Sunday, April 5, 2009

Ni mbegu ndogo iletayo mazao makubwa

Ni kawaida kwa mwanadamu kufikiria pale alipoanguka na kushindwa kufanikisha ndoto zake. Na mbaya zaidi ni pale tuamuapo kuwa maisha yetu na ya wenzetu yamefika kikomo kwa kuwa tu hatujatimiza tuliyotaka kutimiza katika muda tuliojipangia. Na hili hutokea kwa kuwa kila binadamu ana ndoto ambazo angependa kuzitimiza, lakini si mara zote huwa tunatambua nafasi yetu katika kufanikisha ndoto zetu kupitia wengine. Mfano unaposhindwa kuwa na "mafanikio" utakayo, hudhani kuwa unaweza kutumia kile ulichonacho kuibadili familia, jamii na hata ulimwengu kwa ujumla?
UNAWEZA. Na hii yaweza kuwa CHANGAMOTO YETU sote kutazama nafasi pana tuliyonayo kwa jamii yetu tutakapoamua kuwa msaada kwa kila chema tulichobarikiwa nacho.
Nilikuwa nikimsoma Dr Benjanim Carlson (pichani) ambaye ni kati ya madaktari wenye heshima kubwa sana katika utabibu ulimwenguni. Ni Mkurugenzi wa upasuaji wa hospitali ya John Hopkins na pia hufanya upasuaji kutenganisha mapacha walioungana na uipasuaji wa ubongo pia. Lakini Dr Carlson ambaye kwa sasa ni tegemeo kwa wengi alipata malezi na mafunzo ya awali kumuandaa kwa nafasi aliyopo toka kwa mama yake ambaye hakujua hata kusoma na kuandika. Pengine haikuwa mipango ama malengo ya mama kuwa na familia wakati yeye hana elimu, lakini aliamua kutumia kipaji alichonacho cha ushawishi kuwafanya watoto wake wapende kusoma na kuthamini elimu na sasa mbegu hiyo iliyokuwa na elimu ndogo ndio iliyozaa matunda haya makubwa tuyaonayo.
Ni mfano wa kuigwa nasi sote. Tunapaswa kutambua kuwa kila mtu ana nafasi ta kumuwezesha kufanya mabadiliko ulimwenguni iwapo tutaamua kuwa na mtazamo chanya.
Msome na msikilize Dr Carson aliporekodiwa na redio ya jamii akielezea namna mama yake alivyo msingi wa maisha yake kwa kubofya hapa ama kutembelea tovuti yake kwa kubofya hapa kumsoma
Pia Kaka Bwaya alishaandika maelezo ya vitabu vyake unayoweza kuyapata hapa
JUMAPILI NJEMA

6 comments:

Koero Mkundi said...

Nimefurahi kuwa kitendea kazi kilichochanvgamotolewa kimepona.
Ahsante sana kwa habari hii ya huyu Dakitari mwenye kipaji.
Kusema kweli hivi vitabu viko vipo nyumbani sema tu nimekuwa mvivu kidogo wa kusoma lakini kwa habari hii itabidi nikae chini na kuchota elimu ya huyu bwana.
Hivi hawa madakitari wetu hapa nchini, mbona wao hawaandiki?
halafu mbona hawana utaratibu wa kueleza mafanikio yao pale wanpofanikiwa kutibu ugonjwa fulani au hata kugundua tiba fulani kama wanvyofanya wenzetu?
au wamewekewa mipaka?

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Nilitazama programu nzima kumhusu katika Discovery channel/BET? na hata ile muvi ambayo nafasi yake imechezwa na Cuba Gooding Jr. ninayo katika collection yangu. Ni hadithi yenye kutia moyo na hata kuliza kutokana na makuzi na mafanikio aliyoyafikia.

Koero, madaktari wetu sidhani kama wana muda wa kukaa chini na kuandika kitabu. Wengi wako kila mahali wakihangaika kujiongezea kipato. Hata wakiandika ni nani atakayesoma vitabu vyao? Pia wataandika kwa lugha gani? Sidhani kama wanafahamu Kiswahili vizuri kuweza kuandika kitabu kinachoelezea mambo ya tiba. Na wakiandika kwa Kiingereza ndiyo kabisaaa - ni akina Koero wachache zaidi ndiyo wataweza kusoma vitabu vyao. Kazi eeh!

Koero Mkundi said...

Matondo, si wandike tu, kama ni swala la lugha tunayo Bakita na Tuki pale chuo kikuu, kazi yao ni kutafiti lugha ya kiswahili, hili nalo linawahusu.
waandike halafu ndio waseme kuwa jamanie si mnaona tumeandika saaana na kazi zetu zinaishia kwenye makabati ya maduka ya vitabu.
Swala sio lugha, swala ni ule moyo wa kutaka wengine wanufaike na maarifa waliyonayo.
mbona huyu ni Mmarekani lakini kuna watanzania wengi wansoma kazi zake........

Yasinta Ngonyani said...

Nasema kama Koero nafurahi kuwa kitendea kazi kimepona.
Hongera mama, kuwezesha watu yataka moyo.

malkiory said...

Mzee wa Changamoto,

Binafsi nimefurahi sana kwa kutufahamisha kuhusu huyu daktari bingwa wa masuala ya ubongo.

Nimejikuta nikitumia siku nzima kuangalia video mbali mbali kuhusu mambo aliyoyafanya Dk Ben. Ukitaka kumjua zaidi ingiza jina lake kwenye youtube, hapo ndipo utamjifunza vizuri.

Yeye mwenyewe amekiri kuwa watu weusi wamevumbua mengi katika hii dunia bila watu kujua hayo. Mfano traffic lights zimevumbuliwa na mtu mweusi, na mengine mengi kadhaa ambayo utayasikia kwenye video zake kwenye youtube.

Kuhusu madaktari wa Kitanzania kutoandika vitabu, nadhani wapo wachache ambao wanafanya hivyo, kwa mfano leo hii wakati nimepitia gazeti la habarileo, nilikutana na kichwa cha habari nyota ya wiki hii ni Daktari Lawrence Chipatta, kwa kweli huyo ameandika vitabu kuhusu matatizo yanayoambatana na uzazi. Kwa habari zaidi pitia hii link na utapata undani wa shughuli zake( http://www.habarileo.co.tz/wikinyota/?n=352

Mbele said...

Ni kweli, huyu bingwa ni maarufu. Nilisikia habari zake na kusoma kitabu chake kimoja miaka kama mitatu iliyopita. Habari za watu makini kama hao ndio zinahitajika katika kuwafundishia watoto wetu. Tulipokuwa tunasoma zamani, tulikuwa na vitabu vya watu maarufu kama vile akina Marie Curie. Tulipaswa kuendeleza jadi hii katika kuwafundisha na kuwahamasisha watoto wetu na kuwaunganisha hao akina Dr. Carlson na mashujaa wengine kem kem wa barani Afrika kwenyewe.

Nimeandika kijitabu kidogo kinachoonyesha mchango kihistoria wa Waafrika na wengine wenye asili ya Afrika, katika nyanja mbali mbali, kama nilivyoeleza hapa.