Wednesday, March 17, 2010

Nguvu ndogo ndani mwetu, iliyo kubwa kwetu na chanzo cha mafanikio na maanguko yetu.

Mwanzoni mwa miaka ya 200 nakumbuka nilikuwa nasikiliza kipindi cha KUMEPAMBAZUKA cha Radio One ambapo muongozaji wa kipindi hicho Kaka Godwin Gondwe aliyekuwa akihojiana na mwathirika wa virusi vya UKIMWI alitoa kauli ya hitimisho ambayo mpaka leo naamini ina ukweli maishani mwetu.
Alisema KAMA HUTAKI KITU, USISIKILIZE CHOCHOTE KUHUSU KITU HICHO. Kauli hii ilikuja baada ya binti mwathirika aliyekuwa akihojiwa kusema namna ambavyo alikuwa amejiwekea "nadhiri" ya kutomkubali mtu yeyote kwa uhusiano wa kimapenzi, lakini baada ya kumpa nafasi ya kuongea mwanaume mmoja, alijikuta akikubali kuwa na mahusiano naye kisha kufanya naye mapenzi na kusambaziwa virusi hivyo.
Ukiangalia kwa jicho la ndani, utagundua NGUVU YA KUSIKILIZA NA KUELEWA ilivyokuwa chanzo cha hayo yote.

Ni nguvu hii hii ambayo imeleta maanguko kwa familia nyingi. Familia ambazo zmeshindwa kutatua matatizo ya wazai na kuishia kwenye talaka kwa kuwa mmoja ama wazazi wote wanajiona kuwa sahihi na hakuna aliye tayari kusikiliza upande wa pili. Ni kutosikiliza huku ambako kumeyafanya mataifa makubwa kuelekea vitani na kugharimika kwa mamilioni ya pesa na baadae kuja kutambua kuwa walichokuwa wanadhani kuwa ndicho sasa sicho ama walichodhani kimefichwa hakijafichwa na mwisho wa mambo yajulikana kuwa waliofanya maamuzi HAWAKUSIKILIZA WALA KUELEWA.
Na hakuna ubishi pia kuwa nguvu hii ya KUSIKILIZA NA KUELEWA huwaponya wengi wanapoamua kutosikiliza yale ambayo yanaweza kuwaweka matatani. Nguvu ya USHAWISHI inayopitia kusikiliza huweza kuwatumbukiza wengi katika matatizo ama shughuli ambazo si sahihi ama salama kwa maisha yao na jamii kwa ujumla. Wapo ambao si makahaba, wezi, majangili, wauaji ama wakabaji kwa kuwa hawakuwapa nafasi ya kutosha wale ambao walitaka kuwashawishi kuingia huko.
Vivyo hivyo, wapo ambao si wafanyabiashara, watangazaji, waigizaji, waalimu, madereva, wachungaji na hata ma-Sheikh kwa kuwa hawakusikiliza na kuwaelewa wale ambao wangewashawishi kufanya hivyo.
Ina maana KUNA NGUVU KUBWA SANA YA KUSIKILIZA NA KUELEWA AMBAYO INAWEZA KUTUFANIKISHA NA KUTUANGUSHA
Lakini pia tukitafakari vema, kuna mengi tunayoweza kuyatambua na ambayo yatakuwa SULUHISHO la matatizo meengi hapa ulimwenguni
Nilichogundua ni kuwa HAKUNA MJINGA kwani kwa kukaa chini na kumsikiliza unaweza kujua kile ulichodhani kuwa ni ujinga na kutoka kwa "mjinga" huyo utaweza kujifunza namna walivyo wajinga hivyo utakuwa umeerevuka. Na huwezi kuerevushwa na mjinga. Hivyo, kama utamsikiliza mtu yeyote, utagundua kuwa si mjinga (hata kama hudhani kuwa ana busara na uelewa kama ulionao wewe katika uelewalo wewe kwa namna uelewavyo wewe)
Machi 5 mwaka jana niliandika kuhusu Nguvu baina yetu isiyo na nguvu ndani mwetu, yenye nguvu kwetu.(Isome hapa) ambapo nilizungumzia kwa kiasi nguvu hii kwa mtazamo mwingine na kisha Desemba 3 2009 nikaandika juu ya Nguvu ndani mwetu isiyo na nguvu kwetu bila nguvu miongoni mwetu.(Isome hapa) ambayo inajikita katika KUSHIRIKIANA ambako ni sehemu kubwa ya mafanikio ya kila mmoja wetu.
Dunia ya sasa inaongozwa na watu ama taasisi ambazo hazijihusishi na kusikiliza upande wa pili wa tatizo na matokeo yake hakuna suluhisho. Angalia mashariki ya kati kisha utaelewa. Bushman aliwahi kusema "United Nation should be dealing with equal rights, it is the only chance it can give us INTERNATIONAL PEACE, they only pretend to be what they're not. One day, one day, i know there'll be PEACE. There will be peace on earth" Dwight Bushman Duncan
Msikilize huyohuyo Bushman katika wimbo huohuo aliowaomba watu wapunguze kuongea na kuanza kusikiliza kisha watende aliouita TALKATIVE

2 comments:

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

kusikiliza ni bora kuliko kuongea. ndo maana tuna masikio mawili na mdomo mmoja tu.... R.Kiyosaki

Albert Kissima said...

Kaka,nakusifu kwa kuwaza,ni wengi ambao hatukuwahi kuwaza juu ya nguvu hizi ambazo umekuwa ukitujuza, ni knowledges mpya hususani kwangu mimi.