Kuchukia si kitu kizuri. Lakini ukweli haupingiki kuwa watu wanawachukia wenzao. Na wengine wanawachukia watu kwa kuwa wanahisi watu hao wanawachukia wao. Sijui hapo nani anatibu nini!!! Nakumbuka kusoma nukuu ya mtu mmoja ikisema "huwezi kutatua tatizo kwa kutumia njia iliyopelekea tatizo hilo kutokea." Ina maana kwa kumchukia umdhaniaye anakuchukia nawe unakuwa na chuki kama yeye. Na kwa undani zaidi ni kama vile unataka kumdhihirishia kuwa nawe unaweza na pengine unasikitika kuwa hukuanza wewe kumuonesha hivyo. Tayari umeshakuwa kama yeye.
Lakini kuna binadamu aliye sahihi katika kila atendacho? HAPANA. Hata mapacha walioungana wana tofauti japo ya fikra (na twajua kuwa fikra hufuatwa na matendo) kwa hiyo lazima tukubali kuwa hatuwezi kuwa kama kila mtu na si kila mtu anaweza kuwa kama sisi. Na Je! Kuna binadamu asiye sahihi katika kila kitu? HAPANA. Hata umuonaye si sahihi ana wafuasi wamuonaye sahihi. Ukimuona adui wengine wanamuona shujaa kwao na wanamuiga.
Sasa kama kila mtu si kamili na si kila mtu ana mapungufu kama tuyaonayo sisi (na pengine tunaona hivyo kwa kuwa tuna mapungufu kwenye sehemu hizo) unadhani wao wanatuonaje katika misimamo yetu? NAO WANATUONA TUNA MAPUNGUFU.
Sasa kama ni mtu ambaye huna nafasi yoyote ama uwezo wa namna yoyote kum'badili tabia ama mwenendo utaendelea kuumia kwa chuki ndani mwako? Si suluhu ya tatizo na pengine usipokuwa makini utajikuta unakutana na mwingine kama wa awali na kama hukujifunza kitu toka kwa huyo wa mwanzo utaendelea kuwa mhanga wa watu hao. Ni kama waibiwavyo watu kwa kuwekewa "kanyaboya" na bado hawawi makini wanapofungiwa walichonunua.
Kubwa ni kwamba kila mtu ana kitu unachoweza kujifunza toka kwake. Uwe unampenda ama unamchukia. Ni namna tunavyojijengea utashi wa kujifunza kutoka kwa watu. Na kama kuna mtu m'baya kuliko wote uliowahi kukutana nao duniani, funzo la kwanza ni kuwa "kumbe wapo wabaya zaidi ya nilivyokuwa nafikiria!?" na kuanzia hapo unaweza kuamua kujifunza kujiepusha na / kukabiliana nao.
Ukikutana na mchoyo jifunze kwamba si kila mahali utakuwa na aliye tayari kukupa.
Ukikaa na mlafi jifunze kuwa usipokuwa makini utalala na kufa njaa.
Ukimuona muuaji jifunze kuwa maisha ya binadamu hayana thamani sawa machoni pa wengi.
Ukimuona fisadi jifunze kuwa tunaweza kutafsiri tofauti neno "mali ya umma."
Na mengine mengi.
Lengo kuu hapa ni kujua kuwa kila anguko lina nafasi ya kukupa funzo la ulipoanguka na ukiamua utajifunza kuwa makini usianguke tena, na hata ikitokea ukaangua basi isiwe kwa sababu iliyokuangusha awali.
Labda ni namna nionavyo tatizo, maana namna uonavyo tatizo ......................
Jumamosi njema
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
1 comment:
Heri ya Pasaka.
Wakati mwingine mtu anaweza asikuchukie wewe bali matendo yako. Mtu huyu anakupa changamoto ya kuyaacha yale yasiyowapendeza watu.
Lakini nakubaliana kabisa kuwa binadamu wote hawajakamilika. Hivyo ni vigumu kupendwa na wote. Lakini mara nyingi hutokea kumchukia mtu uhisiye anakuchukia.
Wengine wanakuchukia kwa sababu umewakosea.
Wengine kwa sababu wazazi wako na wake ni maadui.
Wengine hata ukikosana na dada ama kaka yake.
Hao ni wale nionao chuki yao imeambukizwa na ni ya kujitakia.
Chuki ipo sana na zaidi inamea dhidi ya wale wenzetu wasiyoyajali maslahi ya wengine.
Ni hayo tu!
Post a Comment