Tuesday, October 13, 2009

ILI UKWELI UWE UKWELI

Image from http://contendingfortruth.net/
Majuzi tulikuwa tumekaa kazini baada ya mlo wa mchana. Kisha jamaa (ambaye alikuwa amekula vitunguu vibichi) akawa anaendelea kusimulia habari fulani. Mwenzake pembeni yake akamwambia "ukweli" kuwa alikuwa amebaki na harufu ya vitunguu alivyokula. JAMAA HAKUPENDA NA ALIHISI KUDHALILISHWA. Nikajiuliza maswali mengi kama aliyesema alistahili kusema aliyosema ama alistahili kutosema alivyosema??? Akili yangu ikanirejesha mbali kiasi, mwaka 1997. Nakumbuka nilikua nikimsikiliza Askofu Mkuu wa KKKT Dr Sebastian Mushemba (sasa ni mstaafu) na katika mengi mema aliyosema nakumbuka alisema "ukweli ni kitu kizuri. Lakini ni kizuri kama kimetumika katika mahali na wakati muafaka." Wala sikuhitaji mtafsiri kunisaidia kulitambua hili. Kwani mimi (niliyekuwa mwanafunzi wakati huo) sikutaka mtu aseme UKWELI kama nilikuwa nimekimbia darasa na kulala bwenini. Sikupenda UKWELI toka kwa mtu ambaye alijisikia kufanya tofauti na nilivyokuwa natamani mimi. Kwa hiyo sentensi ya Askofu Mushemba ilikuwa na bado ina UKWELI kwangu.
Na sasa nimekuja kujiuliza kama UKWELI ni kitu ambacho kinatakiwa kuaminiwa na kusikilizwa kama kilivyo ama mara zote huwa inategemea na pande mbili zihusikazo?

Na nililogundua ni kuwa ILI UKWELI UWE UKWELI, NI LAZIMA PANDE MBILI ZIWE KATIKA MAZINGIRA YA KUUONA KAMA UKWELI. Kama upande mmoja utaamua kutoutambua kama ukweli basi tunaweza kuishia kuuita huo ni Udhalilishaji ama hata kuvunjiana heshima. Hebu jaribu kufikiri kama leo hii ntasimama na kusema SERIKALI YA TANZANIA IMESHINDWA KAZI ILIYOAHIDI KWA WANANCHI MIAKA MINNE ILIYOPITA. Unadhani Mheshimiwa Rais na watendaji wake wataenda kwenye vyombo vya habari na kuniunga mkono? Lakini labda kabla hawajaenda watakaa na kujiuliza kama
Je!! WAMEWEKEZA KATIKA MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA (kwa kadri ya uwezo walioahidi ama rasilimali na uwezo uruhusuvyo)?

Je!! WAMESAMBAZA NA KUBORESHA HUDUMA ZA ELIMU, AFYA NA HUDUMA ZA MTEJA KWA WANANCHI?

Je!! WAMEONGEZA USALAMA WA RAIA KWA WANANCHI?

Je!!WAMEWEZA KUBORESHA MIUNDOMBINU KWA MANUFAA YA TANZANIA?

JE!!! UWAZI (GAP) ILIYOPO KATI YA MASKINI NA TAJIRI INAPUNGUA AMA INAONGEZEKA?
Lakini kwa maswali yangu haya, bado naamini kuwa nisemalo halitakuwa UKWELI kwani kwao ni kama kuwanyang'anya tonge la mlo mdomoni mwao. WATAWALA WETU wanajua wazi namna ambavyo wananchi wanazidi kutaabika na si kwa kuwa uchumi wa dunia umekuwa m'baya, bali kwa kuwa kwa kutumia kisingizio cha uchumi m'bovu, wanazidi kuwanyonya na kuwadidimiza walio na uhitaji.
Sote wenye imani tunaelezwa kuwa UKWELI UTATUWEKA HURU japo tunaona wenye imani haohao wanendelea kuudidimiza ukweli huo kwa kisingizio kimoja ama kingine. Najiuliza kama ningeweza kuwauliza wananchi na kuwaasa wawe wakweli (na wao kuniamini na kuniambia ukweli), sijui ni wangapi wangesema wanaipenda serikali iliyopo, sijui wangapi wangesema kuwa wanaitaka irejee madarakani, sijui ni wangapi wangesema wanataka yeyote aliye madarakani arejee na sijui ni wangapi wangekuwa wakweli juu ya nafsi zao na kuelekea kupiga kura kutokana na ukweli huo.

Hawawezi na ndio maana UKWELI wanaoueleza mara kwa mara na UKWELI wanaoupigia kura si UKWELI halisi japo unaonekana kuwa UKWELI. Ni kwa kuwa hawajawekewa mazingira ya kuweza kuusema ukweli huo, na ni mbaya zaidi kuona kuwa wanakosa mazingira hayo katika kipindi wanachomuweka MTAWALA madarakani kwa miaka mingine mitano.

Lakini kwako wewe UKWELI (ama mfano wa ukweli) ni upi??
Kwamba sisi ni maskini licha ya madini na maliasili zote tulizonazo?
Kuwa UTAWALA uliopo unaendeleza MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA licha ya hali tuionayo sasa?
Kuwa wataweza kujenga zahanati nchi nzima (kama alivyonukuliwa Waziri Mkuu februari) ilhali zilizopo hazina wauguzi na nyingine hazifikiki?
Kuwa watasambaza umeme nchi nzima ilhali umeme unaotumika sehemu ndogo ya nchi ni wa mgao wa zaidi ya nusu siku?
Ama kuwa sera na ilani za uchaguzi ujao zitamfaa zaidi mwananchi???????
NI KWA KUWA WATAWALA HAWATAKI KUUNGANA NA WANANCHI KATIKA KUSIKILIZA NA KUTEKELEZA MAHITAJI YA WANANCHI, BASI KILA UKWELI WA WANANCHI HAUTAKUWA NA UKWELI KWA WATAWALA KWANI ILI UWE UKWELI WANASTAHILI KUUNGANA NA HISIA ZA WANANCHI NA WAO (WATAWALA) HAWATAKI KUUTAMBUA

4 comments:

Simon Kitururu said...

Lakini mara nyingine nafikiri ukweli unategemea tu staili inayotumika kuuwasilisha.

Nafikiri kama unamjua unayetaka kumpa ukweli au tu ni mzuri katika kusoma watu na mudi zao , kwa kupatia staili ya uwakilishaji muda wowote na wakati wowote unaweza kuwa ni wakati wa kumpa ukweli.

Evarist Chahali said...

Mzee wa Changamoto,watawala wetu hawajisumbui hata kusema uongo (let lone kusema ukweli) kwa vile wamejiridhisha kuwa ukimya,dharau,puuzo na hata kashfa havitawaondolea nafasi zao.Sijui kitokee kipi kitakachowaamsha watu usngizini na kuwakaba koo (figurately) watawala wetu kudai haki.

Hii safari inaweza kuwa sio tu ndefu bali inayoelekea kusikoeleweka.

chib said...

Maisha bora kwa kila mtanzania, mimi kwa mtazamo wangu ina maana nyingine. Labda waseme mtanzania halisi ndio nitaelewa. Ukweli ni kwamba mtanzania kwa mtazamo wao, ni yule aliye na kazi nzuri inayoweza kumpa dhamana ya kupata mikopo bila ya wasiwasi, lakini mtanzania halisi ni yule ambaye anategemea nguvu zake na jasho lake kujipatia mlo wa siku hiyo, na hana mamlaka au uwezo wa kupanga maisha yake. Labda awamu ijayo ndio itakuja na maisha bora kwa kila mtanzania halisi

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

wewe ni sehemu ya huho ukweli na hivyo wewe ndiye kweli na sio maneno yangu au ya kitururu.

sasa unasemaje wewe kweli! je unadhani kuna anayeweza kukufanya ujisikie vile unavyotaka kujisikia?