Wednesday, April 20, 2011

Nionavyo u-CHANYA wa HASI yao

Inarudiwa kwa kuwa inatakiwa kuendeleza ijayo juu yake. Na pia Yaeleweka vema ikiangaliwa kwa "jicho la ndani"
Image from The Summit Blog
Bado naendelea kuamini kuwa suala la UBAYA na UZURI wa kitu ni tafsiri itokanayo na uhusianishaji wa kilichotendeka sasa na mfululizo wa kilichotokea ama kitakachotokea. Kwa maana nyingine ni kuwa bado naamini katika kile nilichoandika Septemba 14, 2009 kuwa Hakuna kibaya kisicho na uzuri...... Yategemea umeachia wapi kuoanisha na tukio (irejee hapa). Na hili laendelea kujidhihirisha maishani mwangu.
Labda niseme kuwa maisha tuishiyo binadamu wengi ni tofauti saana tuwapo na raha na pale tuwapo na hofu. Umeshawahi kuwa kwenye chombo cha usafiri halafu ukatikea mtikisiko ambao unaashiria mwongozaji kupoteza uwezo wa kumili chombo? Utasikia sala zisemwazo na MUNGU aitwavyo. Ni kwa kuwa tukiwa "wahitaji" twafikiria mbaali zaidi ya tufanyavyo tukiwa na "raha". Na katika maisha ni vivyo hivyo. Wapo walio makini kuwaza mpaka tukio lilipoishia na si uwezekano wa ambacho kingetokea kama kile kilichotokea kisingetokea wakati ule.
Na kibaya zaidi ni kuwa wanawaza katika UPANDE HASI PEKEE bila kuwaza CHANYA ya kile kutokea wakati huo. Niliwahi kumsikia mfanyakazi mwenzangu akisema anatamani asingepewa ruhusa alipoomba (akidanganya) kwenda kumpokea mwanawe ilhali alikuwa anaenda kwa mpenziwe na kisha akafumaniwa. Nilisikitika kuwa amefikia kiwango cha KUTAMANI ANGENYIMWA RUHUSA lakini ninaloamini ni kuwa angenyimwa, basi angekasirika na angelichukulia hilo kama jambo HASI (negative) kwake. Na kama angeishia hapo (aliponyimwa ruhusa) asingeona u-CHANYA wa kunyimwa ruhusa huko ambako ndio kungekuwa kumuepusha na fumanizi.
Miezi kadhaa iliyopita nilikamatwa na askari kwa kuzidisha mwendokasi. Ilikuwa ni mwendokasi ambao hata sikujua kuwa nilikuwa niko zaidi ya kiwango kitakiwacho kwa kuwa nilikuwa nikiwaza mengi yaliyochukua umakini wangu. Lakini ukweli ni kuwa nilikuwa ninaendesha 84mph katika sehemu inayostahili 55mph. Niliposimamishwa na askari nilishukuru. Na licha ya adhabu iliyokuwa mbele yangu, nilifikiria ni nini kingetokea kama (kwa kupoteza umakini nilikokuwa nipoteza) ningeenda nje ya njia na kugonga nguzo, ama gari nyingine, ama kupata ajali ya aina yoyote? Je nisingetamani kama ningekuwa nimekamatwa na kulipa faini kubwa (ambayo haitafanana kwa vyovyote na kugonga gari ama nguzo)?
Hebu fikiria kama mkianza safari kisha tairi ikachomoka utawaza nini? Wengine husema huo ni mkosi japo nafikiri ni afadhali ya hilo kuliko tairi kuchomoka wakati mmeshafika mbali na mkiwa kwenye mwendo kasi mkubwa.
Eti watu wakioana na kuachana ndani ya muda mfupi wapo wanaouona huo kama mkosi japo (licha ya kutopenda kuvunjika kwa ndoa yoyote) naamini ni heri hiyo kuliko kama wanandoa wanaishi miaka 20, wanazaa watoto pamoja kisha wanatalakiana na kuacha watoto wakiteseka wakiwa hawajajengewa msingi imara wa maisha.

Kwani ni kipi ambacho kinatokea kikiwa na u-HASI na ambacho hakina u-hasi zaidi? Na kuna haja gani ya kung'ang'ania u-hasi ilhali kuna uwezekano wa kushikilia u-chanya ambao (hata kama hautupi matokeo ya papo kwa hapo) yanatuwezesha kuwa na "moyo" wa tumaini (ambalo wakati mwingine twauhitaji) ili kuweza kusonga?
Na kuna haja gani ya kung'ang'ania ambacho hakionekani kuwa na suluhisho na hata mtazamo utakaopunguza aina yoyote ya uwezekano wa kupata suluhisho

Ni kwa kujiuliza haya, najitahidi kuwa na mtazamo chanya na hivi ndivyo Nionavyo u-CHANYA wa HASI yao.

4 comments:

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

"Niliwahi kumsikia mfanyakazi mwenzangu akisema anatamani asingepewa ruhusa alipoomba (akidanganya) kwenda kumpokea mwanawe ilhali alikuwa anaenda kwa mpenziwe na kisha akafumaniwa."
Oh boy!

Kama tungekuwa tunauona u-chanya ndani mwa u-hasi katika maisha yetu tungeishi maisha ya furaha sana na yenye ridhiko tele. Tusingeweza kusononeka na kukaa tukilalamikalalamika hata kwa vitu vidogo visivyo na msingi.

Unajua, kuna watu waliokosa nafasi katika M.V. Bukoba kwa sababu ilikuwa imejaza abiria pomoni katika bandari ya Bukoba. Badala ya kuuona u-chanya katika tukio lile na kusubiri meli nyingine, wao walikodi teksi na kukimbilia Kemondo kwenda kui-taimu upya. Kilichotokea tunakifahamu.

Inabidi umtafute huyo "trooper" aliyekupa tiketi ya kwenda kasi umnunulie bia.

Mzee wa Changamoto said...

Ni kweli kabisa Kaka.
Nina hakika kuwa wale walioachwa na Mv Bukoba walililia pesa zao mpaka kulipokucha wakasikia kilichoikuta meli hiyo.
Hapo kuna ambao ninawafahamu ambao WALIENDA KUTOA SADAKA KANISANI wakiuona "ukuu wa Mungu" (u-chanya wa kukosa meli siku hiyo).
Ingetokea vipi kama isingezama?
Na je wangefika mwanza wangekuwa salama?
Pengine waliepushiwa ajali ya barabarani ndani ya Mwanza, ama kuporwa ama kujeruhiwa ama baya jingine.
Lakini nina hakika SADAKA ile waliyoitoa wasingeifikiria kama mambo yangeenda sawa.
Na ndio maana kama nilivyoanza kwenye bandiko langu, "Bado naendelea kuamini kuwa suala la UBAYA na UZURI wa kitu ni tafsiri itokanayo na uhusianishaji wa kilichotendeka sasa na mfululizo wa kilichotokea ama kitakachotokea"

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

hasi ni muhimu kwa chanya na chanya pia

Albert Kissima said...

-ngali- na -ngeli- ni miongoni mwa maneno ambayo hudhihirisha mtu aliyeshindwa kuzitawala nguvu za U-chanya na U-hasi wa jambo na ni kweli kuwa wengi wetu hatumudu kuzitawala nguvu hizi.


Wapo wanaokufa kwa kujinyonga,kwa shinikizo la damu,wanaokosa raha n.k kwa sababu tu ya kushindwa kuzitawala nguvu hizi. Lakini pia kuzitawala nguvu hizi nakiri kuwa ni kazi ngumu kwani zina ushirika mkubwa sana na hali za maisha tulizonazo wanadamu.
Yupo mama mmoja aliyemuua mwanae kwa kuwa alichukua "mhogo" aliokuwa ameuhifadhi kwa ajili ya mlo. Yupo baba aliyemuua mtoto wake kwa kuwa alitengewa "ugali wa maziwa" badala ya "ugali na nyama" kwani wakati anaondoka aliwaachia vipande vichache ambavyo hata watoto havikuwatosha. Naamini wote hawa baadae walikuja kujuta na kugundua u-hasi wa maamuzi yao.

Yawezekana kupunguza kutawaliwa na nguvu hasi kwa kujijengea hali za utulivu ktk kuyakabili mambo na kikubwa zaidi kujijengea uvumilivu na kuhitaji msaada wa ushauri inapobidi japokuwa yote haya kwa upande mwingine yanaweza pia kuleta matokeo ambayo yanahusishwa na nguvu hasi.