Wednesday, August 26, 2009

Tanzania yangu...Inauza Baiskeli na kununua kengele

Kwa sisi waendesha baiskeli, msemo wa KUUZA BAISKELI ILI KUNUNUA KENGELE ulimaanisha kubadili (kwa kupoteza) kilicho muhimu na manufaa kwa kile ambacho hakiwezi kufanya kazi bila kile uuzacho. Na hili limejidhihirisha nchini mwetu. Haioneshi kuwa watawala wetu wanajua ni kipi cha kufanya ili kupata maendeleo katika kile wanachopanga. Wanazuia njia ya kuwafikisha waendako ilhali wanawapa wananchi matumaini kuwa watafika watamaniko. Tanzania yetu haijengi wala kukarabati shule na inaendelea kutuumiza masikio na UONGO kuwa tunaingia katika karne ya Sayansi na Teknolojia kwa KISHINDO na mpango ufuatao ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wanajifunza kompyuta nchi nzima. Kama hakuna majengo, hakuna madawati, hakuna walimu, hakuna vitabu, hakuna nyumba za kukaa walimu, hakuna maktaba, hakuna mkaguzi, hakuna mwenye kuonekana kukerwa na haya inakuwaje mseme mnapanga elimu kwa wote? Niliuliza swali kwenye bandiko langu juu ya SHEREHE ZA MIAKA 47 ZA UHURU (Bofya kuisoma) kuwa kama shule hizi zimejengwa ndani ya miaka 47, kuna tofauti gani kati ya wakoloni na watawala wa sasa? Na kama zina zaidi ya miaka 47, ina maana zilikuwa na hali nzuri wakati wa ukoloni kuliko sasa. Kwanini hatuwekeze katika mazingira mazuri ya kuwasomesha watoto badala ya KUWAJIBISHA KWA KUWACHAPA VIBONO WANAOPATA MATOKEO MABAYA? Mto Mzinga uliokuwa ukitiririshiwa maji yenye kemikali toka Karibu Textile cha Mbagala
Waheshimiwa wetu hawawekezi kulinda afya ya mlaji ambaye kwao ni mwananchi. Wanasema wanaleta wawekezaji ili kuinua pato la nchi na kumnufaisha mwananchi ilhali wanawaruhusu wawekezaji kumwaga sumu kwenye vyanzo vya maji wanayotumia wananchi kuvua na kunywa. Ni faida gani wanapata wananchi kama watakufa kabla hata hiyo kodi haijawafikia? Tumesikia juu ya kuuza madini na udongo wake. Yaani waondoke na kila kitu na hakuna anayejali. Hivi atakayefukia mashimo hayo atatoa wapi mchanga na kwa gharama za nani? Ni kwanini hatufikirii wananchi na mazingira badala yake tunaendekeza "kitukidogo" tunachopewa kujaza matumbo? Nikamuona Rais akitembelea vituo mbalimbali kama CISCO, Google na IBM ambapo pamoja na mambo mengine ilisemekana alielezea suala la kuja kuwekeza Tanzania. Kwa mujibu wa makala iliyoandikwa katika mtandao wa IKULU MAWASILIANO (Bofya hapa kuisoma) imedhihirisha kuwa "Kazi kubwa ya Rais Kikwete ilikuwa kuzishawishi taasisi hizo kubwa za teknolojia ya kompyuta katika nchi kiongozi wa teknolojia hiyo ya Marekani kuja kuwekeza katika uchumi na taasisi za Tanzania kwa nia ya kuifanya nchi hiyo kiongozi katika teknolojia hiyo katika Afrika." Sina hakika kama anajua kuwa KAMA UMEME HAUKATIKI IKULU, BASI PENGINE NDIO SEHEMU PEKEE ISIYO NA KADHIA HIYO kwani hatuna uhakika wa Umeme. Na kuleta makampuni makubwa kama google bila kuwa na uhakika wa umeme, kuwa na miundombinu ya kutosha, kuwa na barabara zenye (angalau) usalama kidogo, kuwa na viwanja vya ndege vinavyoweza kufikiwa na wawekezaji hao na pia mazingira mazuri ya uwekezaji ikiwemo kuondoa RUSHWA NA UFISADI ni sawa na ku-deposit LAWAMA, AIBU NA HASARA kwa wawekezaji endapo watashindwa kufanya kazi zao kutokana na mapungufu hayo
Tumeshuhudia mapokezi ya Hasheem Thabeet. Mchezaji anayestahili mapokeo ya namna hiyo (kwa mtazamo wangu) lakini si kutoka kwa serikali ambayo haijafanya lolote kufufua michezo mashuleni. Sote tunajua kuwa Hashimu amefika alipo kwa mgongo wa elimu na tunapoangalia michuano ya kimataifa tunaona namna ambavyo nchi kama Barbados (yenye wakazi wakaribiao 300,000) inavyong'ara kwa kuwa iliendeleza wachezaji wake kielimu wakapata scholarship nje na kushiriki michuano yenye ngazi za kimataifa na wakirejea wanakuwa katika kiwango cha ushindi. Leo hatutaki UMI-YOYOTE (iwe Umishumta ama Umiseta ama Umisavusta) lakini tunataka nyota kama Hashimu. Ni kutamani mbinguni bila kutaka kufa.Labda mimi ni kati ya wachache wanaoamini kuwa Uwanja wa Taifa ni UTANI kwa jamii ya Tanzania. Uko pale na umegharimu mamilioni na bado utagharimu mamilioni ilhali hauwezi kutufikisha popote kwa kuwa hakuna utaratibu wa kuendeleza wacheza soka toka umri mdogo. Ni kweli kuwa tunategemea watu wajifunze soka baada ya elimu ya sekondari ama vyuo na kisha watuwezeshe kushiriki vema na kuutumia vilivyo uwanja wa Taifa?. Hivi pesa hizo zingejenga kumbi ngapi za kisasa maalumu kwa kuonesha matamasha na burudani za asili, ama hata Sanaa za Jukwaani ama Muziki wa Dansi na hata hiyo Bongo fleva mbavyo Tanzania tunaweza kujivunia kuwa tunafanya vyema zaidi ya soka? Tumeacha kujenga na hatujengi vinavyojenga jamii na kuendekeza vinavyotugharimu ambavyo haviwezi kutufikisha popote kama hatuviambatanishi na vile tunavyopuuza na ndio maana naisikitikia TANZANIA YANGU kwani INAUZA BAISKELI NA KUNUNUA KENGELE.

8 comments:

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

sijui niilaumu serikali au wanaoichagua serikali hiyo?
ni swali tu

chib said...

Laumu wote tu bwana!

Yasinta Ngonyani said...

Ni jambo la kusikitisha kuona hakuna maendeleo yoyote katika nchi yetu lakini kuna amani. Ni kweli ni ajabu kwa hiyo inabidi walaumiwe wote.

Nicky Mwangoka said...

Yaani kama vile tu vipofu katika nchi ya vipofu. Sijui hata itakuwa hivi mpaka lini. Hatujifunzi kwa wenzetu tunapowaona au kusoma habari za maendeleo yao.Kazi ipo. Asante kaka kwa changamoto hiii

Mzee wa Changamoto said...

Swali lako kaka limenikumbusha mambo mawili. Kwanza ni ile Post yangu ya UJINGA 360 DEGREES. NI KAMA HADITHI YA KUKU NA YAI ambayo nilikuwa nasaka jibu la "kama kuna kizazi kibaya cha kuku, tubadili lishe ya kuku ama utaratibu wa mayai?" yaani nikimaanisha kuwa "kama kuna uozo nchini mwetu, tuanze kuuondoa kwa kuibadili jamii ama watawala?" Ilikuwa hapa http://changamotoyetu.blogspot.com/2009/06/ujinga-360-degrees.html
Lakini pia nimekumbuka ilee hadithi ya MWENYE MTINDIO WA UBONGO aliyekuwa akipita mahala kisha akaona mtu anaoga (kwenye mabafu yetu ya passport na akaamua kukwapua nguo. Na yule jamaa aliyekuwa ndani akaanza kumfukuza akiwa mtupu. Watu wakabaki wakijiuliza "kichaa ni yupi?"
Kama serikali inajua wananchi ni wajinga na inatumia mwanya huo kujinufaisha, nadhani yenyewe ina ujunga-plus

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

@chib, na mimi nimo nibakie wapi?

@kijana wa Cmoto, nimekupata

Albert Kissima said...

Mimi nadhani kinachokosekana ktk nchi yetu ni "uzalendo".Asilimia kubwa ya viongozi wetu si wazalendo na hata wale wazalendo/wanamapinduzi huandamwa kila uchao na wasiotaka mageuzi.Wapo wananchi wanaoficha maovu ya viongozi na pia kuwaandama wananchi wazalendo wanaotaka mapinduzi ya kimaendeleo.


Mimi nadhani la msingi ni sisi kujiuliza uzalendo utapatikana vipi, miongoni mwetu na hata kwa viongozi wetu.Kwa hali ya nchi yetu, ni bora viongozi wetu wakaanza kudemonstrate uzalendo kwani uzalendo wa wananchi ni dhahiri kuwa ni wa force na unaoweza kupelekea kugharimu maisha yetu.Hili limejidhihirisha kwa jirani zetu Wakenya.

chib said...

:-)