wenye umaskini wa fikra.
Labda wako chini na hawaoni haya, tukiwapandisha mlima Kilimanjaro wataona aliyoona Innocent Galinoma, pengine watabadili mtazamo wao na kuisaidia jamii iliyowachagua. Msikilize

Tuonane "Next Ijayo"

5 comments:

Koero Mkundi said...

Nilisoma habari ya yule mtoto wa malawi aliyeasiliwa na Mwanamuziki Madona, alipomuuliza baba yake wa kumzaa kwamba kwa nini yeye ni masikini?

Kumbe hata watoto wanweza kumuangalia mtu na kujua kuwa mtu huyo yuko kwenye lindi la Ulitima?

Siosi sio masikini rasilimali kwani mungu katujaalia kuana na rasilimali za kutosha kabisa bali tunao viongozi ambaoni masikini wa mwisho kabisa katika kufikiri......
Wakati mwingine naona haya kujivunia Utanzania...

Mzee wa Taratibu said...

Umasikini si kilema matatizo ya dunia, Kuna watu unawakuta masikini kwa siku anapata chakula mara moja tu lakini inatokea bahati nzuri akatajirika ghafla yote hayo ni uwezo mungu.

Fadhy Mtanga said...

Umasikini?
La hasha!
Sisi siyo masikini kaka. Ila tunalazimishwa kuwa hivyo na wale wenye maneno matamu kila baada ya miaka mitano. Ambao baada ya sisi kukaa kutwa nzima katika foleni ndefu ya kuwapigia kura, huanza kuonja pepo ya duniani.
Kama rasilimali zilizopo nchini mwetu (Mungu hapendi tuwe masikini nd'o maana nchi imebarikiwa) zingetumika kwa maslahi ya taifa unadhani tungekuwa hapa?
Kama sekta ya kilimo ingetiliwa mkazo na kupewa kipaumbele, watu wangekumbwa na njaa? Wakati mwingine viongozi wafike pahala waone aibu. Kwa nchi yenye mvua ya kutosha na ardhi ya kutosha yenye rutuba bado tunaimba umasikini! Wanaotutazama lazima watushangae kisha watucheke.
Vipi sekta ya madini? Wanataka watuite masikini kwa kusaini kwao mikataba mibovu!
Hivi kweli inaingia akilini?
Mi nadhani wenzetu waomba kura hawana shida ya kuendeleza nchi. Lucky Dube katika Rastaman's prayer aliimba kuwa hata viongozi wa kisiasa humshukuru Mungu kwa kuwawezesha kulidanganya taifa hata linapolia wakiwa na nyuso kavu.
Nao wanaimba umasikini wakiwa na nyuso kavu ili tuamini 'sisi ni masikini'
La hasha!
Ni hayo tu!

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

siku hizi sipendelei sana kusoma habari zozote zinye harufu ya kisiasa ziwe za kitaifa, kimataifa na hta za kifamilia kwani zinakujaza wazimu na hasira juu ya ujinga ufanyiikao. nimeacha hata kusoma magazeti yakisiasa nikaingia kwenye kujitambua zaidi na zaidi.

mtu ambaye anaisha kwa kuutukuza mwili wake badala ya roho daima atafanya maamuzi ya kichizi na wazimu. yule anayetanguliza au kutawaliwa na roho atafanya vitu vya akili baada ya kugundua kuwa mwili si chochote si lolote utaishia pafupi tu!

ukiangalia ujinga wa binadamu na mali utacheka mpaka ufe kama una macho ya kuona.

labda nyie ni masikini.

watanzania wanakazi japo hazijasajiliwa.

msifagilie sana vitu vya duniani bwana sisi ni matajir wa kutosha kwa sababu bado tunaishi na tuuuaendelea kuishi

Unknown said...

Nimewahi kusema kuwa, kila mtu anvuna alichopanda hapa duniani.
sisi tumepanda umasikini na sasa tunavuna umasikini.
Tahitaji tafakuri kubwa kuukubali ukweli huu.
Lakini ukweli ni kwamba tumejitakia wenyewe umasikini, tumepewa macho hatuoni, tumepewa masikio hatusikii na tumejaaliwa akili lakini hatuzitumii.
sasa tunamlaumu nani?