Tuesday, April 13, 2010

KIZAZI KIPYA...Kizazi tunachopandikiza ujinga na uzembe

KWA UFUPI NI KUWA NAZUNGUMZIA "UJINGA" WA KUTOTAKA KUSOMA MAANDISHI MAREFU KAMA HAYA.
Photo: Mind of The Grind Blog
"If you wanna save the world, you gotta save the children. Set an example for the children to follow and make a brighter tomorrow"
Hii ni nukuu yake Luciano aliyoimba katika wimbo wake wa Save The World ambao unaakisi maisha ya sasa ambayo yalitokana na maamuzi na makuzi yaliyotendeka miaka kadhaa iliyopita.
Nakumbuka mihula kadhaa iliyopita shuleni tulisoma makala ya mchunguzi na mwandishi Peter Gibbon aliyoiita "End of Admiration: The Media and The Loss of Heroes" ambayo alisema kuwa kizazi cha sasa kimeweka kando heshima kwa mashujaa na kutukuza mambo na watu wa ajabu watendayo mengi yasiyoinufaisha jamii. Amezungumza juu ya vyombo vya habari vinavyochangia kutothaminisha mashujaa na kuendekeza kuwatukuza nyota wanaofanya mambo yasiyofaa jamii.
Japo swali laweza kuwa NANI AFAAYE KUITWA SHIJAA?, na japo naamini kuwa shujaa huonekana na kuthaminiwa kulingana na jamii, bado naamini katika alilosema Bwn Gibbon. Hata kwa ushujaa na mashujaa wa sehemu mbalimbali, bado twaona baadhi ya vyombo vya habari yakiwemo "majamvi" yetu haya "yanavyoenda nje ya ukawaida na majukumu yake" na kuandika habari za ajabu ambazo zitaweza kuwapa "attention" ya wengi.
Blogu zimekuwa zaidi ya sehemu ya kutafuta umaarufu na kukusanya idadi kubwa ya wasomaji hata kama itamaanisha kuandika kisicho na maana.
Siku hizi habari ya mpiganaji anayetetea haki za wanyonge, haina maana kama ilivyo ya nyota aliyefanya upuuzi na kupelekwa jela ama ya fulani aliyepiga picha za nusu uchi ama za tamasha ama onesho fulani. Na utashangazwa na tofauti ya idadi ya maoni ktk habari hizi mbili.
Jana niliingia katika mjadala na Kaka Richard Mgamba (Mhariri wa The Guardian on Sunday) kuhusu kauli ya Rais wa awamu ya Tatu Mhe B. W. Mkapa kuwa waandishi wa sasa Tanzania hawako makini katika kazi, na katika moja ya maoni yake alisema "Waandishi ni watoto wetu, mafunzo na uadilifu huanzia kwenye familia, koo, jamii, shule, na hadi taifa. Sasa tukianzia huko sio kwa waandishi tu, pote penye uozo ni jukumu letu wote kushirikiana.
Wangapi wanajisomea leo hii? Tunajisomea pale tu kunapokuwa na mitihani shuleni na tukisha hitimu, vitabu vimesahaulika.
Jiji la Nairobi lina bookshops kubwa kubwa mara saba ya Dar, lakini tuna bar nyingi na grocery kuliko Nairobi, japo wakenya wanakunywa sana pombe na nyama choma.
Viongozi wetu hawasomi hata hao walioko juu, sidhani kama wanajisomea. Tukijenga nyumba siku hizi tunaweka mpaka sehemu ya Mazoezi, lakini hakuna study rooms.
Forms three na four zamani languange three walikuwa wanasoma vitabu zaidi ya arobaini, lakini leo havizidi vitatu. Ukimuuliza mwanafunzi wa kiingereza hapa kwete William Shakespear alikuwa nani, hatakujibu.
Angalia mashindano ya Zain, uone uwezo wetu katika current affairs, ndipo utajua tuko wapi. Hao akina Mkapa ni product ya Elimu ya Zamani ambayo ilikuwa inajali quality kuliko quantity.
Kaka yangu Bandio sasa katika jamii kama hii, tunahitaji mapinduzi katika elimu, vinginevyo tutaendelea kuwa na waandishi uchwara, wanasiasa uchwara, madaktari wababaishaji, engineers wezi nakadhalika "
Habari ya mwelimishaji anayekwenda kuielimisha jamii kuhusu mambo mbalimbali yaisibuyo jamii hiyo haipewi uzito kama ambavyo atakuwa supastaa fulani anayedhaniwa kuchukua mke wa mtu.
Hoja za waelimishaji kuhusu namna ya kuishi katika uchumi huu unaoyumba hazionekani kuwa za maana kuliko za "concert" ya msanii fulani mahala fulani.
Siku hizi hata wasanii wanaopenda kujulikana kama "kioo cha jamii" wanapanga na kufanya yasiyotendeka ili mradi waweze kuwa kwenye habari. Inasikitisha kuona sasa hivi hata watoto ambao wanatakiwa kufunzwa namna njema za kufanikiwa wanaona kuwa ujinga na kashfa ni njia ya mkato ya mafanikio (hasa kwa wale wanaotafsiri mafanikio kama kuandikwa kwenye magazeti na kuonekana kwenye vyombo vya habari)
Na katika kudhihirisha hili, unaweza kuona kuwa hata wasanii wanaanza kujiingiza katika uimbaji wa nyimbo za ajabu zenye kuwawezesha kujibizana hali itakayowapa "air time" ambayo inawapatia maonesho na "interviews" nyingi na kuwafanya wawe wanavyotaka kuwa.
Cha kujiuliza ni kuwa ni nini twarithisha wanetu juu ya ujasiri na ushujaa?
Ni kwanini wale maBIBI na maBABU wanaoachiwa watoto na watoto wao wasionekane mashujaa kwa yale watendayo?
Vipi kuhusu wale ambao kwa moyo mweupe wanasaidia kufanya kazi ngumu kufanikisha usalama na uhai wetu?
Na wale ambao kwa mshahara mdogo na ambao unachelewa kila mwezi bado wanaendelea kutuelimisha mashuleni na kututibu mahospitalini?
Na wale ambao kupitia nafasi na taaluma walizonazo wanajitolea bila kikomo kuwekeza katika kuwasaidia wengine ili nao wawe msaada kwa jamii nzima?
HAWA HAWAONEKANI, HAWAANDIKWI NA WENGI HAWATHAMINIKI jambo ambalo sio tu lasikitisha, bali laonesha ni nini twajitahidi kufanya na kizazi cha aina gani twataka kuwa nacho.
Ni kweli twaelekea kwenye kizazi kipya alichozungumzia Kaka Kissima ambacho hakina utambuzi wa Mashujaa halisi waliotenda na kuishi kwa utaratibu wa P.U.G.U ambao Kaka Makulilo Jr amekuwa akiuhimiza mara zote. Kizazi cha sasa kinakueleza wazi juu ya umuhimu wa kusoma ili urejee nyumbani "kufisadi" kwa namna nafasi yako itakavyokuruhusu.
Tunaona tofauti kubwa ya namna ufujaji na ukatili ulivyoongezeka miaka ya karibuni na kushuka kwa heshima na thamani ya mashujaa wetu wengi ambao walijitolea kwa hali na mali kutenda yaliyo mema kwa jamii na sasa wanataabika bila hata uwezo wa matibabu. Tumeona baadhi ya watumishi waliolitumikia taifa katika awamu ya kwanza wakiendesha maisha yao kwa taabu na hawa ndio waliojitolea kuwezesha kuwa tulipo na kujinyimba licha ya nafasi walizokuwa nazo wakati huo kufanya ufujaji. Lakini hakuna ajaliye hali zao, bali kila siku ni habari za mfujaji fulani anayedhuria mahakama kwa ufujaji aliofanya na hakuna wa kumjali SHUJAA anayeganga njaa huko kijijini. Na kizazi chaiga nini cha kufanya kuepuka aibu iwakumbao hawa MASHUJAA WETU WA KWELI.
Kama nilivyotangulia kusema, nanukuu aliyoimba Luciano kuwa "If you wanna save the world, you gotta save the children. Set an example for the children to follow and make a brighter tomorrow"
Msikilize hapa chini

Hiki ni kizazi chetu. Kizazi kipya. Kizazi kinachorithishwa ushujaa wa ujinga na kashfa badala ya kutenda yaliyo mema na yaifaayo jamii


JICHO LA NDANI ni kipengele kinachozungumzia mambo mepesi na yaliyo ndani mwetu, ambayo yakiangaliwa vema na kwa tafsiri ama tafakari njema yanaweza ama ndio suluhisho kwa matatizo yetu. Kwa matoleo yaliyopita katika kipengele hiki, BOFYA HAPA

5 comments:

Fadhy Mtanga said...

Nimeipenda sana post hii. Hivi ndivyo maisha ya sasa ya wa-tizii yalivyo. Ukitazama hata filamu zetu zinazoibuka kwa wingi kama uyoga, utaona ni jinsi gani upeo wetu ulivyo mdogo.

Tazama magazeti yanayonunuliwa kwa wingi ni yapi... Tazama kwenye mtandao wa jamii wa Facebook, status zinazokimbiliwa kutolewa maoni ni zipi.....pengine ndivyo kizazi cheti kimefikia ukomo wa uwezo wake wa kupambanua vema..unaweza kujiuliza kwa nini ipo hivi. Nakubaliana nawe, na wengine, tatizo la kwanza la msingi, ni mfumo mbovu wa elimu. Kisha ndo twaja kwenye mmomonyoko wa maadili na mengine meeeeengi.

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

@Papa Fadhy: ndivo utandawazi wizi ulipotufikisha :-(

Kama taifa sasa hatuna dira unategemea mtu binafsi atakuwa na dira?

Ni wachache

Albert Kissima said...

Posti hii nami nimeipenda sana, inanigusa na inanihusu mimi kama kijana na kama imgusavyo kila mmoja mpenda maendeleo,wazee na hata watoto. Ninahitaji ulimwengu mzuri,wema na wenye manufaa. Nahitaji Tanzania iongozwe na viongozi waadilifu,wazalendo,wenye kuwajali wananchi kwa manufaa ya sasa na ya vizazi vijavyo,nahitaji kizazi kipya kiwe na upya wenye tija, ubora wa utendaji wa mambo yenye kukubalika na jamii nzima,kisichohitaji umaarufu kwa mambo yasiyo ya msingi,chenye ushujaa wa kweli wenye suluhisho la mambo mengi ambayo yamekuwa ni kero kwa Tanzania na ulimwengu("save the world");hivyo basi,mimi kama mzazi mtarajiwa sina budi kujua ni jamii au ni familia gani nataka kuijenga na kwa malengo gani ya baadae("save Children")ili kusaidia na kama namna pia ya kuuokoa na kuusaidia ulimwengu na Tanzania yangu kwa mambo ambayo yangekuwa yamewekewa misingi bora na sahihi toka awali(likiwemo hili la makuzi stahiki ya watoto) tusingeangukia kwenye matatizo ambayo kwa asilimia kubwa yamesabishwa na kizazi cha juzi na jana(kizazi cha leo ni waathirika)

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

watoto wetu ni victim, ila na sisi tunakuwa wajinga wa kuwaacha waharibiwe na vyombo vya habari vyetu

SN said...

Post nzuri!

Tokea tuanzishe www.vijanafm.com, mwitikio umekuwa unasuasua ingawa tunajua fika kuwa viewers wanaongezeka kila kukicha.

Kusema ukweli nashukuru jinsi mtandao ulivyonifumbua macho (kuhusu kipi hasa hupendwa na Watanzania wengi).

Napenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha Vijana FM.