Na leo najiuliza kama tunasherehekea miaka hiyo kwa kufuata matakwa ya wale wallio (ama niseme wanaotakiwa kuwa) huru ama kwa kuendeleza mifumo na taratibu za KIKOLONI NA KITUMWA?
Sijui kama ni maigizo ya ya Rais na serikali yake ama ni nini, lakini najiuliza ni kipi cha muhimu kinachotendeka katika sherehe za miaka ya uhuru ambacho hakiwezi kufanyika bila gwaride hilo la gharama?
Hivi serikali inaweza kueleza UMMA kuwa ni kiasi gani cha fedha kinatumika kuandaa gwaride la sherehe za uhuru? Gharama za kuwakaribisha, kuwalinda na kuwasafirisha viongozi wa nje wanaokuja kuhudhuria sherehe hizo, mazoezi ya gwaride, mavazi ya washiriki, mafuta kwa misafara yote, usalama, gharama za ukarabati wa nyasi ya uwanjani na mengine (achilia mbali "cha juu"), kisha kinachofuata ni HOTUBA ya Rais baada ya "kukagua" gwaride.
Hivi Rais hawezi kutoa hotuba kupitiq Redio?
Kwanini serikali itumie mamilioni ya pesa kwa gwaride ilhali NCHI INA UHITAJI MKUBWA WA HUDUMA ZA ELIMU na AFYA ambako kuna uwiano wa mashine moja ya X-RAY kwa wananchi 400,000? Angalia Video hii kujua hali nzima ya afya
Hivi ni lazima uhuru wa nchi yetu (ambao wananchi wengi wa kipato cha chini hawaufaidi) usherehekewe kwa namna ambayo nina hakika wananchi wengi hawataiidhinisha wakipewa takwimu halisi za gharama zake?
NA WABUNGE WETU nao wapo tu wakikusanya pesa bila hata kuhoji pesa zitumikazo kwa sherehe hizo na uhalali wake ukilinganisha na mahitaji halisi ya mTanzania wa leo?
Kama leo hii ingepitishwa kura za maoni kujua wananchi wanapenda kusherehekea UHURU kwa namna na gharama za sasa, NINA HAKIKA kuwa wengi wangepinga.
Lakini WATAWALA wetu hawawafikirii wananchi hata kidogo.
Huu ndio ungekuwa wakati wa Rais kujibu maswali muhimu ambayo yangekusanywa na watendaji wa vijiji, kata, tarafa, wilaya na mikoa na hata wabunge badala ya yale MAIGIZO aliyofanya ya kujibu maswali ya TABAKA MOJA LA WATANZANIA. Nasema tabaka kwa kuwa njia iliyotumika kukusanya maswali hayo (kwa sms na email) ilikuwa aghali kuliko bajeti ya siku kwa waTanzania wengi. Ndio maana maswali yalitoka kwa "wenye kujiweza" ambao ni wachache na ambao hawakuuliza matatizo halisi ya mTanzania mhitaji.
Tanzania Yangu ni kipengele kinachozungumzia ytale yaendeleayo nchini Tanzania na namna ambavyo "ndivyo sivyo" inavyozidi kupamba moto nchini. Kwa matoleo yaliyotangulia BOFYA HAPA
Tuonane "Next Ijayo"
5 comments:
Hii ndiyo Tanzania yetu... Kuna wakati huwa najiuliza kama viongozi wetu huwa wanafikiri kwa makini wanapofanya maamuzi yahusuyo mstakabali wa taifa letu. Na mbaya zaidi, kadri siku zinavyokwenda ndipo nionapo vipaumbele vinawekwa katika mambo yasiyobadili hali za maisha.
Ni kazi kwelkweli!
siasa zetu hizi. sasa wanakuwa vituko mbele ya vijana wa kizazi kipya wasiojua maana ya uhuru wasiojua umuhimu wa uhuru na sasa wanajiona utumwani kuliko ule wa zamani
Mimi nasema... nashukuru kwa kunikumbusha ya kuwa siku ya uhuru wa Tz imekaribia. Nafikiri uzalendo umeanza kuniponyoka kwa sababu ya madudu mengi...
Tafsiri halisi ya uhuru ule wa mwaka 1961 si tafsiri ya uhuru unaokumbukwa leo . Kwa hali ya watanzania wachache kumiliki uchumi na njia za uchumi, hali ya ufisadi, rushwa zilizokithiri,mikataba mibovu ya madini na waliodai kutuacha huru,mikataba isiyokuwa na tija kwa wananchi na kwa taifa na mambo mengine mengi. Watanzania wachache wanatunyang'anya uhuru wetu kwa maslahi yao. Hatuko huru, twatawaliwa na wazawa(watanzania wachache wazawa), hivyo twalazimika tena kuingia vitani(vile vile bila kumwaga damu) ili hatimaye siku moja tujitangazie ushindi ulio na ukombo wa kweli dhidi ya wazawa wachache wanaotunyonya na kutukandamiza ki-manpower na ki-akili. Leo hii raisi akiulizwa kama malengo ya watanzania kuupigania uhuru na hatimaye kuupata na malengo hayo yametimizwa kwa kiasi gani, sijui kama ataweza kutoa majibu mazuri, kwani kadiri siku zinavyokwenda linabaki swala la "ni bora ya jana kuliko ya leo" japokuwa hata ya jana yalionekana kuwa mabaya kuliko yale ya juzi.Sikatai, kuna mazuri yaliyokwisha fanyika lakini kwa njenzo za uchumi tulizo nazo pamoja na UHURU WA MWAKA 1961 hatukutakiwa kuwa hapa tulipo hata kidogo.
Mzee wa Changamoto
Tatizo ni jamii ya waTanzania. Wanapenda sherehe na makamuzi. Angalia takwimu ya ununuaji wa bia, utaona kuwa watu pesa iko sana mifukoni. Kila kona kuna baa, na baa zinazidi kuongezeka.
Hata katika vimiji vidogo, utaona baa zimejengwa kwa ubora sana, wakati shule hapo pembeni ni ya makuti na haina madawati. Watoto wanakaa sakafuni, au wanakalia mawe.
Watanzania hapo kwenye kamji utawakuta wanalamba ulabu bila wasi wasi, wakati shule ni ya makuti.
Watanzania hapo kwenye mji utawakuta wanajumuika kupanga sherehe za arusi ambazo ni za nguvu na gharama kubwa. Misafara ya arusi inapita hapo kwenye kashule ka makuti, na hakuna anayewazia kupunguza sherehe ili kukarabati shule.
Serikali ya Tanzania ikithubutu kusema baa zifungwe wiki nzima, ili watu wafanye kazi, serikali hiyo itaangushwa vibaya kwenye uchaguzi ujao. Watanzania wanataka starehe na makamuzi.
Ni kweli, wako ambao ni maskini, hawana hela. Lakini akili yao sio tofauti na ya wale wanaotanua na kukamua. Hao maskini nao ndoto yao ni siku moja kuwa watanuaji na wakamuaji.
Sasa katika kutekeleza hii ndoto, unaona watu wanafanya kila namna kujitafutia utajiri, hata kwa kuwachuna ngozi wengine.
Hatuna maadili kama yale aliyoongelea Mwalimu Nyerere, ya kujali utu kwanza, na kutoabudu mali. Nyerere alikemea mambo ya ulimbwende na matanuzi, tangu mara tulipopata Uhuru.
Leo, kuanzia viongozi hadi walalahoi, ndoto yao ni kukamua au kupata fursa ya kukamua.
Post a Comment