Nikiwa na baadhi ya wasanii walioshiriki wimbo ulioitwa HAKUNA (urejee hapa). Hapa ni ndani ya Bacyadr Studio kurekodi Video ya wimbo huo uliokuwa maalum kumuenzi Justin Kalikawe
Tukiwa Idara ya Habari Maelezo (2003) na Ras Pompidou, Jah Kimbuteh, Ras Inno, Bi Georgia (Mjane wa Justine) na meneja wake wa zamani Allen Mbaga kuzungumzia Tamasha la HAKUNA lililomuenzi Justine
Jana ni kati ya siku nilizokumbuka meengi saana kuhusu nyumbani. Na ni katika kuwaza huko nikajikuta nawaza SAFARI YANGU YA MAISHA na kujiuliza msururu mzima wa matukio ya maisha yangu. Nikawaza nimetoka wapi, niko wapi na pengine ninaenda wapi. Kama ilivyo kwa wengi wetu, tunaweza kuwa na majibu ya maswali ya tulipotoka na pengine tulipo (kwa mtazamo wetu0 lakini tuendako bado ni KITENDAWILI. Na ni kitendawili hicho tunachojiuliza ambacho kina meeengi yanayohitaji muda zaidi ya tujipao katika kusaka majibu. Nilipofikiria tulikotoka na kilichonileta huku na ninavyosonga ki-umri na kuwaza mustakabali (future) ya maisha yangu na familia, nawaza mengi. Lakini ni jana hiyohiyo ambapo Kaka Gotha Irie alinitumia picha ambayo tulipiga mwaka 2003 wakati tukirekodi video ya wimbo HAKUNA wake Justine Kalikawe. Hivyo nikaenda kumsikiliza Justine na kukutana na wimbo huu ambao nimeona nishirikiane nanyi kwa mara nyingine.
"nilikuja kutafuta ugenini, nikazoea pakawa ni nyumbani, sasa ninaelekea uzeeni, nibaki huku au nirudi nyumbani. Nilioa nikazaa na watoto, na nilipotoka kwao ni kama ndoto; lakini najiuliza siku nikirudi kwetu, niende nao au wabaki huku"
Hayo ni maneno anayoanza nayo mwanamuziki aliyepata kufanya vema saana katika miondoko ya Reggae nchini Tanzania Marehemu Justine Kalikawe katika wimbo wake Kitendawili. Kama ilivyo kwa nyimbo nyingi ambazo zinakuwa na UJUMBE HALISI wa maisha kwa hadhira, wimbo huu bado unaendelea kuwa na maana na mguso uleule kwa wale walio mbali na nyumbani na hasa wale walioanzisha familia ambapo ikifika suala la maisha baada ya kustaafu unarejea kujiuliza kama alivyojiuliza Kalikawe.
Haijalishi alitunga wimbo huu akiwa wapi, ama akijifikiria kama aliye wapi, lakini kwa kuwa alifanya kile afanyacho vema zaidi kwa kutunga nyimbo zenye uhalisia kwa jamii, bado sasa hivi ndugu wengi tulio mbali na nyumbani tukiusikiliza wimbo huu tunapata hisia halisi ya alichoeleza Justine na kuweza kujiuliza maswali ambayo naye aliuliza kwenye utunzi wake huu, bado ujumbe wake unawagusa wengi ambao kwa bahati mbaya kutokana na mfumo wa maisha ya sasa wameelekea popote duniani kwa namna yoyote kusaka chochote ili kuweza kurejesha uwekezaji nyumbani, na kama ilivyo kwa binadamu yoyote, unapofika mahali ndio unapoanzisha urafiki na "udugu" na uliokutana nao, na wakati muafaka ukifika unaanzisha familia na kwa majaaliwa ya Mungu unapopata watoto inakuwa baraka, lakini baadae waweza kujiuliza kama aliyojiuliza Kalikawe kuwa "nilikotoka niliishi na wazazi, babu na bibi, mjomba na shangazi, lakini huku mimi na familia, ndugu wengine ni eneo la kazi eeeee; katikati kuna bahari, tena ni mbali elfu kumi maili, nikisafiri nafika alfajiri tena ni mbali natumia utajiri eee"
Sijui la kusema, lakini namkumbuka Justine kama moja ya nguzo za muziki wa Reggae mkoani Kagera na Tanzania kwa ujumla. Alitumia lugha zake za Kihaya na Kiswahili kufikisha ujumbe aliokusudia kwa jamii husika na mara zote ALIELIMISHA, AKIBURUDISHA NA AMA KUIFUNZA JAMII KUJIKOMBOA KUTOKA KATIKA UTUMWA WA KIAKILI.
Justine alifariki ghafla mwezi wa nane mwaka 2003 katika Hospitali Kuu ya Mkoa wa Kagera mjini Bukoba miezi michache baada ya kurejea kutoka ziara ya kimuziki nchini Denmark. Aliacha mjane Georgia na watoto wawili Abayo na Niwe na mpaka mauti yanamkuta alikuwa ndiye msanii mwenye albamu nyingi zaidi za Reggae nchini Tanzania (8 za audio na 3 za video katika miaka 16 aliyodumu katika muziki wa Reggae). Katika kumuenzi, wasanii nyota wa Reggae nchini walitunga wimbo wa HAKUNA na kuandaa Tamasha maalum la kuenzi kazi na maisha ya Justine lililofanyika Don Bosco. Tulishapata kujadili FIKRA PEVU / MAONO ya Justine Kalikawe katika wimbo wa HAKUNA kwa kuhusisha na uchaguzi ujao HAPA
RIP Justine Kalikawe
Bofya player kusikiliza KITENDAWILI hiki
**Them, I & Them ni kipengele kikujiacho kila Ijumaa kinachoelezea kazi za wasanii (Them) kulingana na maono yangu (I) kwa ajili na manufaa ya hadhira (Them)**
Kwa nyimbo zaidi ndani ya kipengele hiki bofya hapa.
IJUMAA NJEMA
6 comments:
"Wewe baba yetu na wewe mama yetu, babu na bibi waliwazaeni, halafu wakawalea mkakua katika amani, na hiyo ndiyo furaha yetu sisi kama wanadamu, lakini mbona sasa mnatuharibia sisi amani yetu." UTARATIBU WETU WENYEWE UNATUKANDAMIZA SISI WENYEWE YEEH YEEH! May his soul RIP. MZEE WA UPANGA NA MTOTO WA TAMBAZA.
Kaka, sifahamu nikushukuruje siku ya leo. Ahsante sana.
Mimi nimefurahi mno leo kwa kuona umezungumza kuhusu Justine Kalikawe. Ni mwanareggae niliyempenda sana. Nitampenda daima huku nikijivunia urithi wa muziki wenye ujumbe ugusao hisia zangu.
Siisahau Agosti 13, 2003 nilipomsikia mtangazaji wa Redio Free Afrika, Prince Baina Kamukuru akitangaza kututoka kwa Justine. Ilinichukua muda kuamini. Nilipolazimika kukubali ukweli, nilishika kalamu na karatasi na kuandika mistari kuelezea hisia zangu kwa kifo chake.
Justine ni shujaa wa kweli wa reggae.
Namwomba Mwenyezi Mungu azidi kumwangazia mwaka wa milele, na kuifariji familia yake.
Amina.
kifo chake wanakihusisha na mizengwe ya tajiri mmoja pale bukoba eti ni kweli?
Kaka Baraka. Huyu ndugu alikuwa na MASHAIRI ya kina. Mashahiri ya haja. Na nakumbuka tulipokuwa tunatoka Zamunda studio (kwake Athanas Sajula) ambako alikuwa akirekodi, kuna mtu alizungumza kuhusu uwezo wake wa kuandika nyimbo na kuzifanyia mazoezi ama rekodi ya mwanzo kisha akarejea kuzimalizia na akatuambia kuwa alikuwa na nyimbo zinazotosha zaidi ya albamu 2 ambazo alikuwa akizifanyia mazoezi lakini zilikuwa hazijakamilika kurekodiwa. Mpango wa awali nakumbuka ulikuwa zimaliziwe na wasanii wa Tanzania Reggae Family kisha mapato yote yakamfae mjane na watoto. Sijui lilipoyeyukia. Kisha likaja wazo la kila msanii wa Tanzania Reggae Family kuchagua wimbo mmoja wa Justine halafu je ufanyiwe mazozei na kuimbwa na msanii huyohuyo na mafao yakaisaide familia yake. Nalo likayeyuka. Duh!!!
SIJUI TUTAMUENZI VIPI MTU HUYU.
@Kaka Fadhy. Nafurahi kama nimeweza kurejesha hisia halisi za mwanaharakati.
Mimi kwangu taarifa za kifo chake zilikuwa zaidi ya mshtuko. Nilikuwa namsaka kufanya naye mahojiano baada ya kumkosa alipokuwa Dar na nilipoenda Bukoba nikaambiwa kuwa amerejea toka nje ya nchi na alikuwa akitegemea vifaa vyake vya muziki kuwasili pia. Nikajua atakuwa na mengi mapya ya kuueleza umma. Siku hiyo Mamangu ambaye ni muuguzi Hospitali ya Mkoa alipokuja na kuniambia "ulikuwa unamtafuta Justine Kalikawe?" nami kwa shahuku kuwa amemuona na kumwambia na pengine kuniwekea miadi nikasema haraka NDIO, YUKO WAPI? na akasema kwa huzuni kuwa "AMEFARIKI GHAFLA LEO PALE HOSPITALINI"
Iliniuma. Nilishiriki maziko na mazishi yake mwanzo mpaka mwisho na ilisikitisha kuwa mtu ambaye ametangaza mkoa na tamaduni za Kagera alizaikwa bila hata afisa Utamaduni kuwepo. HAKUNA KIONGOZI / MWAKILISHI WA SERIKALI ALIYEKUWEPO MPAKA TUNAZIKA.
Tutamuenzi kwa kazi zake alizotuachia.
@Kaka Kamala. Nasikia habari juu ya "kuwekezwa" ili biashara ya mtu isonge mbele. Nilipikuwa Bukoba nilitamani saana kwenda kwenye hiyo hoteli ambayo mwenye nayo anahusishwa na kifo chake lakini mara zote ningesikia mtu akisema "kule ukienda ukakaa hadi usiku sana utamuona Justine Kalikawe". Sikuwahi amini kwa kuwa sikumuona ila nilihisi hiyo dhana inampunguzia wateja saana kwani yaonesha inaaminiwa na kundi la watu wanaotosha kushawishi baadhi ya wageni kutokwenda huko. Japo siamini lakini sidhani kama ningeweza kwenda kama nimeambiwa kuwa atanitokea usiku na zaidi kama najua naenda lala peke yangu.
BLESSINGS TO YOU ALL
Marehemu astarehe kwa amani peponi amina. Tutazidi kukukumbuka kwa njia ya miziki yako.upendo daima
Yaani Mubelwa umenikumbusha mbali sana mpaka nimekumbuka DJ wetu Marehemu Kali Kali R.I.P Kalikawe
Post a Comment