Saturday, December 27, 2008

Ni kama hadithi ya KUKU na YAI

Nani angetakiwa kuwa wa kwanza kutoa uelekezi wa hapa? Mjenzi ama mipango miji? Picha mali ya Kaka Issa Michuzi
Unapofika wakati ukaanza kuwaza namna ambavyo unaweza kubadili jamii fulani kuelekea kule ambako unaamini ndiko inakotakiwa kuwa, unaweza kujikuta ukikwama unapokosa jibu la wapi pa kuanzia kurekebisha. Ni kama ukijiuliza matatizo tuliyonayo nyumbani (Tanzania) kama ni ya kuilaumu Serikali ama wananchi. Najisikia kumwaga lawama pande zote maana kila upande una UOZO wake unaoendekezwa na ambao unategemea kwingine kuanze kubadilika kabla hakujafanya hivyo. Ni kama kujiuliza ni nini kilianza kati ya kuku na yai.
Yaani suala la rushwa linalotumung'unya "vibaya-mbaya" laweza kuwa mfano tosha wa nini cha kuanza kurekebisha na nani wa kuanza kurekebisha. Sijui wa kumkamata ni aombaye ama apokeaye na ni nani mwenye shida zaidi kati ya aombaye na apokeaye rushwa. Wapo wasemao kuwa tatizo ni mshahara na maisha duni (hasa kwa polisi) lakini ni kweli kuwa wakiongezewa mshahara wataacha kuomba rushwa? (hivi ni nani alisharidhika na pesa?). Ama tukiangalia "juhudi" za serikali kusambaza umeme nchini zinazorota lakini pia ndani ya uzorotaji huo kunakuwa na "waheshimiwa" ambao wanaendelea kuiba nyaya hizo "chache" zilizopo. Sina hakika kama huo uhujumu ni njia ya kuwakilisha ujumbe kuwa wamechoshwa na longolongo za serikali ama la, lakini pia nadhani wanawapa serikali nafasi na kisingizo cha kutokamilisha yale ambayo pengine hata bila kisingizio hicho yasingekamilika kwa wakati. Ninapoangalia ujenzi wa kuitwako mabondeni unavyoendelea huku serikali ikisema si makazi ya watu lakini shirika la serikali na ugavi wa Umeme limeweka huduma hiyo na kukusanya malipo mwisho wa mwezi napata kigugumizi kama aliyejenga kule ndiye aliyekosea ama aliyepeleka huduma ya umeme mahali ambapo atakuja kuvunja baadae ndiye mkosaji? Na mipango miji je? Kujenga shaghala baghala lakini ukapewa huduma zote kisha serikali ikasema hakujapimwa ni nini? Na kwanini watu wajenge wakati wanajua huko ni mabondeni? Na kwanini serikali ipeleke huduma ilhali yajua hakustahili? Nani wa kupewa lawama kwanza?

Maswali mengine huwa yana majibu kulingana na "maslahi" ya mjibuji na wala si usahihi wa hali halisi na hili nahisi ni moja kati ya hayo.

Pengine namna nionavyo tatizo ndilo tatizo. Ukinisaidia naweza erevuka zaidi.
Blessings

2 comments:

Fadhy Mtanga said...

Ok, ok., mwalimu anafundisha nidhamu na madhara ya mapenzi katika umri mdogo kisha ye mwenyewe anatongoza vitoto vya shule. Ok, ok.,daktarh wa mapafu ndo anapuliza fegi usipime. Ayaah,!usishangae mtu anachezea Simba huku ye ni Yanga damu.
Mtu anajenga bonge la mradi eneo la wazi, utamwambia nini? Mmh, we wacha tu kaka...mpiga kampeni mkubwa wa kutonyanyasa na kuajiri watoto wadogo nyumbani kwake ana beki tatu (house girl) na shambaboy anda eitini.
Halafu, mmiliki wa kiwanda cha juisi ye anakunywa juisi za Sauzi. Hivi ni kweli? Mmhu, yah, sijui nini tena!
Ni hayo tu!

Yasinta Ngonyani said...

Na pia mmwanamume anamchukua mdogo wa mke wake(shemeji yake) kazi kweli kweli!