Wednesday, January 26, 2011

Kipi chazeeka kwanza? Miili ama akili?

Nikiwa kazini na "rafiki" yangu (ambaye ana umri mkubwa), tulikuwa tukiongelea jinsi watu wanavyoukimbia muonekano wa umri wao. Na yeye alionekana kutetea hilo na kusema kuwa awali alikuwa akionekana ana mvi nyingi kichwani na alijihisi MZEE. Lakini baadae akapata dawa ya kubadili rangi ya nywele zake na hilo likamrejesha katika "ujana" aliokuwa akiutaka. Na baada ya kuonekana kuwa kijana zaidi, akaanza kujihisi kuwa na hata nguvu na uwezo wa kufanya mazoezi. Sasa hivi anakimbia dk 30 za mapumziko ya mchana kazini na amebadili mfumo wake wa chakula, amebadili mfumo wa maisha na kwa hakika sasa anaishi "maisha ya afya" zaidi kuliko ilivyokuwa awali. Hakuna anayebisha kuwa KUJIONA KIJANA kumemsaidia kubadili mfumo mzima wa maisha. Lakini kwangu maswali yakabaki kuwa
1: alizeeka mwili ama akili?
2: Ni kweli kuwa kabla hajajiona kuwa kijana zaidi mwili wake usingeweza kutenda mazoezi afanyayo sasa?
3: Na je! kama angekuwa amezeeka mwili, angeweza kutenda atendayo hata kama angekuwa anapenda kufanya hayo?
Ninawaona wengi ambao kwa kujiona "wamezeeka" hawajiendelezi na shule, hawawekezi maishani na hata hawafanyi mengi mema ambayo yangewasaidia miaka michache ijayo. Wanaokimbia vivuli vyao kwa kujifanyia upasuaji kutafuta muonekano wa ujana, kutumia makemikali "kijijananisha" na hata kuvaa ki-ujanaujana wakiamini hilo litawapa HISIA nzuri za namna walivyo. Pengine inawasaidia kwani wapo ambao wakishakuwa katika "ujana" wautakao huanza kutenda yale ambayo ni ya manufaa kwa maisha yao na zaidi kwa wale wategemezi wao lakini ambayo wangekuwa wamefanya ama walistahili kuyafanya kabla "hawajajibadilisha."
Hivi sasa Baba huyu anaendelea na mazoezi na imekuwa kama desturi. Anaonekana mjana kuliko alivyokuwa takriban mwaka na robo uliopita. Na ndipo ninapoendelea kuwa na kuwaza kuwa alizeeka akili ama mwili? Na kama ni akili, mwili wazeeka vipi? Kama ni mwili, kwanini aonekane kijana sasa kuliko nilipoandika mara ya kwanza?
Haya na mengine mengi hunifanya nijiulize tena na tena.
KIPI CHAZEEKA KWANZA? MIILI AMA AKILI?

KUMBUSHO: Haya ni marejeo ya August 11, 2009. Ni kwa kuwa swali likingaliapo.

6 comments:

Yasinta Ngonyani said...

kwa huyo rafiki yako, labda inawezekana alizeeka kimawazo. Na pia na kuhusu kipi chazeeka kwanza! mimi naamini ni miili yetu kwa sababu akili haizeeki mpaka mtu uwe mkwongwe kabisa hapo ndo akili yako inarudia tena kama ulivyokuwa miaka miwili mitatu. Ni mtizamo wangu tu ruksa kupinga.

Unknown said...

Hivyo ndivyo hasa na mimi nilivyokusudia mwishowe niseme, Yasinta umegusa.

Mwili huchoka kiasi cha kudiriki miguu kuuma na pengine kushindwa kutembea, ni sehemu ya mfano hai halisi. Mwingine utasikia "jamani Kiuno!!"

SWALI:
Je akili ilishalalamikiwa?

Bado naendelea kuwaza changamoto zinazowazika, muziki umezidi kelele.

Rachel Siwa said...

Mimi nadhani ni miili kwanza!!akili inafuatia, nayoakili ikianza kugongana mmhh kazi yake pevu!!!!.

Simon Kitururu said...

Mimi nafikiri hiki kitu hutegemea mtu na mtu! Kuna ambao akili huchoka mapema na utashangaa kusahausahau kumezidi ila bode poa tu na ukumpeleka tena shule hesabu zilezile za zamani inabidi atumia muda au pia milungula ili apasi.

Kuna mshikaji wangu hakumalizia kozi chache ili kupata Digrii sasa hivi ingawa bado anadai kiumbile anakwambia masomo yaleyale ambayo kwa kifupi anayarudia kwa kuanza tena upya chuo hayapandi tena kiurahisi.:-(


Na kwa ujumla mie naamini kuna watu HUBADILI aina za NGUO na kuvaa za ghali, hununua gari jipya ila watibucho na tatizo lao ni lilelile wafanyalo WAJIPAKAO rangi nywele ili kujisikia VIZURI kwa kujihisi ni vijana.


Kwa hiyo kwa kuwa swala hili ni la KISAIKOLOJIA ZAIDI ,...
.... naamini usione mtu kajiachia mvi ukafikiri hana kaudhaifu kake ambako kanaweza kuwa ni kuwa na mpenzi kijana na akawa anatibu ambacho mwingine kabadili rangi tu za nywele na kujisikia vizuri na kudunda na kigoli mzee wa kila siku tokea miaka ya zilipendwa.

Nachojaribu kusema ni:
Kila mtu na tiba zake na si rahisi kustukia kila mtu siri za furaha zake hata ikiwa wote hawajisikii wazee kwa kufuata matibabu tofauti.

Faith S Hilary said...

Sidhani kama akili inazeeka kaka...yes mtu anaweza kusahau baadhi ya vitu na kama alivyosema dada Yasinta hapo, wanakuwa wanarudia akili yao ya utotoni (it's why they say childhood is very important - raises my curiosity though what if someone went through a difficult childhood?). Na hayo mazoezi and eating healthy si ndio mambo ya "forever young"...you don't want to live forever?...haha I'm out! x

Simon Kitururu said...

Labda akili haizeeki lakini UBONGO unazeeka ingawa asemaye ubongo umezeeka na akili imezeeka wanaweza kuwa na maana sawa.


Kama mtu aliye sahau kitu anapata ugumu zaidi kujifunza kitu kilekile achowahi kujifunza nahisi akili au ubongo kitafsiri yangu una aina ya kuzeeka.

By the wei KIBAOLOJIA , cells za ubongo zabadilika karibu kila siku kwa hiyo labda hapa ni tafsiri tu kwa kuwa kuanzia NGOZI ya mtu mpaka UBONGO hubadilika kila wakati kwa hiyo hakuna labda mwenye UBONGO wala ngozi ya zamani KISELI yaweza kuwa ni tafsiri fulania!

Huu ni mtazamo tu!