Tuesday, May 14, 2013

 Chonde Chonde Mhe. Makalla...Kabla hujawaketisha Ruge na Jay Dee

Photo Credits: Vijimambo Blog
 Moja kati ya habari ambazo zimesambaa wiki iliyopita, ni HII ya Naibu Waziri wa Habari Michezo Vijana na Utamaduni Amos Makalaambaye amenukuliwa "kutangaza hadharani kulivalia njuga suala la mzozo kati ya Mkurugenzi wa wa Kampuni ya Clouds Media Group Ruge Mutahaba na msanii nyota wa kike wa Bongo Fleva Judith ‘Wambura Lady Jaydee"
  Hili ni JAMBO JEMA na la kupongezwa kwa kuwa hakuna ambaye anapenda kuona MZOZO HUU ambao kwa hakika wengi wanauona USIO WA MAANA KWA JAMII YETU ukiendelea kutawala vyombo vya habari na kuweka kando masuala muhimu ambayo yangeweza kuanzisha mijadala chanya kwenye jamii yetu.
Lakini...
Pamoja na PONGEZI zangu katika kuondoa hili, napenda kuleta OMBI / TAHADHARI kwa Naibu Waziri kuhakikisha kuwa ANATATUA CHANZO CHA TATIZO HILI PAMOJA NA YALE YAFANANAYO NA HILI badala ya kujikita kwa RUGE na LADY JAY DEE.
Ninalomaanisha ni kuwa aangalie kinachosababisha watu wamuunge mkono Lady Jay Dee na wengine wamuunge mkono Ruge japo wote wanapingana na ni katika KAZI MOJA (muziki)
CHONDE CHONDE Mhe Makalla, kabla hujakutana na WAPENDWA HAWA (wachukianao), naomba ufanye uchunguzi kujua kile ambacho kiko nyuma ya kinachosikika na kusomeka kwenye mitandao.
Kwa yeyote mwenye akili timamu, atatambua kuwa KINACHOLALAMIKIWA NI ZAIDI YA KINACHOSEMWA.
Kumekua na matatizo katika fani nzima ya muziki nchini Tanzania. Na sehemu ya matatizo haya inatokana na serikali yetu.
Oktoba 12, 2008 niliandika hapa kuhusu Wasanii kama "chombo cha starehe" cha serikali na kati ya niliyoeleza ni kuwa
"Pengine kubwa na lenye kuonesha "kuthamini burudani" ya wasanii wa nyumbani ni pale wanapoalikwa kwenda kuwatumbuiza waheshimiwa wabunge ambao kwa miaka nenda rudi wameshindwa kuweka sheria ambazo zingelinda haki na mapato yao.
Najua Waheshimiwa wabunge na wenye mamlaka wana-enjoy saana sanaa ioneshwayo na wasanii wetu, lakini kama wanaishia kuwalipa pesa ya onesho (kama hayo ya bungeni) ama kuwapigia makofi na pesa ya onesho la airport, ama kama ni suala la mkataba wa kupiga kampeni na ama propaganda za wasanii, basi napenda watambue kuwa "kwa mujibu wa tafsiri niliyopewa na mwalimu wangu ninayemuamini, nao wanawatumia wasanii kama chombo cha starehe".
Hivi si wakati wa kuweka sheria kali kwa wale wanaosambaza kazi za wasanii? Si wakati wa kupitia vyema hakimiliki na unyonyaji ufanywao kwa wasanii na watu wachache kujinufaisha kwa jasho la wasanii? Ni kweli kuwa viongozi serikalini hawayaoni haya ama hayana "sound" ya kisiasa? Nachukia kila ninapoona "politrix" inaingilia uhalisia wa maisha na kuweka pembeni suluhisho linaloweza kumnyanyua msanii, familia na taifa kwa ujumla.
Lakini pia lawama hizi ama haya yote yatokeayo yana mkono wa wasanii wenyewe. Kutokuwa na umoja miongoni mwao, kuendekeza njaa na majungu baina ya baadhi yao na kutokuwa na elimu na utawala wa KAZI YA SANAA kunawafanya wagawanywe na kutumika bila wao kujijua. Kutokuwa na hesabu kamili na halisi za namna ya kugharimisha muda na kazi zao kulingana na hali ya maisha ya sasa ukizingatia kuwa ndio kazi yao wategemeayo kwa maisha ya sasa na uwekezaji wa maisha yajayo...."

 Na ukweli wa hili la UMOJA na KUENDEKEZA NJAA linadhihirika zaidi sasa ambapo katika MGAWANYIKO uliopo sasa, hakuna wanaojitokeza wazi kuunga ama kupinga kinachosemwa na yeyote kati ya Ruge na JayDee.
UKWELI NI KUWA.....

Kati ya hawa washutumianao (hasa katika hili la kazi za muziki), mmoja kati yao alistahili kuwa "MKWELI KWA KILA MSANII" ambaye (kulingana na msimamo na mahusiano yake kikazi) anauona UKWELI toka upande wake wa maisha.
Lakini mpaka sasa tumesikia WACHACHE sana wakizungumzia hili, kama vile lizungumzwalo haliathiri kazi na / ama fani yao.
Ina maana TATIZO LAWEZA KUWA KWANINI HAWAJASEMA NA WAKISEMA NI NINI KITAWAKUTA?
CHONDE CHONDE Mhe MAKALLA.....KABLA HUJAWAKETISHA RUGE NA JAY DEE, tafuta sababu za ukimya uliopo sasa juu ya hili linaloathiri maisha ya wasanii wengi.
Kama ni kweli kuwa asemalo Lady Jay Dee ni "uzushi", basi tuangalie namna ambavyo wasanii wanaweza kutambua wajibu wao katika jamii na kisha kuwajibishwa kwa kusema kisicho sahihi.
Kama ni kweli kuwa asemalo Ruge ni "uzushi", basi tuangalie namna ambavyo vyombo binafsi vya habari ambavyo pia ni wadau wakuu wa ajira za wasanii vinaweza kuwajibishwa pale vinapotenda yasiyo haki kwenye kazi za wasanii.

Na huu ni MTAZAMO wangu kwa namna ninavyoona tatizo.
Labda....namna nionavyo tatizo ndio tatizo

No comments: