Tuesday, February 15, 2011

Nguvu ndani mwetu...Yenye u-siri wa mafanikio yetu na wenzetu

Nimekuwa nikijaribu kuzifuatilia NGUVU ZILIZO NDANI MWETU ambazo zaweza kuwa CHANYA maishani mwetu na kwa nyakati tofauti nimeandika juu ya kile nilichotambua ama kutambulishwa ambacho ingetufaa sote. Na leo narejea kwenye mazungumzo ya kile ambacho tumeshakisoma kwenye mabaraza yetu mara kadhaa lakini nimekisikia tena kwa NGUVU ZAIDI. Nikukumbushe kilichowahi kusemwa
"Kwa washauri au counselors, watu kibao hulalamika juu ya ukosefu wa amani, upendo na utulivu. Swali la kwanza unaloweza kuwauliza hao walalamikiao wengine kuwa wanawanyima amani ni je, wewe uko katika amani na wewe mwenyewe? Au una amani binafsi?

Swali hili lina maana kuwa amani ya kweli imo ndani mwako na hakuna awezaye kukupa wala kukunyanganya amani hiyo japo wengi hatuna na tunaitafuta kwa wenzetu na kamwe hatutaipata Utulivu wa akili kwa kiingereza wanasema ni peace of mind ndio utuletea amani ya roho na nyinginezo.

Kwa njia ya tahajudi na meditation utapata amani."

Haya ni maneno ya mwaanzao katika MAKALA HII YA KAKA KAMALA ambayo ilieleza kwa kina saana kuhusu TAHAJUDI ama TAAMULI ambayo yeye aliomba tuiite MEDITATION. Kwa namna yoyote ile, alisisitiza kuwa "Ni lazima tuwe na utaratibu wa kukaa mahali patulivu na kujiambia maneno yenye furaha naya kututia amani." Nami June 12,2009 nilizungumzia umuhimu wa kile nilichokiita RIVERSIDE nikirejea wimbo wa Culture (hapa). Bado nikanasa pale kwenye faida ya kujipatia muda binafsi kujiakisi na kuangalia undani wa kile tunachodhani ni matatizo kwetu.
Na leo hii nimerejea kile nilichosikiliza katika kipindi cha Tell Me More cha NPR kinachoongozwa mtangazaji ninayemheshimu na kupenda sana kazi zake redioni Michel Martin na waweza kusikiliza na kusoma mahijiano hayo HAPA
Waweza angalia sehemu ya filamu iliyotengenezwa huko jela ambayo imeanza kuoneshwa jana hapa Marekani kwa kubofya hapa chini


Kilichonigusa na kunifurahisha ni namna ambavyo jela imetumia njia hii isiyo aghali na yenye kugharimu muda wa wafungwa (ambao wangeutumia vinginevyo) kuwafanya waitafute amani ya mioyoni mwao.
Niliwahi kuuliza Kwani kazi ya jela zetu ni ipi???? (Irejee hapa) na japo sijaweza kupata jibu, bado naamini kuwa JELA / VYUO VYA MAFUNZO vyetu nchini Tanzania vinahitaji MAPINDUZI MAKUBWA na kuwa sehemu za kubadili tabia na mienendo badala ya kuwa sehemu za kutesea na kurundika wahalifu na walioingia katika "anga" za "wahalifu safi" (wanaowabambikiza wenzao kesi zisizo za kweli).
Nililojifunza kutokana na kusikiliza kipindi hiki na kuwa tunaweza kubadili maisha ya watu waliotenda yale yasiyokubalika katika jamii kwa kuwafanya wajifikirie mara kadhaa na kuisaka kweli iliyo ndani mwao na iwafanyao wao kuwa wao na kisha kulinganisha walipo na ambapo wangetaka kuwepo ambayo itawafanya watambue pale walipojipoteza katika kutafuta walichodhani wangepata kwa njia iliyowafikisha gerezani.
Na nimesikia namna ambavyo Nguvu hii ya meditation ilivyo na nguvu ya kumfanya mtu kutambua kile ambacho hakuwa akikijua ama kukitambua ama kuwa wazi juu yacho na hivyo kumsaidia kuweza kufanikiwa na pia jamii kufanikiwa kwa mafanikio yake.
Na ndio maana naiona MEDITATION kama NGUVU NDANI MWETU.....YENYE U-SIRI WA MAFANIKIO YETU NA YA WENZETU.
Blessings

JICHO LA NDANI ni kipengele kinachozungumzia mambo mepesi na yaliyo ndani mwetu, ambayo yakiangaliwa vema na kwa tafsiri ama tafakari njema yanaweza ama ndio suluhisho kwa matatizo yetu. Kwa matoleo yaliyopita katika kipengele hiki, BOFYA HAPA

No comments: