Thursday, January 20, 2011

Labda ni kweli. Lakini kweli hii si lazima iwe kweli ki-kwelikweli

Photo Credits: Making your own reality blog
Jana nilipokuwa napitia taarifa na habari katika blogu mbalimbali, nikakutana na HABARI HII kwa Kaka Malkiory Matiya kuhusu "namna ya kuzuia watu kunakili habari toka kwenye blogu yako".
Niliisoma na mwanzo nilishangaa nikidhani TUMEANZA KUNYIMANA HABARI, mpaka pale nilipoingia kwenye maoni ambapo Kaka Matiya amekuwa wazi kuwa lengo si kunyimana, bali lilikuwa wazo lililomjia "baada ya kusoma maoni ya mdau mmoja pale kwenye blogu ya jamii," ambaye kwa mujibu wa Kaka Matiya, "alidai kuwa sisi junior bloggers hatuna ujuzi wa IT na hivyo hatuwezi kulinda kazi zetu kama ilivyo kwa blogu ya jamii na hivyo kampongeza mmoliki wa blogu ya jamii kwa kigezo hicho". Maelezo haya na mengine yaliyofuata yalinifanya kuelewa kwanini amefanya aliyofanya.
Lakini baada ya hapo nikarejea kwa MTOA MAONI huyo na hata BLOGU YA JAMII. Nikawaza NI KWANINI TUNAHIMIZA KWENYE KUWEKA "KUFULI" ZA HABARI ZETU BADALA YA KUELIMISHA JAMII UMUHIMU WA KUTOA CREDITS KWA MWANDISHI?
Kwenye post hiyohiyo ya Kaka Matiya, wengi wa wachangiaji (na hata Kaka Matiya mwenyewe) walihimiza umuhimu wa kutoa credits na Kaka Matiya alisema kubwalililompa changamoto ya kufanya hivyo si UCHOYO, bali nia ya kujifunza kitu kipya. Na AKAJIFUNZA, KISHA AKATUFUNZA.
Lakini narejea kwa wadau kama huyo mtoa maoni AMBAO WANAONEKANA KUAMINI KUWA KUFUNGA HABARI NDIO NJIA SAHIHI YA KUENDENDA. Hivi wanawaza nini?
Hivi ni ipi nia ya kuelimisha kama elimu tuitoayo haiwafikii tunaotaka iwafikie? Kwani ni wangapi wanasoma blogu zote?
Mfano halisi wa faida za kushirikiana habari ni UKURASA WA WAVUTI ambao ni chanzo cha habari za pande zote kwa wote, na pia chanzo kikuu cha habari za wengi. Da Subi (kama ilivyo kwa blogu nyingi za MAANA) hutumia blogu na tovuti nyingine kutupa HABARI KAMILI. Subi hutumia picha toka blogu zaidi ya moja kuhakikisha unapata taswira halisi la tukio husika. Mara nyingi hukusanya habari toka kwa blogu nne ama tano.
Na mimi binafsi sio tu kwamba napata habari toka kwingine, lakini pia hata niandikazo (kama hii) zatokana na mawazo kutoka blogu nyingine, na mara zote huwa ninatoa credit hata kwa yule aliyeandika kitu kilichonipa WAZO LA KUANDIKA.
Labda TUHIMIZE KWENYE UTOAJI WA CREDIT KWA CHANZO CHA HABARI.
Ni akili zilezile tulizonazo kuhusu KUTOKOMEZA UKIMWI NA MALARIA.
Yaani wapo (na hata viongozi) wanaoamini kuwa matangazo ya matumizi ya kondom na vyandarua ni njia muafaka kutokomeza maradhi haya, JAMBO AMBALO SI KWELI
Labda ni kweli kuwa kutumia kondom yaweza kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Labda ni kweli kuwa vyandarua vyaweza kupunguza maambukizi ya Ukimwi.
Labda ni kweli kuwa kuweka copyright kutaweza kuzuia wengine "wasiibe" post
LAKINI NI KWANINI TUSIZUIE CHANZO CHA HAYA YOTE?
Kwanini tuwekeze kwenye kuhimiza manunuzi ya kondom na vyandarua (ambazo ni biashara za watu na wananufaika na hili) ilhali tunaweza himiza kwenye kuua mazalia na kuzuia maambukizi ya malaria na VVU?
Kwanini jamii yetu isiwekeze kwenye kuhimiza umuhimu wa KUTHAMINI KAZI YA MTU na kuonesha umoja kwa wote tutakaposhirikiana kusambaza NENO JEMA kuliko kuendelea kumtukuza yule "anayebania" habari?
Labda masuluhisho tuliyonayo ni ya kweli, lakini si lazima kuwa ukweli wa masuluhisho haya, yawe na ukweli wa kikwelikweli kuzuia kile tutakacho.
Na huu ni mtazamo wa namna nionavyo tatizo, LABDA NAMNA NIONAVYO TATIZO NDIO TATIZO

10 comments:

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Plagiarism ni kosa kubwa hasa vyuoni. Kwa wale waliowahi kusomea kwenye vyuo vya huku wanajua hili ingawa sijui kama ni vyuo vyote vinahimiza hili.

Hakuna haja ya kuzuia mtu kuchota habari toka kwako. Hata BBC na Reuters hukopiana lakini muhimu utoe rejea (Attribution) ulikopata hiyo habari. Hii inakuza ujuzi na kujitafutia na kufundishana.
Hii si mbaya ila ni muhimu pia kuzingatia kuwa kuna haja ya kufanya mambo kisomi na si kimazoea. Mie kwa mfano, kwenye blogu yangu unaweza kunakiri chochote hata kama hutatoa rejea au utajo. Lakini inafurahisha mtu kurejea alikopata habari ingawa si mara zote habari nyingi hufuata mfumo huu.

Unknown said...

Naungana na NN Mhango kwa nyongeza. Hivyo ndivyo inavyopaswa kuwa ili kusisitiza thamani ya kazi husika...mfano wa BBC na Media zingine ndio sheria hasa ya vyombo vya habari kokote, ndio maana ukifuatilia hasa tulio katika tasnia ya habari twafahamu kuwa mwisho wa habari yako ni vyema kusema habari hii ni kwa msaada wa...:(mashirika ya habari ya kimataifa, mtandao ama ni kwa msaada wa blog ipi na pengine website)

Ni kukumbushana tu ndio muhimu.

Yasinta Ngonyani said...

Naafikiana na waliotangulia kwani kueneza habari ndio kujifunza na kama alivyosema mzee wa Changamoto pia wasomaji wetu hawatembelei blog zote. Kwa hiyo cha muhimu ni kukumbushana au kutosahau kutaja wapi umepata. Kwa kufanya hivi itakuwa wote tumefaidi na kuelimishana.

malkiory said...

Mubelwa yaelekea ujumbe uliwafikia wadau kwani usiku wa siku niliyoandika hiyo posti blogu ya jamii ilikuwa na kufoli lakini asubuhi yake nilikuta kofufuli imetolewa na hadi leo ni ruksa ku-kopi na ku-pesti.

Rachel Siwa said...

Naungana na wote waliotangulia,mfano ni huu hii habari nimeipata hapa na hapa aliipata sehemu nyingine ,pia nimefaidika kuijua blog ya Malkiory amboyo ni chanzo cha habari!

Ubinafsi haujengi.

Aksante kaka Mubelwa na wengine!

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

kana nisingetaka kazi yangu inakiliwe, basi nisingeandika, ningekaanayo kwangu tu

emu-three said...

Ni kweli ujumbe umefika, sisi sote ni ndugu na udugu wetu ni kusaidiana. Kuna mzungu mmoja alisema Waafrika sio masikini kama watu wanavyozania, angalia jisni gani wanavyopendana, je kuna UTAJIRI GANI MKUBWA ZAIDI YA KUPENDANA. KIDOGO walicho nacho wanachangiana...hebu nenda kwa mzungu kama hujaalikwa kama utapewa tonge...
Kwahiyo kama wewe umejaliwa kujua hiki, wapo wengi hawajui, na hawana nafasi hiyo,labda wangepata wangejua,. Ndio maana kukopi na kupaste imekuwa jadi yetu.
Kwa wale wanaojua umuhimu wa kutoa credits, ni vyema kabisa, na hiyo ndio ahsante ya aliyetunga.
Ahsante nayo ni moja ya jadi zetu, basi na wewe ukikopi kazi ya mtu fulani mpe ahsante kwa kusema umetoa wapi...AU SIO JAMANI

Masangu Matondo Nzuzullima said...

Pengine nikopi na ku-pesti tena maoni yangu niliyoyatoa kule kwa Matiya, maoni ambayo kimsingi hayatofautiani sana na ya Mwalimu Mhango. Nilianza hivi:
==============
Oops! Kumbe siwezi hata kuyakopi na kuyadondosha maoni yangu hapa kwani yametiwa kufuri na Bwana Matiya. Ningependa msome hasa maoni yangu ya mwanzo na ya mwisho (jibu kwa Dada Koero) kutoka katika blogu ya Matiya. Asanteni!!!

malkiory said...

Matondo, kofuli ilikuwa ya majaribio tu sasa imetolewa. Yafuatayo ni maoni ya Matondo dhidi ya Matiya, Mbele na Koero:

Asante kwa hili. Mimi hata hivyo nina maoni tofauti kidogo kuhusiana na jambo hili.

Mimi nadhani kwamba badala ya kuzuia watu ku-copy na ku-paste, pengine ningependelea kuweka tu tangazo kwamba ukiokota kitu hapa kwangu (picha au habari) basi hakikisha unatoa "krediti" kwamba umekitoa kwangu. Nafikiri ni bora tukaacha ujumbe na mawazo yetu katika vibaraza vyetu hivi ukawafikia watu wengi zaidi kwa kadri inavyowezekana - hata kama wana-kopi na ku-paste. Hii hata hivyo inategemea na malengo ya mwenye blogu.

Ni mawazo yangu tu haya mkuu na samahani kama nimekukwaza!

Naona hata kule kwenye blogu ya jamii imewekwa hii kitu. Tuliozoea kwenda huko ku-kopy na ku-paste tutakoma ingawa kama kweli mtu unataka kufanya hivyo ni rahisi tu.

Matiya unataka nami nikuonyeshe jinsi ya ku-copy na ku-paste kutoka kwenye blogu "iliyokatazwa" kama hii yako?

Matiya - kama ulikuwa unajibu hayo majigambo ya kidharau kwa junior bloggers ni safi sana. Ambacho hajui huyo aliyekuwa anadai hivyo ni kwamba wengi wetu hatuna muda wa kutosha na hatuna WAFADHILI wa kuhangaika na hizi blogu zetu. Mwambie anipe ufadhili wa Voda au TBL nimweke mtu wa kuishughulikia blogu hii kitaalamu aone itakavyokuwa. Na mambo mengi ya kublogu pengine wala hayahitaji utaalamu sana wa IT. Sasa nami nimebadili mawazo. Nitaijaribu hii nione kama itaonekana vizuri.

Jana usiku baada ya kusoma ujumbe wako huu nilienda "blogu ya jamii" na ilikuwa protected na yenye mwonekano tofauti. Hili lilinishangaza kidogo kwani blogu hiyo kimsingi ni matangazo na habari zo zote ambazo mimi sioni umuhimu sana wa kuzibinya. Na kweli sasa ni ruhusa kukopi tena na kupaste. Wataalamu wa IT hao (pengine ni kubadilisha template tu au "codi" hapa na pale!)

Profesa Mbele - kidogo inakwaza mtu anapokwapua makala ya uchambuzi na kuidondosha kwake kama ilivyo hata bila kusema kaitoa wapi. Kwa makala za uchambuzi kama hizi pengine ni muhimu kuzilinda na kuzitetea.

Hapa akimjibu KOERO:

malkiory said...

Masangu Matondo Nzuzullima said...

Koero. Wengi wetu hapa tunaongea kutokana na uzoefu wetu. Kwa sisi ambao tupo katika akademia, ni MARUFUKU kunakili hata sentensi moja tu ya mtu mwingine bila kusema ukweli kwamba sentensi hiyo si yako na kwamba umeitoa kwa mtu mwingine. Na hivi ndivyo dunia nzima inavyoendesha mambo yake.

Kama hivi ndivyo, mimi nadhani si vibaya hata sisi wanablogu tukajifunza tabia hii ya muhimu. Kama umekopi kazi ya mtu mwingine - hata kama ni "ujinga" -, basi onyesha ustaarabu japo kidogo na kusema ulikoupata huo ujinga kwa vile siyo wako. Ni tabia na mazoea ya muhimu sana ambayo yatakuja kutusaidia hata katika kazi zetu zingine.

Kwingineko naungana na Mtakatifu kuhusu kimya chako Bwana Matiya. Baridi imezidi nini mpaka umeshindwa kutaipu???? Rudi! Harakati huwa hazitaki likizo ati!