Wednesday, July 14, 2010

Tanzania yangu.......Isiyojua kuziba ufa, wala kujenga ukuta

Image Credit: SECURE CHANNEL
Alhamis ya Januari 14 niliandika bandiko Niangaliapo HAITI naiona TANZANIA (irejee hapa) nikihusisha niliyoyaona HAITI wakati na baada ya tetemeko na nilivyokuwa nikiichungulia nchi yangu TANZANIA. Nikaangalia MAANDALIZI ya nchi yangu katika majanga ya asili na yale tusababishayo na namna ambavyo tunajitahidi kuyazuia ama kukarabati pale tulipochelewa. Sehemu ya bandiko hilo niliandika nikisema
"Tukumbuke kuwa Tanzania (na hasa Dar Es Salaam) iko katika hatihati ya kukumbwa na athari za ongezeko la kina cha maji na ilionja athari za Tsunami japo haikuwa na madhara. Sasa nawaza................
Hivyo "vikwangua anga" ninavyosikia "vinaota" kila siku vimejengwa kuweza kuhimili matetemeko ya ardhi ama ndio mwendo wa "kitu kidogo" tusonge? Na ziliishia wapi tetesi za kupinda kwa jengo la Mafuta House? Ni kweli kuwa majengo yote yanayojengwa sasa jijini ni salama na yanafikia kiwango cha kuhimili athari kama haya?
Kwa mji kama Dar Es Salaam, kuna urahisi gani wa waokozi kuwafikia watakaokuwa matatizoni iwapo litatokea? Kama majengo ndio haya (ambayo ubora wake hatuujui) na barabara hazipanuliwi wala kuboresha mfumo wa usafiri wa ardhini, ni vipi tunajiandaa kiuokozi kwa matatizo yasiyoepukika kama hili lililotokea Haiti?
"
Japo sijasikia tamko lolote kuhusu mambo ambayo niliwahi kuzungumzia (na pengine sikutegemea kusikia lolote kwa kuwa hakuna anayejali), lakini bado nawaza kama yale tuyaonayo yakitendwa ama kupangwa na serikali yana mipango ya kuzuia ama kutatua tatizo.
Kila wakati nasikia MISAADA YA VYANDARUA IMETOLEWA kwa ajili ya kujikinga na mbu ambao wameachwa kuzaliana, na bado twajua kuwa misaada hiyo yaweza kuwa aghali kuliko gharama za kuua mazalia ya mbu. Nawaza ni kipi kilicho chema zaidi? Kukinga mbu wasizaliane ama kuzuia mbu waliozaliana wakati wa kulala ilhali wanaendelea kutuuma tunapoenda "kuchanja kuni" ama tutumiapo vyandarua hivyo kimakosa?
Tatizo nilionalo hapa ni kuwa MBU HAWAZUIWI KUZALIWA na hata juhudi za kuwazuia waliozaliana wasidhuru watu si halisi.
Niliwahi kuandika juu ya Tanzania Yangu.... Ijengayo Ghorofa ikipuuza msingi (irejee hapa) ambamo humo nilishangazwa na utaratibu wa kiutawala wa nchi yangu ambao hauoneshi kujali CHANZO CHA TATIZO zaidi ya kulipuuza na kisha kuweza hata kupuuza TATIZO LENYEWE.
Image: NYDaily News.com
Na sasa naangalia sakata la uchafuzi wa Ghuba ya Mexico hukooo kusini ya Marekani na nawaza kuhusu pwani zetu. Nawaza wenye dhamana za kuziweka salama na utendaji wao wa kazi. Nimewaza "mnuko" ninaousikia katika fukwe za nyumbani kama ni UCHAFU unaiathiri bahari ama ni nini. Na nawaza zile tetesi za "taka zimwagwazo baharini" na kisha naangalia kama kuna anayehusika kutambua MADHARA YA MUDA MREFU YA UCHAFU HUO na pia kuangalia namna ya kuzuia sasa. Nawaza kama kuna taasisi inayoshugulikia USALAMA NA UBORA WA MAJI NA FUKWE kwa manufaa ya wananchi.
Ni nini chahitajika kufanyika kuhakikisha kuwa TUNAJIFUNZA KUZUIA MAJANGA na pia pale pawezekanapo KUYATATUA?
Naiwaza Tanzania Yangu katika harakati nzima za kuzuia na kutatua.
Iwe ni kuzuia ukosefu wa ajira, RUSHWA, UFISADI na hata USALAMA WA WATU KUTOKANA NA UWEKEZAJI KAMA HUU na hata malipo kwa waathirika. Na licha ya hayo yote, hatuoni HARAKATI ZA KUREKEBISHA MAKOSA YALIYOTOKEA.
Hivi majuzi SERIKALI IMETANGAZA KUWA MAJI YA KWENYE MTO ULIOATHIRI WATU YAKO SALAMA KWA MATUMIZI YA BINADAMU (bofya hapa kujisomea)

Na hili lanifanya niiwaze TANZANIA YANGU..... ISIYOJUA KUZIBA UFA, WALA KUJENGA UKUTA

Tanzania Yangu ni kipengele kinachozungumzia ytale yaendeleayo nchini Tanzania na namna ambavyo "ndivyo sivyo" inavyozidi kupamba moto nchini. Kwa matoleo yaliyotangulia BOFYA HAPA


Tuonane "Next Ijayo"

1 comment:

Christian Bwaya said...

Tanzania yetu ndivyo ilivyo. Kila kitu kwa mtindo wa operation. Hakuna program inayoeleweka. Mipango yote kwa miaka mitano mitano. Bado tuna safari ndefu sana.