Tulipokuwa skuli tulifundishwa kuwa, ili tuendelee tunahitaji mambo manne: Ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora. Jumuiya ya Wazanibari Waishio nchini Marekani (ZADIA) inauelewa fika umuhimu wa maneno hayo ya hekima, na ndio maana uongozi wake bora, kwa kutambua jukumu lake, daima umekuwa mbioni katika kutafuta na kubuni mbinu za kusaidia maendeleo nyumbani Zanzibar.
Kwa vile kuwa na watu tu haitoshi kuleta maendeleo ya nchi, ndio maana ZADIA imelipa kipaumbele swala la afya na ustawi wa jamii, kwani bila kuwa na watu wenye afya bora hatuwezi kufikia maendeo.
Kwa mantiki hiyo, kama ilivyoelezwa siku zilizopita, uongozi wa ZADIA ulifanya mawasiliano na Shirika la Pure Ultrasound la nchini Marekani na kufikia makubaliano ya kimsingi ya kuwapatia wataalamu wa Zaznzibar vifaa vya Ultrasound na mafunzo ya kuvitumia vifaa hivyo.
Na kama inavyokumbukwa, ujumbe wa shirika hilo tayari umeshatembelea Zanzibar katika hatua za awali za kuangalia ni jinsi gani wanaweza kuisadia Zanzibar katika uwanja huo.
Katika kufuatilia hatua za utekelezaji wa makubaliano hayo, Mwenyekiti wa ZADIA Bwana Omar Haji Ali, kwa mara nyengine alikutana na uongozi wa Pure Ultrasound mnamo tarehe 18 Mei, 2015.
Katika mkutano huo, pande hizo mbili zilikubaliana kuwa Pure Ultrasound itatuma mtaalamu wake wa ngazi za juu Visiwani Zanzibar mara tu baada ya kumalizika kwa mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Mtalaamu huyo atakaa Zanzibar kwa kipindi kisichopungua mwezi mmoja kwa ajili ya kufanya utafiti wa kimkakati kuhusu mahitaji ya vifaa vya tiba katika hospitali za Zanzibar, pamoja na mafunzo yanayohitajika kwa wataalamu wetu katika fani hiyo.
Upande wa Pure Ultrasound, unaomba kama ikiwezekana, wakati mtaalamu wao atakapokuwa Zanzibar akutane na uongozi wa ngazi za juu wa Wizara ya Afya, kuanzia Waziri, Naibu wake na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya. Aidha, wanaomba kukutana na Mkuu wa Kitengo Cha Huduma Za Dharura (Director of Emergency), wakuu wa Hospitali zote, watunga sera za afya pamoja na Wakuu wa vitengo vya Upasuaji (Surgery)
Baada ya tarehe ya kuwasili mtaalamu huyo nyumbali Zanzibar kupangwa, ZADIA itawasiliana na Wizara husika kwa ajili ya maandalizi ya lazima kwa ujumbe huo.
MAPENDEKEZO
ZADIA inatambua kuwa mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Kutokana na hali hiyo, ilipendekeza ujumbe wa Pure Ultrasound ufike Zanzibar kabla ya kipindi cha kampeni rasmi za uchaguzi kuanza, na kwamba wataalamu watakaoleta vifaa na na kutoa mafunzo ya jinsi ya kuvitumia wafike baada ya uchaguzi kumalizika. Kwa hali hiyo, tunaomba Maofisa waliotajwa katika taarifa hii, wapangiwe, au wajipangie ratiba zao ili zitoe nafasi ya kukutana na mtaalamu huyo.
ZADIA inapiga mbwiru tu, goma kubwa liko mikononi mwa Uongozi Bora wa Wizara husika. Hivyo, basi, ni vyema kuitumia nafasi hii ikiwezekana kuwepo na mapatano ya mpango huu kuendelezwa kila baada ya kipindi fulani.
Aidha, tuzithanmini juhudi na mchango wao. Kwani katika mkutano na Ndugu Omar, walitoa maelezo ambayo kana kwamba yanaonesha kuwa walidharauliwa, kwa vile mjumbe wao aliyekuja mara ya mwanzo hakupata nafasi ya kukutana na Waziri wa Afya.
Wahenga walisema: "Abebwaye hujikaza". Kwa hivyo, ZADIA inapendekaza kuwa, ili kuwahamasisha wahisani hao, Serikali ya Zanzibar ichangie japo kidogo katika gharama za mtaalamu huyo wakati atakapokuwa akiendeleza utafiti wake, kama vile malazi na chakula.
SHUKURANI
Pure Ultrasound imeelezea shukrani zakeza dhati kwa ukarimu ulioonneshwa na watu wa Zanzibar wakati wa ziara ya mjumbe wake Bi Trisha mwezi April mwaka huu. Halkadhalika mjumbe huyo alitoa shukrani na pongezi maalum kwa Dakta Omar Ali Juma kutokana na umahiri aliouonesha katika taaluma yake. Hivyo basi, Pure Ultrasound itafurahi sana iwapo Dk Omar atakuwa na mtaalamu wao Bi Abiola wakati wa ziara yake Visiwani Zanzibar. Tusisahau kumtayarishia zawadi ya kanga, kwani Bi Trisha zilimvutia sana.
Tupo pamoja kwa ajili ya maendeleo ya Zanzibar.
No comments:
Post a Comment