Tuesday, February 1, 2011

Wasipokuwa wao bila wewe, labda nawe si wewe bila wao.

MAISHA NI UTEGEMEZI. Ndio maana licha ya kuwa kuna wanaojiona kama "vichwa vya familia", bado wao si wao peke yao, bila hao wawaonao "mikia". Kwa maana nyingine, familia haiwi familia ikiwa na mtu mmoja. Ni lazima uwe na mwenzako / wenzako ambao uwepo wao na utayari wa kukuacha umiliki "u-kichwa" ndio ukufanyao uwe na "hadhi" uliyonayo.
Labda tuhame toka kwenye familia tuingine kwenye sanaa.
Kwenye fani hiyo (na hasa nchini mwangu Tanzania), ninawaona na kuwagawa wasanii katika makundi mawili. Wasanii HALISI wanaofanya kazi wakizingatia MISINGI YA KAZI na kisha kuna wale wanaojibidiisha kupata SIFA ambazo huwawezesha "kutumiwa" na kisha kujipatia sehemu ya mapato halali waliyostahili.
Wale wawekezao kwenye bidii na misingi ya kazi ni wengi japo hawafahamiki miongoni mwa wasiojua snaa halisi (ambao nao kwa bahati mbaya ni wengi zaidi na wamechukua majukumu ya kutambua, kutambilisha na kutunuku sanaa). Wasanii hao nawambia HERI KWAO kwani hawatachuja.
Kwa ndugu ambao sanaa kwao huambatana na SIFA, MATAMASHA, USHABIKI WA MITAANI nk, wanasahau kuwa licha ya kuwa wao ndio watajwao, bado ni kwa MSAADA wa wengine wanaoshiriki katika ufanikishaji wa sifa zao. Labda kwa ndugu wanaofahamu utayarishaji na urushaji wa vipindi vya Televisheni watatambua kuwa Anderson Cooper asingekuwa maarufu alivyo kama si mlolongo wa wafanyakazi wengi wanaofanya kazi kutwa-kuchwa "nyuma ya pazia" kufanikisha afanyalo. Na mara zote utasikia juhudi za kuwathamini na kuwaweka waandishi, wazalishaji, wapiga picha, waongoza kamera nk japo sisi hatuwaoni na kuwajua. Na hao ndio hasa wafanyakazi na yule asimamaye mbele ya kamera ni "kipaji" (talent) tu.
Kwa wanamuziki / wasanii wa nyumbani ni lazima watambue kuwa uongozi wa bendi, wana-bendi wengine nk ndio wawafanyao wao watambulike, waheshimike na hata "wapendwe" na kusemwa walivyo sasa. Lakini wengi wao husahau hilo na kuanza KUPIMA MASLAHI KWA KUTUMIA KELELE ZA MASHABIKI. Yaani kwao, wingi wa mashabiki (ambao kwa bahati mbaya hufuata upepo) ndio kiburi chao cha maslahi. Hutumia hilo kudai maslahi zaidi na / ama kutafuta maslahi zaidi kwingine. Tatizo ni KINACHOFUATA baada ya kuondoka toka kwa wale wanaokufanya uwe mashuhuri kwa namna ulivyo.
NISEME WAZI KUWA MARA NYINGI WASANII HAWA HUWA NA KIPAJI AMA UWEZO WA HALI YA JUU KATIKA JAMBO MOJA AMA MAWILI KATI YA MENGI YANAYOHITAJIKA ILI KUFANIKIWA KATIKA MUZIKI
Photo Credits: Bongocelebrity.com
-Labda ni "watunzi" wa nyimbo nyingi / zote katika albamu
-Labda ni "wapanga alaP wazuri katika nyimbo za bendi zao.
-Labda wana "sauti nzuri" zaidi ya wengine.
-Labda watoa ni "watoa maoni" yanayonogesha nyimbo nyingi n.k
Lakini la kutambua ni kuwa MAFANIKIO KATIKA MUZIKI NI ZAIDI YA HAYO na hata mengine mengi. Na ni mpaka wasanii watakapotambua kuwa kutunga, kupanga ala, sauti nzuri, nk. sio vitu pekee vinavyohitajika katika kufanikiwa ki-muziki, basi wataendelea "kupanda na kushuka" katika kile wakisakacho kwani kwa kutotambua watafutalo, wanajikuta wakijipoteza kwenye harakati za kujitafuta.
Na mifano halisi ni kama hii ifuatayo. Hebu sikiliza wimbo kama MASIMANGO wa TOT Plus ambao uliimbwa na kina Banzastone, Waziri Sonyo, Mhina Panduka, Abdul Misambano nk, na sasa jiulize hawa wasanii wako wapi sasa?

Pia hawa walishiriki katika wimbo mwingine hapa chini wa ELIMU YA MJINGA na zisikilize uone UMOJA wao ulivyokuwa muhimu kuwafanikisha na namna ambavyo UTENGANO wao UMEWAPOTEZA.

Ama labda sikiliza wimbo MTUMAI CHA NDUGU

na hata MAISHA KITENDAWILI

ambamo Mwinjuma Muumini, Badi Bakule, Amina Ngaluma na wengine wameshiriki. Hawa wote wameonesha ujuzi wa hali ya juu katika kuimba nyimbo hizi (kama timu), lakini tazama walipo kwa sasa.
LABDA WASANII WANGEJIFUNZA TOKA KWA KUNDI HILI LA KILIMANJARO BAND ama Wana Njenje
Ambalo takribani kila mmoja ana uwezo wa kufanya kazi kivyake na asilale njaa, lakini umoja wao umewafanya wawe na mafanikio na kujijengea heshima miongoni mwa washabiki duniani kote.
NAWAZA KWA SAUTI TUUUU!!!!

2 comments:

Unknown said...

Kilicho chema kinadumu.

Hata ukitie sumu, kamwe hakitaanguka na daima kitatukuka.

Rachel Siwa said...

kweli kaka leo umewaza kwa sauti nami nakuunga mkono!!!!!!!pia aksante kwa hizo nyimbo leo umenikumbusha mbali sana!!!!!!!!!!!!!!