Thursday, September 8, 2011

Labda sisi si maskini, bali.....

UMASKINI; ni neno nisilopenda kutumia kwa kuwa laonekana kutimiza matakwa ya wanaolisema ili kuendelea kutudharau na kutudhalilisha. Ninaona hivyo kwa kuwa tunakuwa maskini pale tusipokuwa na kile walichonacho, na wao wanakuwa wahitaji pale wanapokosa tulichonacho ambacho wanakihitaji. Kwa bahati mbaya hata viongozi wetu wanapokutana na hao ma-global sheriffs wanapandikizwa mbegu hizi za kujidhalilisha na kujidharau na bila kujua wanarejea nazo na kuendeleza propaganda za wakandamizaji hawa.
Kaka Msangi Jr aliuliza kwa Da Koero kuwa kwanini wafanyabiashara wa kizalendo wanaitwa wajasiriamali wakati watokao nje wanaitwa wawekezaji? Pia Kaka Matondo aliwahi kuuliza kuwa TUTATUKUZA VYA WENGINE NA KUDHARAU VYA KWETU MPAKA LINI? Na hata Kaka Kamala pia amekuwa akizungumzia saana tatizo la watu kutoitambua nguvu iliyo ndani mwao na kuendekeza kila kitokacho nje ya wewe na kudhani kitakupa amani utakayo.
Dunia sasa iko kikaangoni. Uchumi umeporomoka kila mahala na kila mwenye uwezo wa kumnyooshea mwenzake kidole anafanya hivyo. Wengi wanasema kuwa kuporomoka kwa uchumi duniani ni kutokana na kuanguka kwa uchumi wa Marekani. YAONEKANA KUKUBALIKA KWA WENGI lakini najiuliza hivi ni kiasi gani cha utendaji kazi kinahitajika ili kuifanya nchi kama Marekani isitetereke? Kwa sasa kiwango cha wasio na ajira kimepita 8% ambayo inaonekana kuiathiri saana nchi. Hapo ina maana kuwa zaidi ya 91% bado wana kazi na nchi inahaha kujaza nafasi za kazi. Nimesaka takwimu za Tanzania lakini hakuna nizipatapo japo hata nilizozipata zinaonesha kuwa hali ni mbaya zaidi. BOFYA HAPA KUZISOMA.
Ninafikiria kama na Tanzania ingekuwa na kiasi hiki kidogo cha ukosefu wa ajira tungekuwa wapi? Kwanini haya matatizo yasiwe funzo kwetu kuwa wenzetu tunaowaona wameendelea wanafanya kazi kuhakikisha wananchi wao wanakuwa na ajira na kiwango cha kazi kinakuwa kikubwa ambacho kitasababisha mzunguko mkubwa wa pesa na kuimarisha uchumi? Hebu fikiri kama namba za takwimu hizo zingegeuzwa na za Marekani zikawa za Tanzania na za Tanzania zikawa za Marekani, kungekalika? Unadhani nchi na ulimwengu ungekuwa kama vilivyo?
TATIZO
Ni kwamba viongozi (ama niseme watawala) i wabunifu. Wnatoa ahadi ambazo wanajua fika kuwa hazitimiliki.
Wananchi hawaonekani kuwa na subira na pia imani na mipango yoyote isiyotimilika ndani ya muda mfupi.
Viongozi hawaonekani kujali matatizo halisi ya wananchi na wawekezaji ambayo hayaonekani machoni pa wengi (kama mifumo ya maji na majitaka) ambayo ikiwa ya uhakika kunakuwa na mfumo bora zaidi wa maisha
Njaa na urho vinawagawa na kuwaathiri wananchi ambao husikiliza na kufuata kila waambiwacho na wale waliopewa "uchache" na wagombea.
TUJIULIZE....
Tuna rasilimali ngapi ambazo zikisimamiwa vema zinaweza kuwa MKOMBOZI kwa jamii?
Rasilimali hizo zina thamani gani na thamani hiyo ni sawa na sehemu gani ya hitaji la bajeti ya serikali kwa mwananchi?
Zinatumika vipi na kwa uwazi kiasi gani? Kama huna kichefuchefu cha haraka soma taarifa hii juu ya kiasi wanachovuna na kile wanacholipia kodi kwa kubofya hapa
Tujiulize kuwa viongozi wetu wamejitoa vipi kwa jamii wanazozitumikia?
Tujiulize kuna usawa na uwazi kiasi gani katika kuyashughulikia matatizo na mikataba ya nchi yetu kwa manufaa ya wananchi walipo sehemu husika?
TUNA RASILIMALI NYINGI AMBAZO ZIKIPANGWA NA KUSIMAMIWA SAWASAWA, TUTAWEZA KUWA MBALI ZAIDI YA HAPA TULIPO.
Nikitazama yote najikuta nikiamini kuwa labda sisi si maskini, bali "tunamaskinishwa" na wenye umaskini wa fikra.

Kutoka Maktaba. Bandiko hili lilitoka kwa mara ya kwanza April 9, 2009

No comments: