Sunday, September 11, 2011

Tanzania Yangu...Isiyojua kuziba ufa wala kujenga ukuta (II)

Lucky Dube aliwahi kuimba akisema "don't you think it is time to be a little bit more responsible? Too many people dies these days, if you read the paper, check out the news, the numbers are there. But EVERY NUMBER REPRESENT A HUMAN BEING WHO WAS A MOTHER, A FATHER, A SON OR A DAUGHTER OF THIS LAND." Meli ya Mv Spice Islander iliyozama alfajiri ya Sept 10, 2011 na kuua mamia ya watu. Zaidi ya watu 600 waliokolewa
Mwanzoni mwa mwaka 2009 (siku 11 za mwanzo) tulishuhudia ajali mbili zilizoua watu wengi. Nami nikaandika HAPA kuwa TUMECHOSHWA NA SALAAM ZA RAMBIRAMBI. NA SASA HATUZITAKI. Lengo kuu la kuandika hayo ilikuwa ni kuonyesha namna tulivyochoshwa na UNAFIKI wa watawala kuongea bila kutekeleza. Na katika post hiyo nikasema
"Serikali inastahili kufanya zaidi ya kutuma salamu za rambirambi. Kwenye salamu zake za wiki hii, Rais Kikwete "ameunguruma" akisema "hatuwezi kuvumilia kutokea kwa ajali hizi wakati mamlaka zenye dhamana ya kusimamia sheria za usalama barabarani zipo. Tufanye jitihada zote zilizo ndani ya uwezo wetu kupunguza kwa kiwangi kikubwa na ikiwezekana kukomesha kabisa ajali hizi za barabarani ambazo zimeshapoteza maisha ya wenzetu wengi"
MTAZAMO WANGU: Tatizo si kusema bali ni kutekeleza. Hawa wanaotangazwa kuwa wamepona na wameruhusiwa haimaanishi kuwa hawako kwenye maumivu tena makali. Binafsi nimekuwa kwenye maumivu ya ajali kwa miaka 9 sasa, hivyo natambua kuwa mtu kutoka akiwa anatembea ama bila mchubuko haimaanishi kuwa ataweza kuendelea na maisha yake kama zamani. Ni lazima hizi bima zihusishwe, ukaguzi wa magari uwe wa makini, ukaguzi wa waendesha vyombo uwe wa kweli na RUSHWA isiweke pembeni thamani ya roho za watu.
Naamini Rais anajua UOZO uliopo kwenye kitengo anachokizungumzia na ataweza kuwekeza katika kuokoa maisha ya nguvukazi inayopotea.
Naamini sasa ni wakati wa kutenda maana TUMECHOSHWA NA SALAMU ZA RAMBIRAMBI, NA SASA HATUZITAKI KWA KUWA TWATAKA KUTOKOMEZWA KWA AJALI HIZO" (Kumbuka, hii ilikuwa ni Januari 2009)
Hiyo ilikuwa ni mwaka 2009. Miaka 2 na miezi 8 baadae, bado tunaendelea na kilio kilekile.
Niliwahi kuandika kuwa NI WAKATI WA RAIS KUWAJIBIKA KWA TIMU YAKE KUTOWAJIBIKA, NA YEYE KUTOWAWAJIBISHA. Bado naamini katika hili. Leo hii tunasoma habari za ajali mbaya ya meli. NANI ATAWAJIBIKA?
Na asipowajibika utamuwajibisha? Na usipomuwajibisha utawajibika? SISUBIRI SALAAM ZA RAMBIRAMBI. NASUBIRI UWAJIBIKAJI NA UWAJIBISHWAJI.
Mwezi Julai mwaka huohuo 2009, niliandika kuhusu hotuba ya Waziri Mkuu nikisema Mheshimiwa!!!!!! Hizi si takwimu tu, ni maisha ya watu kuhusu KAULI ZAKE ZA "TUNALIFANYIA KAZI". Bado nikiwa na "pointi" ileile kuwa TUMECHOSHWA NA KAULI na tungependa kuona mambo yakitendeka tena katika KUKINGA NA SI KUKARABATI. Katika nukuu niliyoanza nayo hapo juu, Lucky Dube amezungumzia THAMANI YA MTU na si kuweka msisitizo kwenye IDADI ya waliokufa ama kuokolewa. Amesema kila mtu ni Baba, Mama, Mwana ama Binti. Na kama WATAWALA wetu wataweka thamani hizi mbele, basi wataliangalia tatizo hili kwa jicho la ndani.
Nimeshaona ZIARA za wanasiasa wengi (pengine kuliko ilivyowahi kutokea kabla) ambao wamekwenda kutoa pole. Pengine mnapoangalia wahanga mnapaswa kujiuliza kama msingeweza kufanya lolote kuzuia ajali hiyo. Siku za karibuni, Ndugu yetu Dennis Matanda aliuliza kwenye mtandao wa Wanabidii kuwa kwanini wanasubiri ajali ndio watoe maamuzi? Akatoa mfano akisema:
1. Wamesimamisha leseni ya Champion buses kati ya Dar - Mwanza baada ya kupata ajali na kuua watu kadhaa mkoani Dodoma.
2. Wamesimamisha leseni ya (wa ukaya) Moro Best kati ya dar to Ifakara baada ya kupata ajali Ruvu ranchi.
3. Wamesimamisha leseni ya Mohamed Classic baada ya kupata ajali somewhere Arusha wakati basi likiwa linakuja Kahama.
4. Wanachunguza mabasi ya Simba mtoto baada ya nalo kupata ajali na kuua likitokea Tanga kwenda Dar
Sasa kwenye usafiri wa maji nako ni yaleyale. Mwaka jana meli ya Mv Fatahi ilizama. Pia kulikuwa na matukio mengine ya kuzama kwa meli nchini mwetu. Suala ni kuwa TUNAJIFUNZA NINI KUTOKANA NA HAYA? Kuna atakayesimama na kusema TUMEFANYA HILI NA LILE KUZUIA AJALI? Ni kweli kuwa UBORA WA VYOMBO VYA USAFIRI UNAZINGATIWA? Meli hii ilipata tatizo wakati inaletwa Zanzibar, Je! Kuna mamlaka yoyote iliyofuatilia kuhakikisha tatizo limetatuliwa?
Kuna maswali kadhaa ninayojiuliza kutokana na ajali hii.....
1: Kama hatuna vifaa vya uokozi, kwanini tusihakikishe vyombo vya usafirishaji viko katika hali stahili?
2: Kama hatuna vifaa vya uokozi, kwanini tusihakikishe kuwa vyombo vya usafiri havizidishi idadi ya abiria?
3: Kama hatuna vifaa vya uokozi, kwanini hatuhakikishi kuwa safari za boti zinafanyika mchana ili hata "wasamaria wema" wajitokeze wakati wa maafa kama haya?
3: Kama hatuna vifaa vya uokozi, kwanini tunaendelea kutumia vyombo hivi vya usafiri ambavyo tunajua hatari zake?
Kutojua namna ya kuzuia ajali ama kupunguza ukubwa wa madhara ndiko kuziba ufa, na kushughulikia tukio pale mambo yanapokwenda mrama ndiko kujenga ukuta. Na nchi yangu hainyeshi kufanya vema katika yote haya. Na ndio maana naisikitia Tanzania yangu....Isiyojua kuziba ufa wala kujenga ukuta.


Tanzania Yangu ni kipengele kinachozungumzia ytale yaendeleayo nchini Tanzania na namna ambavyo "ndivyo sivyo" inavyozidi kupamba moto nchini. Kwa matoleo yaliyotangulia BOFYA HAPA

Tuonane "Next Ijayo"

No comments: