Saturday, February 13, 2010

Ufunguzi wa Michuano ya Olimpiki, unajifunza nini?

Blogu hii "ilizaliwa" August 25 2008. Na post ya pili kubandikwa hapa ilikuwa kuhusu kumalizika kwa michuano ya Olimpiki ya majira ya joto. Na swali nililouliza hapa lilikuwa Olimpiki imeisha. Tumejifunza kitu? (isome hapa). Na humo (licha ya uchanga wa uandishi)niliandika na kuuliza maswali kujua kama kuna tunachojifunza. SINA HAKIKA KAMA KIPO.
Na sasa leo nimekaa kutazama ufunguzi wa michuano ya Olimpiki ya majira ya baridi huko Vancouver Canada. Na swali lanijia tena kuwa TUNAJIFUNZA KITU?
Wapo wanaouliza kama kuna "utimamu" wa swali langu hasa ukizingatia kuwa michuano hii ni ya majira ya baridi ambayo sisi hatuna. Lakini kuna ninalotaka kuongea hapa.
Nimewahi kuandika juu ya KUUNGANISHA ELIMU NA MICHEZO NA FAIDA ZAKE KAMA ITASIMAMIWA VEMA.
Ni muunganisho huu (wa elimu na michezo) ambao umekua zao la uzalishaji wa wanamichezo wanaong'ara katika nchi mbalimbali. Mfano mzuri ni wanamichezo wanaong'ara kwenye nchi zisizo na uwezo mkubwa wa kuwaandaa ambao wanatumia uwezo wa kimichezo kwenda kusoma kwa scholarship huku wakijinoa na kutumia nafasi hiyo kufikia kiwango cha kuwawezesha kushiriki michuano mikubwa inayowapa pesa, heshima kwao na heshima kwa nchi zao.
Tumeona nchi kama Jamaica na nyingine ndogondogo za Carribean zikitamba katika michezo lakini asilimia kubwa ya wanamichezo wake wamekuwa wanafunzi katika nchi zilizoendelea. Pia katika michuano hiyohiyo ya majira ya joto tulishuhudia mwadada toka Afrika Kusini akiiwakilisha nchi japo makazi na mazoezi alikuwa akiyafanyia katika chuo kikuu cha Texas.
Na sasa TANZANIA tuna "tunda" moja la mfumo huu ambalo ni HASHIM THABIT ambaye kwa kutumia Scholarship ya UCONN, aliweza kufikia kiwango cha kuingia katika ligi kubwa na maarufu zaidi ya kikapu duniani ya NBA.
Leo hii tunashuhudia nchi ya ETHIOPIA (ambayo iko kwenye ukame zaidi ya Tanzania) ikiwakilishwa katika michuano hii. Mshiriki wake Robel Teklemariam anashiriki katika mchezo wa Cross-Country Skiing. Mzaliwa wa Addis Ababa, Robel alikulia New York nchini Marekani na kupenda mchezo huo kisha akarejea Ethiopia ambako ilimchukua miaka 3 kuweza kutimiza mambo muhimu kuiwezesha nchi kuwa na vigezo vya kuwa na kamati ya Olimpiki ya majira ya baridi na kumuwezesha kuiwakilisha. Alishiriki michuano ya 2006 ambako hakufanya vema sana na sasa amerejea.
Pia kuna Kwame Nkrumah-Acheampong wa Ghana ambaye alikuwa mfanyakazi wa mapokezi katika kituo cha skiing nchini uingereza kisha akaanza kujifunza na sasa anakuwa m-Ghana wa kwanza kushiriki michuano hii.
Senegal nayo inawakilishwa naye Leyti Seck ambaye anashiriki katika skiing.
Afrika ya kusini nayo itawakilishwa na wanamichezo watatu ambao ni Peter Scott (Alpine Skiing), Bruce Warner (Paralympics Alpine) pamoja na Oliver Kraas (Cross Country Skiing).
Sijui unajifunza nini katika haya, lakini naamini kwa kuwekeza katika michezo kwa watoto ama wanamichezo wadogo, tunawajengea mazingira mazuri ya kunyakuliwa na vituo mbalimbali vya kuendeleza michezo na kisha kukuza vipaji vyao na kukuza uwakilishi nchi yetu.
Kutegemea kuwa na wawakilishi wazuri ambao hawana matayarisho mazuri ni kujidanganya. Na kutegemea kuwa na timu itakayotuwakilisha vema kwenye michuano mikubwa kwa kuanzia michezo ukubwani pia ni ndoto.
Tanzania imeamua kitu kimoja ambacho ni AMA KUWA NA WANAMICHEZO WAZOEFU WASIO NA ELIMU (kwa kuwa utastahili kutosoma ili ucheze) AMA KUWA NA WASOMI LAKINI WASIOLELEWA KIMICHEZO (kwa kuwa hakuna michezo mashuleni)
Sina hakina na DANGANYA TOTO ambayo Rais Kikwete anaifanya kwa KUGHARAMIA MAMILIONI YA DOLA KUMLIPA KOCHA WA KIMATAIFA ILHALI ANASEMA HAWEZI KURUHUSU MICHEZO KUANZIA SHULE ZA MSINGI. Alipohojiwa na mchambuzi wa michezo Bwn Israel Saria hapa, Rais Kikwete alisema "it is up to the Minister of Sports to come up with a good structure for how talent can be identified from class level up to national level. We should not forget that we also have good talent on the street and in some way this talent has to be identified and developed by having sports officers in the area or in clubs and retired sports figures, for example."

2 comments:

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

ni ajabu kwa Rais kutegemea waziri wa michezo aje na plan nzuri ilhali waziri mwenyewe hana passion na michezo :-(

tutaendelea kuwa 'chichwa cha mwendakuzimu' mpaka 'basi' :-(

Fadhy Mtanga said...

Kaka Mubelwa na Chacha kuna mchezo mnausahau. Huu mchezo ukiingizwa kwenye Olimpiki, tutafanya vizuri sana. Tena tutaongoza. Maana hapa kwetu ni mchezo unaotawala nyanja zote. Nao ni politiks