Wednesday, February 11, 2009

Hah!! Kwani msaada wa madeni watakiwa umfae nani?

Nilijivunia kumsikiliza Waziri Mkuu Mhe Mizengo Pinda akieleza jinsi wanavyotegemea "kufunga mkanda wa anasa" za magari ya kifahari kwa ajili ya kuwafaa wananchi. Ilikuwa moja kati ya zile taarifa ambazo unapozisikia unapata ahueni ya fikra kuwa baada ya yote kusemwa, hatimaye wamemka. Lakini wakati naendelea kusaka habari za nini na kipi kimetokea nyumbani, nikakutana na hii ya Zanzibar ambako Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Kiongozi Mhe Hamza Hassan Juma amesema pesa za msamaha wa madeni ambazo hazitokani na kodi ya wananchi zimetumika kuwanunulia "watendaji" mashangingi 80 na pia matrekta 12 kwa ajili ya kuendeleza kilimo Unguja a Pemba.
Bofya hapa kusoma kioja kamili.

Zanzibar ina matatizo mengi saana na siamini kama kulikuwa kuna ulazima wa kumaliza pesa hizo kwa kununua mashangingi ambayo viongozi wasio na uchungu nayo watayatumia kwa namna watakavyo tena kwa gharama za kodi ya wananchi. Sina hakika na gharama za kuyaendesha na kuyakarabati kwa mwaka na zinatoka kwa nani. Ninaamini inawagharimu wananchi fedha nyingi kuwaweka "viongozi" barabarani kuliko wanavyosaidiwa na viongozi hao. Kununua magari 80 ya kifahari kwa viongozi na matrekta 12 kwa wananchi wenye uhitaji ilhali hali za hospitali na sehemu nyingine za huduma za wananchi twazijua zilivyo ni kupoteza pesa na kuongeza mzigo kwa mwananchi anayehitaji msaada.

1 comment:

Subi Nukta said...

Nadhani tatizo kubwa ni 'kutokujali'. Imefika hatua kuwa matatizo ya wananchi ni kama wimbo na si kitu cha kushangaza ama kuhuzunisha. Ni kama umekuwepo usugu fulani juu ya matatizo ya binadamu mwingine na 'umimi' umezidi sana. Waliobaki wenye imani na wenye kutenda kwa imani ni wachache sana, aghalabu, wengi wao wanamezwa na mabaradhuli wengi.
Lakini kelele zisikome, kwani nina hakika huwa wanapata japo mawili matatu yanayoandikwa katika blogu zetu sema hawathubutu kukiri hadharani.