Monday, April 5, 2010

Za Kale vs Maisha ya Sasa...SHUKRANI KWA MJOMBA

Tarehe 8 April 2009 niliandika juu ya suala la shukrani kwa wale waliotuwezesha kufika mahala tulipo nikisema Huwezi kuwashukuru wote, waombee tu!!!(isome hapa) na nilizungumzia namna ambavyo maisha yetu HUGUSWA na watu wengi. Sisi hupita kwenye mikono ya wengi na kwa maana hiyo, kufanikiwa kwetu ni matokeo ya ushirikiano wa watu wengi sana. Na jana nilipokuwa napitia vibaraza mbalimbali KUJIFUNZA, nikakutana na bandiko hili la Mfalme Mrope (lisome hapa) ambalo nalo limezungumzia kwa mfano suala zima la kutowasahau wanaotufikisha tulipo. Ni rahisi saana kutokumbuka UHALISIA wa uhitaji tunaokuwa nao punde tuondokanapo na hitaji tulilonalo.
Pengine si kazi rahisi kuwashukuru wote na kama nilivyosema awali kuwa kubwa tuwezalo kufanya ni kuwaombea, lakini pale tuwezapo, twahitaji japo kuwatembelea na kuwajulia hali katika KUONESHA KUTHAMINI MCHANGO WAO KWETU.
Msingi mzima wa kuwathamini waliotuwezesha kwa namna ya kuwajulisha kuwa twathamini mchango wao kwetu ni jambo muhimu kulifanya. Si wakati wote ambao twajua liendelealo "nyuma ya pazia" ambako wale washirikio kwenye ukuaji wetu hukumbana na makwazo na mambo mengi kupima kile wafanyacho.
Pale tuwezapo na tuwashukuru lakini kwa tusioweza kuwaona na kuwaonesha thamani ya mchango wao kwetu, basi TUWAOMBEE.
Na jumatatu ya leo tuungane na mkongwe Muhidin Maalim "Gurumo" akiwa na Orchestra Safari Sound Band ambao wanatukumbusha funzo la kuthamini waliokwenda hatua kadhaa kutufanikishia maisha yetu.
Sikiliza wimbo wao SHUKRANI KWA MJOMBA

** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia kila Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama mitandao shirika hapa** . Ama ili kuweza kujua tasnia nzima ya muziki na wanamuziki wa Tanzania BOFYA HAPA

2 comments:

Unknown said...

Swadakta kaka hii imetulia...

Yasinta Ngonyani said...

za kale ni safi sana Ahsante kwa kipengele hiki!!