Monday, August 10, 2015

MAISHA ya sasa. Ni kukimbiza DEATHDAY kuliko kuikimbia BIRTHDAY

Na Mubelwa T Bandio
MAISHA. Nimejifunza kuwa hayako sawa. Na naamini huo ndio usawa wake, kwani humu tuishimo hakuko sawa. Hivyo, haitakuwa sawa kwa maisha kuwa sawa katika "uwanja" usio sawa kwa waishimo.
Na...
Najua nililoanza nalo na nitakaloendeleza halitaeleweka sawa, na huo ni udhihirisho wa usawa wetu, ambao nao hauko sawa.
Leo, Agosti 10,  ninapoadhimisha mwaka mwingine katika maisha yangu, naitumia siku hii KUAKISI maisha yangu kuliko kusherehekea.
UKWELI ni huu...
Unasoma hapa kwa kuwa "umekua" na kufikia umri wa kusoma na kuelewa. Huu ni umri wa kusherehekea ama kuadhimisha siku kadhaa za kuzaliwa kwako.
Na, kama unasoma hapa, jambo moja ninaloweza kukuhakikishia ni kuwa UTAKUFA.
Kwa hiyo, kama wanadamu, haya mawili yanakuwa ya lazima. Ukizaliwa, utakufa. Tofauti ya maisha yetu ipo katikati ya haya mawili.
Kama nilivyowahi kuandika, kuwa UTAKUMBUKWA KWA DESHI YA MAISHA YAKO (rejea hapa)
Maishani, nimehudhuria BIRTHDAY(s) na MISIBA mingi tu, na kote nimejifunza mengi kuhusu maisha yetu ya sasa, tuyatakayo na namna tunavyojitahidi kuifikia TAMATI yetu.
Labda funzo kuu nililowahi kushiriki nanyi ni lile nililoliandika HAPA Agosti 22, 2011 baada ya kuhudhuria msiba wa Dada yetu hapa Washington DC.
Maisha yetu ya sasa yanaonekana kuwa ya mchakamchaka, twayakimbiza matumaini na (katika hali ya kushangaza) hata siku zaonekana kuwa fupi kuliko awali.
Kabla hujajipanga, ni kesho, ni juma lijalo, ni mwezi ujao na mwaka bila kukamilisha mengi uliyoamini ungependa kuyakamilisha katika muda uliojipangia.
Ninapoangalia miaka hii niliyoishi, naiona kuwa mingi sana. Si kwa kuwa nimeishi mingi kuzidi wote, bali kwa kuzingatia ni mara ngapi nimekuwa nikiamini nimefika mwisho wa uhai.
Nakumbuka kusoma makala ya Kaka Eric Shigongo, iliyosema kuuona mwaka mpya ni nafasi ya ziada. Na naamini katika hilo.
Mara kadhaa (na ni zaidi ya moja) nimekuwa kwenye nafasi ya kuona kama kesho ilikuwa mbali na isiyofikika kwangu nikiwa hai. Siku ambayo hunijia akilini zaidi juu ya hilo, ni HII
Lakini leo wasoma niandikalo.
NI NAFASI YA ZIADA katika kuikimbiza "siku ya mwisho"
Nikirejea kwenye kichwa cha bandiko hili,fikra kwamba maisha yetu ya sasa ni kama kuikimbiza kesho kuliko kuifikiria leo na hata jana, kunatufanya tuonekane kuyawaza yajayo kuliko tulikotoka.
Ni hili linalonifanya niamini kuwa, maisha yetu ya sasa yamewekeza katika yajayo. Na kama nilivyoeleza kabla, jambo pekee ambalo sote tuna hakika nalo, ni kifo.
Na ndio maana nikasema, MAISHA ya sasa. Ni kukimbiza DEATHDAY kuliko kuikimbia BIRTHDAY
Anyway!
Nisijesahau kujitakia EARTHday njema.
Japo najua fika kuwa shukrani za maisha yangu nazipokea kwa sababu ni Mungu aliyeniweka hai mpaka sasa. Na ndiye aliyenipa WAZAZI wangu ambao sina ninanloweza kueleza kuhusu nafasi yao maishani ikalingana na walilotenda.
Labda jambo moja tu, kwamba walinibariki na NDUGU ambao uwepo wao umekuwa kama egemeo la kukua kwangu. Hawa ndugu wameniwezesha kuambatana na JAMAA ambao kwa muongozo wa ndugu, wameniwezesha kuwa nilivyo. Si unakumbuka kuwa Twachagua maongezi, maongezi yachagua mawazo na mawazo yatuchagulia jamii? (Isome hapa)
Nina maRAFIKI ambao wananisaidia katika kukua kwangu. Hawa nawajumusha na wale wanajiona kama maadui kwangu, ambao mara nyingi wamenifanya kujitahidi kukamilisha mambo ili wasipate la kusema.
Hahahahahaaaaaaaaaaaaaaaa
Kipekee, namshukuru mke wangu mpenzi Esther na wanangu Paulina na Annalisa kwa kuwa wavumilivu kwenye harakati zangu (nyingine hazielewekagi yaani)
Hahahaaaaaaaaaaaaaa
Ni siku nyingine ya kukumbuka kuzaliwa kwangu. Nalikaribia hitimisho la maisha, na nikilijongelea, najitahidi kukamilisha dhumuni yangu ya kuwa humu duniani.
Mungu akubariki na kuonyeshe namna muafaka ya kutenda kila lililo jema, kadhi uikaribiavyo.
 

2 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Hongera sana kwa siku hii ya kuzaliwa. Mwenyezi Mungu akupe afya uishi miaka mingi na uwaone wajukuu na vitukuu. Na akupe mafanikio mema kwa yale ufanyayo.....dadako Kapulya!

Yasinta Ngonyani said...
This comment has been removed by the author.