Jana na leo kumekuwa na habari nyingine iliyonifanya nirejee kujiuliza kuhusu JUHUDI ZA WAHISANI WETU ukilinganisha na za kwetu.
Hivi karibuni tumesikia kuhusu nyongeza ya mishahara huko Kenya imfanyayo Waziri Mkuu kuondoka na zaidi ya theluthi ya pesa anazopata Waziri Mkuu wa Uingereza na pia asilimia kadhaa zaidi ya mshahara wa Rais wa Marekani.

Waziri Mkuu wa Uingereza Mhe David Cameron ambaye aliingia madarakani na kuanza kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya serikali. Aliahidi kufanya hivyo kwa vitendo baada ya kuamrisha kutoongezwa mshahara kwa baadhi ya watumishi.
Na wiki hii, David Cameron ameushangaza ulimwengu pale alipoamua kutotumia ndege ya kukodi wakati akifanya safari yake ya kwanza kubwa kikazi kuja hapa Washington DC kuonana na Rais Barack Obama. Katika safari hiyo, Waziri Mkuu huyo alitumia ndege ya abiria ya biashara (British Airways) na hivyo kuweza kupunguza matumizi ya zaidi ya $300,000 ambazo zingegharamia usafiri wa kawaida wa kukodi.

Nimeshuhudia baadhi ya msururu wa viongozi wa nchi za Afrika (Tanzania ikiwa mojawapo) na ninawaza kama kuna watakalojifunza sasa.
Natambua Rais mmoja barani Afrika (sina hakika kama ni Zambia) aliamua kusitisha ndege ya Rais kupunguza gharama.
Pengine na sisi Tanzania kama tutafikiria hili na pengine kuongeza utendaji kazi wa MABALOZI ambalo litakata gharama za safari za kila uchao za Rais, naamini tunaweza kubaki na vi-senti vya kuchimbisha visima kadhaa vya maji kwa wananchi wanaohitaji saana, kujenga tu-vituo twa afya na mengine mengi.
Kwa ufupi ni kuwa TUACHE KUTUMBUA KULIKO WANAOTUWEZESHA KUWA NA MATUMBUZI HAYO.
No comments:
Post a Comment