Wednesday, February 8, 2012

Tanzania ni nini na mTanzania ni nani?

Nakumbuka nilipokuwa ninamsoma Da'Yasinta na uTANZANIA wake anaojivunia (msome hapa) . Nikafurahia saana. Katika maoni kama kawaida nikamsoma Kaka Kamala aliyeleta CHANGAMOTO nyingine akiuliza "tanzania nini na mtanzania ni nani?" na hilo likanifanya nirejeshe mawazo kwa wale ambao wanajua wanatokea Afrika lakini hawana hakika na watokeako. Hivi wana pa kupenda ama wataipenda Afrika kwa ujumla wake? Lakini kuna mengi ndani ya Afrika ya kumfanya mtu asiyelazimika kuipenda aipende? Vita, Ubadhirifu, Ufisadi ama? Tarehe 7 Aprili 2009 nilikumbuka saana nyumbani kisha nikaandika kuhusu siku nitakayorejea nyumbani (Bofya hapa kuisoma post hiyo). Nilijiuliza kuhusu nyumbani kisha "nikasindikiza" toleo hilo na wimbo wake Luciano uitwao When Will I Be Home (Bofya hapa kuusikiliza) ambao pia (kwa mshangao wangu nilipousikia mara ya kwanza) unaitaja TANZANIA kama nchi anayojiuliza kama ndiko iliko asili yake ama la.
Nakumbuka mwanzo wa miaka ya 2000, Kaka-Rafiki Gotta Irie aliniandikia mail kunieleza kuwa alikuwa na mpango wa kumualika Luciano kwenda kufanya onesho nyumbani. Nilifurahi kusikia hivyo kwa kuwa mimi ni msikilizaji na mpenzi wa muziki wa Luciano, na aliporejea toka huko (katika onesho ambalo niliambiwa kuwa lilifana licha ya mahudhurio kuingiliana na matukio ya kidini), lakini hata aliporejea toka huko, Luciano ameendelea kuizungumzia Tanzania na anasema katika kukaa nchini na kutembea alijifunza mengi na kisha akaandika wimbo wa Remember When ambao kama aelezavyo kwenye mahojiano haya yajayo, alipata wazo hili akiwa Tanzania. Nikajiuliza MAPENZI aliyonayo kwa nchi ambayo inazidi kumong'onywa na wabadhirifu na namna anavyojitahidi kuielimisha jamii juu ya uzuri wa Tanzania nikaguswa saaaana. Luciano ni msanii nimpendaye (wacha nikiri) na haipiti siku bila kumsikia.
Yeye yuko nje ya nchi na nje ya bara la Afrika lakini amekuwa akijihesabu (kama walivyo wengi) kuwa ni mwAfrika. Na mara kadhaa ameunganisha hisia zake na Tanzania. Lakini hiyo yamfanya kuwa mTanzania? Hivi hawa wafadhili waliowekeza sehemu kubwa ya rasilimali zao nchini Tanzania kwa manufaa ya watu wasio na uwezo mkubwa / wahitaji tunaweza kuwaita waTanzania licha ya kwamba hawakuzaliwa na pengine hawana uraia wa Tanzania?
Vipi juu ya wale waliozaliwa nje ya nchi na wazazi wenye asili ya Tanzania na ambao wanaendelea kushiriki katika mapambano ya kuikomboa nchi, tunaweza kuwaita waTanzania?
Kwani Tanzania ni nini hasa? Na je! MTanzania ni yupi? Na uTanzania ni nini?
Yule mzawa na mwenye uraia wa nchi anayeinyonya nchi kila uchao, ama yule mwenye mapenzi na nchi na kujaribu kila awezavyo kuona inaenda muelekeo ulio mwema?
Kama walivyoimba Morgan Heritage kwenye wimbo wao Nothing To Smile About (japo wao walizungumzia zaidi hali ya Jamaica ambayo kwa namna moja ama nyingine yafanana na kwetu), tunasikia jinsi watu wanavyoisifia Tanzania kutokana na takwimu mbalimbali. Kwa Amani, Upendo na "mafanikio ya kuinua maisha ya mtu wa chini" japo kwa wale walio nchini wanaona namna mabadiliko yamaanishavyo kuzidi kusubiri bila mafanikio.
Ni jambo la kusikitisha sana kama unakutana na mtu anayekusimulia mafanikio haya tena kwa furaha kuu huku sisi tutokao vijijini tukijua hali halisi waishio ndugu zetu ambao tumewatembelea muda si mrefu uliopita. Simaanishi kuwa hakuna maendeleo lakini sidhani hata kama viongozi wetu wanatambua hali halisi wanayokabiliana nayo wakazi wa vijijini ambako hasa ndiko uliko UTI WA MGONGO WA UCHUMI WETU.
Lakini si vijijini tu, hata baadhi ya sehemu za mijini na kwenye maJiji kama Dar na Mwanza ni ya kusikitisha.
TANZANIA NI NINI, NI YA NANI NA MTANZANIA NI YUPI?
Wacha nirejee kwa "mTanzania wa hiari" Luciano kwenye mahojiano haya ambapo anaeleza kuhusu Tanzania. Msikilize hapa katika mahojiano (ANZA DAKIKA YA 2 NA SEKUNDE 31) umsikie hisia zake kuhusu Tanzania na Africa kwa ujumla
.
Na hii hapa chini ndio video ya wimbo wake huo ambao ni kati ya nyimbo bora saana na zilizotulia na kufikirisha kuhusu asili ya watu weusi ambayo wengi wao wanajitahidi kuitafuta.
Itazame
Blessings

1 comment:

Yasinta Ngonyani said...

Kwanza nasema ahsante kwa mada hii. Ni kweli mimi pamoja na kusema Afrika kuna umaskini lakini kuna raha zake. Tanzania ni nchi na Mtanzania kwa mimi ni yule aliyezaliwa Tanzania. Lakini pia kama ulivyouliza Je kwa waTanzania waishio nje na huko wamepata watoto au mTanzania ambaye kaolewa/kaoa mtu ambaye si mTanzania hapo inakuwaje? hapa nami ningependa kujua.