Tuesday, February 2, 2010

Wakuu wa mikoa........

*Watumishi wa wananchi ama mzigo kwa serikali na wananchi??
*Chanzo cha kudidimia maendeleo mikoani
.
Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa wakimsikiliza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (hayupo pichani) wakati alipozungumza nao kwenye ukumbi wa St. Gaspar Mjini Dodoma June 2009. Picha kwa hisani ya DailyHabari Blog
Jirani zetu wa Kenya wameanza harakati za kubadili mfumo wao wa utawala wa nchi yao kuelekea kule wanakoamini kuwa na ufanisi zaidi. Hivi majuzi kamati ya marekebisho ya katiba nchini humo, imekubaliana kwamba Kenya yastahili kuondoa cheo cha Waziri Mkuu. Sababu hasa ni UMUHIMU WA CHEO HICHO KI-UTENDAJI.
Na hili (kama ni kweli) ndilo kubwa la kujivunia. Kuangalia UTENDAJI wa viongozi wetu kujua kama kuna umuhimu wa kuwa na vyeo hivyo ama watu hao wapewe kazi nyingine (kama kuna ulazima)
Na hili ndilo lililonifanya kuwaza tena kazi za WAKUU WA MIKOA TANZANIA.
Tangu utotoni mwangu nimekuwa nikiwaona baadhi ya wakuu wa mikoa ambao mpaka sasa wapo madarakani. Wamekuwa wakihamishwa toka mkoa mmoja mpaka mwingine bila kuacha mafanikio yoyote ya kuridhisha huko watokako. Wengine wamekuwa wakihamishwa baada ya kulalamikiwa saana na wananchi na hivyo kuondolewa. Lakini kibaya zaidi ni kuwa WAKUU WA MIKOA WANATEULIWA NA RAIS.
Hili lanifanya kujiuliza kama

1: Wakuu wa mikoa NI WATUMISHI WA WANANCHI AMA VIBARAKA WA RAIS NA SERIKALI?
2: Hivi kazi yao kubwa ni nini?
3: Wapo kama watendaji wa kuendeleza mikoa na wananchi ama kutekeleza ILANI za uchaguzi za Rais aliyeko madarakani?
4: Hivi Rais awateuaye anajua hali halisi ya uhitaji wa mikoa anayowapeleka wakuu hao?
5: Ni kwanini anawahamisha wakuu hao kabla hawajaweka misingi imara ya maendeleo huko waliko?

NAAMINI WAKUU WA MIKOA NCHINI TANZANIA NI SEHEMU YA CHANZO CHA KUDIDIMIA KWA MAENDELEO NCHINI.
Wakuu hawa wa mikoa hawajajikita katika matumizi ya malighafi na rasilimali zilizoko mikoani ili kuwezesha maendeleo mikoani.
Wakuu hawa wa mikoa hawana uchungu na mabadiliko chanya ya mikoa yao hasa kama maendeleo hayo si sehemu ya ukamilishaji wa ILANI YA UCHAGUZI ya rais mteua.
Wakuu hawa wa mikoa hawana la kupoteza iwapo mikoa itashindwa kuendeleza sekta mbalimbali zilizomo mikoani humo.
Ninalojiuliza ni kuwa
Kwanini cheo hiki (UKUU WA MIKOA) kisifutwe na kubaki na viongozi ambao wanachaguliwa? hasa wabunge ambao wanajua wana deni na wananchi wao?

NINALOAMINI NI KUWA
Endapo wakuu wa mikoa wangekuwa wanagombea basi wangekuwa na ubunifu wa kutumia rasilimali zilizopo mikoani ili kukamilisha bajeti na mahitaji ya mikoa wanayoiongoza na kupunguza kutegemea ruzuku za serikali kuu. Mikoa yetu ina rasilimali nyiiingi na kama ingetakiwa kujiendesha kwa kujitegemea nina imani kungekuwa na ubunifu na uchungu wa kutumia rasilimali hizo. Lakini kwa sasa sioni kazi za wakuu wa mikoa kwa sababu ndani ya miaka mitano ya Rais, wengine wanakuwa wameshahama "vituo" vya kazi zaidi ya mara mbili na hakuna la maana wanalofanya kuiendeleza. Naamini ni mzigo kwa serikali na wananchi kwa ujumla.
Pia kwa kutokuwa chachu ya kufikiri namna ya kuifanya mikoa kutumia rasilimali kujiendesha na kusaidia pato la taifa, basi wamekuwa chanzo cha kudidimia kwa maendeleo mikoani.
Labda wakuu wa mikoa wachagulie. Hii itawafanya wachunguze THAMANI ya mikoa yao na kutumia rasilimali zilizopo mikoani kuiendeleza.
Tuonane "Next Ijayo"

2 comments:

Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti! said...

kaka umenena. Napata shida kama hiyo kwa ma-RC na ma-DC kujua wako kwa maslahi ya nani hasa.

ukichukulia swala la North Mara huko Tarime ambako kuna wawekezaji na wanamwaga maji machafu katika vyanzo vya maji na kusababisha watu, mifugo na mimea kufa wakati hao wakubwa wanaingia mgodini kukagua kisha kutoka humo wakiwa wamefunga vioo vya magari yao bila kuwasikiliza wananchi :-(

Inaumiza na kuchukiza kweli na inaweza kusababisha uasi wa wananchi kwa viongozi wao :-(

sikudhani khamis said...

kwelime cjauona umuhimu wa wakuu wa mikoa wala wa wilaya me nadhani ni kundi moja la watu abao wanafahaiana na waliahidiana vyeo bas lazima wapeane kwasababu ya kutiiza ahad zao, maan kuna wengine hata maswala ya manageent hawajui kabisa lakin kwasabau ni naniliu wa mkubwa et nae ni mkuu wa wilaya . esipend kuona