Leo tunashuhudia nchi yangu niipendayo ya TANZANIA ikiadhimisha MIAKA 49 YA UHURU. Mwaka juzi niliandika HAPA kuhusu nilivyoona tatizo la sherehe hizo na HAPA kuhusiana na suala zima la sherehe hizo zilivyosherehekewa. Na leo najiuliza kama tunasherehekea miaka hiyo kwa kufuata matakwa ya wale walio (ama niseme wanaotakiwa kuwa) huru ama kwa kuendeleza mifumo na taratibu za KIKOLONI NA KITUMWA? Sijui kama ni maigizo ya Rais na serikali yake ama ni nini, lakini najiuliza ni kipi cha muhimu kinachotendeka katika sherehe za miaka ya uhuru ambacho hakiwezi kufanyika bila gwaride hilo la gharama? Hivi serikali inaweza kueleza UMMA kuwa ni kiasi gani cha fedha kinatumika kuandaa gwaride la sherehe za uhuru? Gharama za kuwakaribisha, kuwalinda na kuwasafirisha viongozi wa nje wanaokuja kuhudhuria sherehe hizo, mazoezi ya gwaride, mavazi ya washiriki, mafuta kwa misafara yote, usalama, gharama za ukarabati wa nyasi ya uwanjani na mengine (achilia mbali "cha juu"), kisha kinachofuata ni HOTUBA ya Rais baada ya "kukagua" gwaride.
1: Hivi Rais hawezi kutoa hotuba kupitia Redio ambazo zinawafikia wengi kuliko wanaoweza kuingia hapo kiwanjani na hata kutazama kwenye runinga?
2: Kwanini serikali itumie mamilioni ya pesa kwa gwaride ilhali NCHI INA UHITAJI MKUBWA WA HUDUMA ZA ELIMU, MIUNDOMBINU na /ama AFYA?
3: Wiki hii nimesikia takwimu kuwa kati ya viwanja vya ndege 60 vilivyopo Tanzania (58 bara, 2 Visiwani)9 tu ndio vina lami na 5 pekee ndio vyenye uwezo wa kuhudumia usiku. Kwa maana hiyo, wastani wa huduma za ndege kibiashara ni saa 15 kwa siku nchini Tanzania.
Na bado twaamini tunataka kufanya biashara ili kuendeleza nchi
Hii ni jana tu pale Bibi Titi Mohamed. Ndani ya DAR CITYYYYY. Si unajua "nchi yetu ni ya kiangazi tuuu?"
Photo Credit:Robert Okanda of Daily News
4: Kwanini pesa hizi zisichimbe visima, ama kukarabati mabwawa ya umeme unaokatika kila uchao, ama kukarabati barabara, ama madaraja ama kusaidia katika huduma ya Afya tunaposikia uwiano wa mashine moja ya X-RAY kwa wananchi 400,000 na daktari mmoja kwa watu 40,000? Angalia Video hii kujua hali nzima ya afya NAWAZA....... Hivi ni lazima uhuru wa nchi yetu (ambao wananchi wengi wa kipato cha chini hawaufaidi) usherehekewe kwa namna ambayo nina hakika wananchi wengi hawataiidhinisha wakipewa takwimu halisi za gharama zake?
NA WABUNGE WETU nao wapo tu wakikusanya pesa bila hata kuhoji pesa zitumikazo kwa sherehe hizo na uhalali wake ukilinganisha na mahitaji halisi ya mTanzania wa leo? Kama leo hii ingepitishwa kura za maoni kujua wananchi wanapenda kusherehekea UHURU kwa namna na gharama zitumikazo sasa (ikiwa zitatajwa gharama halisi), NINA HAKIKA kuwa wengi wangepinga. Lakini WATAWALA wetu hawawafikirii wananchi hata kidogo.
Huu ndio ungekuwa wakati wa Rais kujibu maswali muhimu ambayo yangekusanywa na watendaji wa vijiji, kata, tarafa, wilaya na mikoa na hata wabunge badala ya yale MAIGIZO aliyofanya ya kujibu maswali ya TABAKA MOJA LA WATANZANIA. Nasema tabaka kwa kuwa njia iliyotumika kukusanya maswali hayo (kwa sms na email) ilikuwa aghali kuliko bajeti ya siku kwa waTanzania wengi. Ndio maana maswali yalitoka kwa "wenye kujiweza" ambao ni wachache na ambao hawakuuliza matatizo halisi ya mTanzania mhitaji. Tatizo hapa ni kuwa "tunaona wanavyofanya" nasi tunaiga. Kama sivyo basi ni kuwa TUMERITHISHWA HAYA NA WALIOTUTAWALA na sasa bila kujijua TUNASHEREHEKEA UHURU KITUMWA. Ni aibu kufanya haya na kama nilivyowahi KUANDIKA HAPA KUWA UJINGA MKUU NI KUWA MJINGA WA UJINGA WAKO kisha nikanukuu kauli ya Saint Jerome (374 AD - 419 AD)aliyesema "It is worse still to be ignorant of your ignorance", nahisi ujinga tulionao sasa ni kusherehekea uhuru usiokuwepo kwa wengi na kuaminisha kuwa kuwa NDIO UTASHI WA WENGI. Lakini hili si la kushangaa. Tumeona TAKWIMU ZA MATOKEO YA URAISI KWENYE UCHAGUZI MKUU 2010 ambapo Raisi wangu alishinda kwa kupata kura 5,276,827 kati ya 20,137,303 za waliojiandikisha (sawa na asilimia 26.20424) na bado “wapambe” wanaendelea kusema ni USHINDI WA KISHINDO. Ni kwa akili hizo hizo, za wapambe hao hao, wenye mtazamo huo huo, tunaendelea kuona kile nilichowahi kuandika kuhusu HESABU ZA KISIASA...MARA ZOTE NI KINYUME. WENGI NDIO WACHACHE NA WACHACHE NDIO WENGI (irejee hapa)
HAPPY UHURU DAY MY PEOPLE....
Tanzania Yangu ni kipengele kinachozungumzia ytale yaendeleayo nchini Tanzania na namna ambavyo "ndivyo sivyo" inavyozidi kupamba moto nchini. Kwa matoleo yaliyotangulia BOFYA HAPA
1 comment:
Yapo mengi sana ya kuwaza na mwisho wa siku utajiona kama ni uwongo kuambiwa kuwa upo huru, ni swala la kutoka kwa bwana huyu na kuingia kwa bwana mwingine...sasa twamtumikia bwana mwingine...angalia mlolongo wa kodi kwa huyu mdanganyika anayedaiwa kuwa yupo hutu...!
Post a Comment