Sunday, April 17, 2011

Wewe si wewe pekee....ni KILA MMOJA ndani yako.

Kuna watu wanaoamini kuwa FULANI ni mwema ama m'baya na kuachilia mbali kilichomfanya ama asili ya "uzuri" ama "ubaya" wake. Lakini haijalishi watafsiri vipi UBAYA ama UZURI wa kitu ama mtu, bado tunatambua kuwa maisha ya yeyote katika hali yoyote YANATENGENEZWA na pilika, mahusiano na mchakato wa kila siku wa mtu na wale wamzungukao. Jumatatu ya Desemba 29, 2008 niliwahi kuuliza kama Umemshukuru ama kumuombea adui yako (rejea hapa) na kisha Jumatano ya Aprili 8, 2009 nikaeleza kuwa Huwezi kuwashukuru wote, waombee tu! (rejea hapa pia). Lakini ambalo sikuweka bayana ni kile ambacho wengi hushukuru, kutukuza na ama kulaumu na kupuuza mwanzo wa baraka ama laana hiyo. Ukweli ni kuwa KILA UONALO linabadili mtazamo wako wa maisha. Linabadili fikra ya namna unavyoyatazama maisha (iwe kwa kuyafanya yaonekane magumu ama marahisi) na pia linakupa taswira ya maisha ambayo ni kuboresha uliyokuwa nayo ama taswira mpya ya maisha.

Ukweli ni kuwa KILA UTENDALO linaathiri maisha yako. Hii ni iwe kwa kudhamiria ama la. Iwe kwa uwazi ama kwa siri. Lakini utendalo litaathiri kile maisha yako. Na ndio maana wale wanaofunzwa kuhusu DHAMBI wanaendelea kuishi nazo hata kama walitenda bila uwepo wa mtu mwingine. Aziniye ataendelea kuwa na "furaha" ya uzinzi wake kama anaamini kuwa kuzini ni jambo halali na pia yupo atakayeishi na lawama juu ya uzinzi wake kwa kuwa anaamini kuwa kuzini ni kosa. Hisia hizi zitaendelea kuwepo hata kama uko peke yako ama na mtu tofauti na yule uliyezini naya. Ni kwa kuwa ULITENDA.

Ukweli ni kuwa KILA USIKIALO linaathiri maisha yako. Ni kwa kuwa kisikiwacho hakiondoki akilini kwa utashi wa msikiaji. Ni kama kuona. Na ndio maana ukishaona na kusikia utaendelea kuwa na kumbukumbu (iwe njema ama mbaya) ya ulichoona na kusikia.

Ukweli ni kwamba KILA JEMA NA BAYA (kwa mujibu wa tafsiri yako) linabadili mtazamo wa maisha yako. Wapo wanaosema kuwa walikuwa wema lakini waliyotendewa yamewafanya wawe watu wabaya. Wapo ambao HAWANA IMANI tena kwa watu wengine kwa kuwa wale waliowaamini "walivunja" imani yao. Wapo ambao "wanatoa ushuhuda" wa namna ambavyo wema uliotendwa kwao na mtu mmoja uliwafanya wautazame ulimwengu na watu kwa jicho jingine, na kisha kubadili maisha yao kwa ujumla.


Swali kuu hapa ni kuwa NI NANI akuonyeshaye, akutendeaye ama akusikilizishaye? Si wewe. Ni mwingine. Ambaye naye yuko alivyo kwa kuwa kuna aliyebadili ama kuimarisha maisha yake. Naye aliyetenda hayo alikuwa ni "zao" la mwingine na mwingine na mwingine. LABDA ndio maana watu huaminika kufanana tabia ndani ya vizazi kwa kuwa bado sisi ni sehemu ya fikra na matendo ya waliotutangulia. Ni kweli kuwa wewe uko ulivyo kwa kuwa uko hivyo? Ni kweli kuwa hizo ni juhudi zako pekee?

Labda umekuwa jasiri kwa kuwa waliokuwa pembeni yako na ulioamini walistahili "kukutetea" hawakufanya hivyo...NA SASA UNAJIVUNIA.

Labda umekuwa mzembe kwa kuwa waliokuwa pembeni yako walikufanyia na kukuzoesha kukutendea kila kitu.

Kwa namna yoyote ulivyo, ni kwa kuwa wapo walioathiri fikra na matendo yako. Kwa mawazo, maneno na matendo.

Ukweli ni kuwa "Wewe si wewe pekee....ni KILA MMOJA ndani yako"


Na hivi ndivyo nionavyo hili, labda NAMNA NIONAVYO TATIZO, NDILO TATIZO.

Jicho la ndani ni kipengele kinachoangalia mambo kwa mtazamo wa ndani na tofauti. Kwa mabandiko yaliyotangulia hili, BOFYA HAPA

5 comments:

Albert Kissima said...

Ni kweli kabisa. Maisha tuliyo nayo kwa kujua ama kutojua, ni matokeo ya wale watuzungukao. Hili halipingiki. Ndio maana (kama ulivyotangulia kusema) watu wa jamii fulani wanaweza kuwa na mfanao wa tabia.

Watu hupenda kujionesha kuwa wana misimamo kama ishara ya kuweza kujitegemea kimaamuzi, kujiamini n.k. Wengi hujua kuwa hali hizi ni wao wenyewe wamejijengea, lakini ukweli ni kuwa, mazingira, hususani watu ndio hutulazimisha kuwa katika hali kama hii ili kuendeleza uwepo au kumudu mazingira husika. Wengi wetu hudhani namna tulivyo ni matokeo tu ya maamuzi yetu lakini sivyo, watuzungukao wana mchangango mkubwa sana wa namna tulivyo.

Simon Kitururu said...

Mmmmh!

Goodman Manyanya Phiri said...

Haya mambo ni mboga na chumvi yake. Mboga bila chumvi kwa wengi hainogi. Lakini ukiongeza chumvi nyingi zaidi watu hawatakula kabisa! BALANCE IS THE KEY!

Kwa namna ingine, mada ni nzuri sana; lakini ipo hatari kidogo. Tusije tukafumba mikono nakudai "Mimi sitaweza kufanya lolote kubadili hali yangu kwani nilichonacho ni urithi tu".

Mawazo ya "urith tu" ndio yanaleta maringo kwa wale "waliorithi" mazuri, na utumwa kiakili kwa wale "waliorithi" ujinga na ufukara. Tena hio ndio sehemu kubwa katika fikra za ukoloni mamboleo ndani ya kichwa cha Mwafrika kama tunavyoongea hivi: tunamlaumu Mzungu kwa ukoloni wake karne iliopita hata kwa uharibifu tunaosababisha sisi wenyewe karne hii... TUMERITHI!!

Mtu anadai "Mimi sikusoma kwasababu nilifiwa na wazazi au mama wakambo alikuwa natabia ya kunisonya ndipo nikaacha kabisa shule". Mbona wako wengi sana waliekuwa na wazazi tena wenye nia na uwezo nao hawakusoma hivyohivyo?


Ukweli ni kwamba: mazingira mengine nje ya "urithi" kutoka kwa binadamu wenzako labda ndio muhimu zaidi. Mmfano maji unaotumia, aina ya udongo, chakula chako ETC vinaweza kusababisha wewe upoteze au uimarishe "urithi" wako huo kutoka kwa "waliokutangulia".

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

nimeupenda mchango wa manyaya

ila sasa inabidi tuangalie vizuri angalizo la manyanya juu ya visingizio.

lakini mada labda ina ukweli. kuna vitu ambavyo huwa sipendi kuvifanya lakini nalazimika kutokana na kuzungukwa na wengine

kwa mfano, huwa sipendi kuvaa nguo mwili mzima, natamani kuwa huru, kuwa uchi unakuwa huru

huwa sipendi kuhudhuria chooni kwa kufungu mlango, kiuhalisia huwa napenda mlango huwe wazi, nihudhurie huku nikipata kaupepo na haraufu iishe haraka, kwa kuwa nimezungukwa na watu, basi najikuta mtumwa!

Mzee wa Changamoto said...

Ameen kwa WOTE.
Kaka Phiri, ulilosema ni sahihi, ila ujue kuwa HAKUNA ANAYEWAZA HAYO BILA ATHARI ZA JAMII. Kwa hiyo bado tunarejea palepale kwamba mambo ya URITHI na mengine huanzishwa na wale waliokukuza. Wanaokufanya uamini katika mali za "kupeana" na ambao wanaamini kwamba unastahili kuwa na sababu ya kujifariji kwa kila baya linalokukuta.
Unaamini kwamba hakuna walio katika hali kama ya hao lakini wakafanya kinyume nao?
BADO SUALA LA URITHI NI SUALA LA KUFUNZWA NA KUFUNZANA.
Ina maana ni suala la ATHARI ZA WENGINE.
Nawaza kwa sauti tuuuu!!!