Tuesday, July 23, 2013

Nguvu baina yetu isiyo na nguvu ndani mwetu, yenye nguvu kwetu.

Ndio.
Ni nguvu ambayo twaweza kuitumia japo huwezi kuipima kwa namna tupimavyo nguvu nyingine, lakini inaweza kufanya mengi na kutuepusha na yale ambayo hata kwa nguvu tulizonazo hatuwezi kuyatenda kwa urahisi namna hiyo.
Nazungumzia NGUVU YA KUKUBALI KUELEWA TUAMBIWACHO. Wengine wanaita kusikia lakini kuna kusikia na usielewe kama ilivyo kwa aangaliaye na asione.
Pengine tukiangalia mataifa makubwa yanavyohangaika kupambana na wasiowaona, unadhani wangeweza kukaa chini na kuelewa kile wanachoonywa kabla hawajaingiza miguu huko vitani wangeingia gharama za mali na uhai wa watu kama waingiavyo sasa?
Ama kama "watawala" (na hapa sijasema viongozi maana najua viongozi sasa ni wachache na hawatendi haya) wangesikia kilio cha wananchi na kujitahidi kukamilisha kinacholiliwa badala ya kutumia hilo kuwachuma kwa kuomba rushwa tungekuwa katika hali tuliyopo sasa?
Ama watu wangeelewa wanavyoambiwa juu ya usawa uliopo kati ya watu wa rangi tofauti za ngozi wangeendekeza na kuendelea ubaguzi na matabaka? Na unadhani tungelia tuliavyo kwa kuwa tu ndugu zetu ma-albino wanauawa?
Ama kama kilio chetu kingeweza kufika huko "siasani" unadhani ufisadi ungeendelea kuwa namna ulivyo?
Tukitazama nguvu ya kutoelewa waambiwacho inavyoigharimu jamii, utaona kuwa kuna nguvu kubwa sana ya usikivu na uelewa ambayo inastahili kuheshimiwa japo haina kipimo kama upimavyo nguvu ya "kubeba chuma", lakini ambayo ikitumiwa vema inaweza kuepusha matumizi yasiyo ya lazima ya nguvu zetu na kuepusha usumbufu na hata upoteaji wa maisha ya watu.
 
Tuonane "next Ijayo"
JICHO LA NDANI ni kipengele kinachozungumzia mambo mepesi na yaliyo ndani mwetu, ambayo yakiangaliwa vema na kwa tafsiri ama tafakari njema yanaweza ama ndio suluhisho kwa matatizo yetu. Kwa matoleo yaliyopita katika kipengele hiki, BOFYA HAPA

No comments: