Tuesday, March 16, 2010

ASANTE Dk. KINASHA... MAISHA MEMA UYAANZAYO SASA

Dr Abednego Kinasha (kati) ambaye alikuwa Rais wa The College of Surgeons of East, Central and Southern Africa (COSECSA) akiwa na Makamu Rais wa The Royal College of Surgeons in Ireland (RCSI) Profesa Frank Keane (shoto) na Rais wa The Royal College of Surgeons in Ireland (RCSI) Profesa Gerald O'Sullivan katika picha hii ya Mei 8, 2008.
Image from RCSI.IE
Nilipofunzwa somo la UJASIRIAMALI chuoni Dodoma, nilifunzwa sababu kuu tatu za kufanya kazi ambazo ni SABABU ZA KIUCHUMI ambazo ni kwa zile kazi ambazo wafanyao wanafanya ili kupata pesa hata kama hawapendi wafanyalo. Pia kuna SABABU ZA KIJIOGRAFIA ambazo ni kwa wale ambao wanapenda kusafiri na kupanua uwigo wao wa ulimwengu ikiwa ni pamoja na kazi zihusishazo kusafiri. Kisha kuna SABABU ZA KI-UTU ambazo huusisha watu ambao WANAFANYA KAZI ZA WITO na kwa hakika wafanyalo ni huduma zaidi ya kile walipwacho. Ndipo hapa tukutapo waalimu, waokozi / zimamoto na hata madaktari na wauguzi.
Ugumu wa elimu juu ya kazi na nia za watu kufanya kazi ni kuwa mwenye nia yoyote kati hizo tatu anaweza kuwa popote kwa sababu yoyote, na namna pekee ya kujua ama kuona nani anafanya kazi kwa nia gani ni kwa kumuona akitenda kazi hiyo.
Nami maishani mwangu nilibahatika kumuona Dr Kinasha akitenda kazi ya wito.
Kwa wanaofuatilia hapa wanakumbuka post yangu ndeefu ya Desemba 22 2009 iliyokuwa na kichwa cha habari MIAKA 10 BAADAE (Loooong Personal story) Isome hapa ambayo ilizungumzia ajali niliyopata. Katika post hiyo nikazungumzia juu ya msaada nilioupata toka kwa Dada ambaye nikingali natafuta mawasilianao naye, Dada Renatha Benedicto.
Ambalo sikuendeleza kwenye habari hii, ni kuhusu matibabu ambayo nilianza kuyapata kutibu mgongo wangu. Nakumbuka nikiwa chuoni Dodoma mwanzoni mwa mwaka 2000, nilipata maumivu makali saana ya mgongo kiasi cha kushindwa kutembea na nilihofia maisha yajayo kwa kuwa sikuwa na imani kama kuna siku ningeondokana na maumivu yale. Nilipopata nafuu nilirejeshwa nyumbani kwa matibabu. Ni hapo nilipopelekwa Muhimbili kitengo cha mifupa (MOI) na kuonwa na Dk Abednego Kinasha.
Nilitibiwa na Dk Kinasha na Dk Ismail Shariff (kwa sisi wagonjwa tupendao kujimilikisha twasema "ndio wakawa madaktari wangu") kwa muda wote niliohudhuria pale na hata nilipokuwa narejea likizo niliendelea kuangaliwa nao.
Lakini licha ya kunitibu, Dk Kinasha na Dk Shariff waliendelea kufuatiia maendeleo yangu hata nilipokuwa nje ya Dar wakiuliza ndugu waliokuwa na mawasiliano juu ya maendeleo ya mgongo wangu.
HAPO NDIPO UJUAPO KUWA KUTIBU NI ZAIDI YA KAZI KWAO.... NI WITO.
Nimekuwa na maumivu haya kwa muda mrefu lakini sasa niko vema. Na natambua kuwa haijalishi ningepata Daktari bingwa wa vipi huku nilipo, kama Dk Kinasha na Dk Shariff wasingefanya lililo sahihi, basi pengine sasa hivi nisingekuwa na uwezo wa kusogeza mwili wangu bila msaada wa mtu. Ni usahihi wa matibabu ya awali walionipa ambao umenifanya niendelee kuwa nilivyo sasa.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, nilizungumza na Dadangu ambaye alinitaarifu kustaafu kwa Dr Kinasha. Ilikuwa ni HISIA MCHANGANYIKO. Zile za kufurahi kuwa anaenda kupumzika baada ya utumishi wa miaka mingi. Lakini pia kukawa na hisia za kuwafikiria mamia ya wagonjwa ambao watakosa huduma sahihi na ya ukarimu ambayo mimi na wengine wengi tumepata katika kipindi kirefu cha utu na utumishi wa Dr Kinasha. Najua kuwa hata "anapostaafu" bado ataendelea kuwatumikia wengi kama ambavyo aliendelea kunijulia hali hata kama sikuwa Dar kwa matibabu. Ni haya mema ambayo watu wanafanya kama sehemu yao ya maisha ya kila siku, yanayotufanya binadamu kuuona UBINADAMU WA KWELI kama alivyoandika Kakangu Matondo akikumbuka SIKU ALIYOKUTANA NA UBINADAMU WA KWELI PALE MUHIMBILI (isome hapa)
Ni wema huu wa kuwa msikivu, mkarimu, mkweli na mwenye busara aliouonesha Dr Kinasha wakati na baada ya matibabu unaonifanya kuendelea kumuona miongoni mwa HEROES waliopata kugusa maisha yangu. Kama alivyosema Lucky Dube kwenye wimbo wake hapa chini kuwa "Do you see the smile on their faces after you've done what you're doing? Do you see satifaction on their faces, after you have blessed them with your gift. You dont think it's much, but for them it means a WORLD. They wake up in the morning and wish you were there. You don't have to lie to gain their trust"

Leo hii natembea, nakimbia, nacheza na hata kufanya kazi na kulea familia yangu changa kwa kuwa Dk Kinasha alishiriki katika matibabu yangu ya awali.
Nakutakia maisha mema katika "ustaafu" uuanzao Dokta na popote uendapo tambua kuwa NATHAMINI SAANA MCHANGO WAKO.

ASANTE SAANA Dk. KINASHA...NAKUTAKIA MAISHA MEMA UYAANZAYO SASA

8 comments:

Anonymous said...

Mubelwa, pongezi kwa kuandika habari hii, nami kama ambavyo nimekuwa nikifanya kwenye posti nyinginezo (ya Prof. Matondo na dada Yasinta), posti hii naiwakilisha jikoni kwa wenyewe wajue aina ya chakula kinachopikwa ili waendelee kurekebisha mapishi na ladha kiwe cha kulika zaidi.
Kweli yapo mapinduzi mazuri katika matumizi ya blogu na tovuti kwa sasa. Mi nafurahi.

Anonymous said...

Sitoagi maoni lakini habari hii imenigusa sana.
Akisoma atajivunia kazi aliyokuwa akifanya.
Pongezi na zangu pia

Mdau

Unknown said...

Mubelwa,
habari hii sio tu inatoa changamoto kwa wafanyakazi wa sekta ya afya, lakini pia inawakumbusha uwajibikaji, ukarimu, kujitolea zaidi na kuchapa kazi. Dr Abednegro amekuwa ni mfano na muhimili katika sekta hiyo, amejijengea heshima sana, amesaidia watu wengi wenye shida, na amekuwa karibu sana na wagonjwa wake. Ni mwalimu mzuri, asiye na maneno mengi na anayechukia uzembe na aneyependa kuona watu wakiwa na furaha tena..binafsi i salute him for that. i am sure ujumbe wako utamfikia.
Shukrani kwa kukumkumbuka.

Unknown said...

Mubelwa,
habari hii sio tu inatoa changamoto kwa wafanyakazi wa sekta ya afya, lakini pia inawakumbusha uwajibikaji, ukarimu, kujitolea zaidi na kuchapa kazi. Dr Abednegro amekuwa ni mfano na muhimili katika sekta hiyo, amejijengea heshima sana, amesaidia watu wengi wenye shida, na amekuwa karibu sana na wagonjwa wake. Ni mwalimu mzuri, asiye na maneno mengi na anayechukia uzembe na aneyependa kuona watu wakiwa na furaha tena..binafsi i salute him for that. i am sure ujumbe wako utamfikia.
Shukrani kwa kukumkumbuka.

Unknown said...

Kinasha is a great human being. Kati ya madaktari wachache wenaopenda kazi yao tanzania.
ukapige kinanda sasa ila usiache kufundisha

Simon Kitururu said...

Katika moja ya kitu KIMOJAWAPO ambacho nikipendacho na kinikumbushacho kitu ambacho LABDA SIKIFANYI ITOSHAVYO nikitembelea kijiwechako MUBELWA BANDIO ,...
ni kile kiguswacho na moyo wako wa KUSHUKURU kila akugusaye maishani mwako!

Huwa unanifanya nifikirie ni WANGAPI maishani mwangu ambao sijawashukuru na WASTAILIO shukurani za DHATI .

Pamoja na yote ASANTE PIA kwa hilo Mubelwa Bandio!

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Hivi madaktari bingwa kama hawa wakistaafu wanakwenda wapi? Wanakwenda kwenye mahospitali binafsi au wanaendelea kufanya kazi kwa mikataba maalum kama maprofesa wa vyuo vikuu? Ningekuwa "serikali", ningewapa kila kitu wanachohitaji na kuwaomba wabakie kazini mpaka umri utakapowaamuru kuacha.

Anonymous said...

ninamshukuru Dr Kinasha alimfanyia upasuaji baba yangu mzee Simoni Baraka(RIP 2005),Mungu akuongezee hekima katika kustaafu kwako. daktari bingwa kama huyu anastaafu kwa uzee ?mbona anaonekana bado.