Wednesday, March 10, 2010

Unasoma upate kazi, kisha wafanya kazi miaka tele kulipia masomo hayo.

Image from PayScale Resources
Machi 4 niliandika kuhusu gharama za matibabu hapa nchini Marekani katika post niliyoipa kichwa Watu hutengeneza pesa,..... japo pesa zathaminiwa zaidi yao (Bofya hapa kuirejea). Baada ya hapo nilijitahidi kusaka sababu zinazoweza kusababisha gharama hizo kuwa juu na hata madaktari kufanya kazi zaidi ya moja licha ya kulipwa pesa nzuri. Habari niliyoisikia leo katika kituo nikipendacho cha NPR, ilinishitua kiasi. Kwa wastani, Daktari anapomaliza masomo anakuwa na deni la zaidi ya dola 150,000 na wengine wanakuwa wakidaiwa mpaka dola 300,000.
Ina maana kwa wastani, mhitimu wa udaktari hapa nchini anakuwa akilipa mkopo huo kwa kiasi cha dola 1500 kwa mwezi.
Sitaki kuamini kuwa gharama hizi za masomo ndio chanzo cha gharama kuubwa za matibabu, lakini sitegemei mtu anayesoma kwa gharama za juu namna hii na kuwa na deni kubwa la hivi kuja kutoa huduma ya gharama za chini. Hasa ikizingatiwa kuwa asipolipa mkopo wake kwa muda muafaka wanaweza kufanya lolote watakalo kupata pesa zao.
SIKILIZA HABARI HII TOKA NPR ili uendelee kujiuliza nami namna ambavyo madaktari wetu WANASOMA ILI WAPATE KAZI.... KISHA WANAFANYA KAZI MIAKA MINGI WAKILIPIA GHARAMA ZA MASOMO YAO.
Ama kweli

1 comment:

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Yote kwa yote mimi nadhani huu ni utaratibu unaosaidia vijana wao kupata elimu ya juu. Bila utaratibu huu serikali ingebidi ibebe mzigo wa kulipia gharama za elimu - mtindo ambao ni kinyume na mfumo wao wa ubepari dume wanaouendesha hapa. Akina Rush Limbaugh, Glen Beck, Ann Coulter, O'Reilly na "vichaa" wengine wa kihafidhina bila shaka wangeehuka kama hili lingetokea.

Kama gharama hizi ni sababu mama inayowafanya madaktari watoze ada ghali namna hii (drip moja tu ya maji inaweza kukugharimu dola 500 halafu bili inaandikwa kwa kutumia bonge la msamiati wa kitiba), pengine serikali ingeweza kutafuta utaratibu wa kuwapunguzia mzigo wa deni la mkopo wa masomo yao.

Hii inaturudisha kwenye mzunguko fumano usio na fundo na ukiangalia vizuri unaweza usione hasa nani anayestahili kulaumiwa hapa. Na anayefaidika na mfumo huu si daktari wala mgonjwa bali hayo makampuni yanayotoa mikopo pamoja na makampuni ya bima. Nadhani hali imekuwa mbaya mpaka baraza la Congress limeamua kuingilia kati ili kujaribu kuona kama kuna uwezekano wa kupunguza riba katika mikopo inayotolewa kwa wanafunzi. Ubepari...Huwa natamani sana kama Karl Marx angekuwa sahihi katika utabiri wake....