Katika siku zilizopita, niliwahi kuandika nikiuliza kuwa UNA UHAKIKA NI NDOTO SI UFUNUO? (irejee hapa) na hapo nilijaribu kuangalia "mstari mwembamba" baina ya ndoto na ufunuo. Lakini pia nimekuwa SHAHIDI wa kile ambacho nimekuwa nikikiona kama NDOTO lakini kikaja kutimia.
Lakini kabla sijaja na yangu, nianze na ya Dadangu Judith Wambura a.k.a Lady Jay Dee. Nilisoma kwenye gazeti alipotoa albamu ya BINTI akisema kuwa alipoenda kwenye Kora Music Awards punde baada ya kuachia albamu yake ya MACHOZI, alimpa Oliver Mtukudzi aisikilize naye akamshauri kurejea kwenye ala za asili (kama sio ala halisi) na kutotegemea vinanda katika kila kitu. Na matunda tukayaona. Mika Mwamba na P-Funk wakashiriki kutengeneza albamu ya Binti (nyimbo tofauti) wakichanganya ala za kina Andy Swebe na wengine. Kwa ujumla albamu ya Binti ilinoga.
Kisha nikaja kusoma nia ama hamu ya Judith kusimama jukwaa moja na Oliver Mtukudzi kufanya kazi. Na Juni 20 NIKASOMA HAPA jinsi ambavyo walisimama jukwaani na kufanya onyesho moja.
Na zaidi nilifurahishwa na post hii kwenye blog ya Jay Dee kwamba amemshirikisha Oliver Mtukudzi kwenye wimbo wake mpya MIMI NI MIMI.
Huu ni uthibitisho mwingine kuwa UKIOTA, UKAFANYIA KAZI NDOTO ZAKO, UPO UWEZEKANO ZIKATIMIA.
Lakini hili si jambo geni kwa wengi. Labda hatuko makini kuhusisha nia zetu na matokeo yake (kama nilivyowahi kuandika HAPA)
Nakumbuka mwanzoni mwa miaka ya 2000 nilikuwa nikisikiliza Times Fm. Muda nilipofungua tu kituo nikakutana na sauti ya Violeth Mzindakaya (Sister V) na kusikiliza kipindi chake. Nikakipenda na kuvutiwa nacho. Nikawa mfuatiliaji wake nikitamani siku moja kufanya kipindi kama chake ama pamoja naye. Lakini baadae "akapotea". Nikasikia kuwa alibahatika kupata mwana. Nikamtumia kadi ya hongera kisha kumwambia kuwa NATAMANI SIKU MOJA NIFANYE NAYE KAZI.
Wakati huo sikuwa hata na "idea" ya namna studio ilivyo (achilia mbali inavyofanya kazi). Miaka miwili baadae tulikuwa tumekaa kwenye studio nikamuuliza kama anakumbuka kadi yangu niliyosema natamani kufanya naye kipindi. AKAKUMBUKA NA KUSHANGAA.

Wakati huo tulikuwa tukifanya kipindi pamoja.
Lakini wakati nikifanya na Sister V, tayari nilishakuwa mshiriki katika vipindi vya SUNRISE, Michezo na pia MATUKIO YA WIKI.

Kwa wakati huo sikuwa na ndoto wala njozi za kuja Marekani na hata sikuwa katika fani ya habari. Nilishajikita kwenye UHANDISI.
Lakini wiki kadhaa zilizopita nilipokuwa namalizia mazoezi yangu ya vitendo pale VOA, nikawa katika mazungumzo na baadhi ya watangazaji wa pale. Kati yao ni Kaka Vincent Makori na Dada Esther Githui-Ewart ambao wote niliwauliza kama wanakumbuka barua pepe zangu za mwaka 2002 nilipokuwa nikieleza ninavyotamani kufanya nao kazi? Well!! Wakati huo, Kaka Vince alikuwa ni mwelekezi wangu wa shule kwenye suala la sauti, Dada Esther alikuwa mhariri wa zamu
Na bado nilikuwa nikifanya kazi na kina Mkuu wa Idhaa Mwamoyo Hamza, Abdushakur Aboud na Khadija Riyami ambao wote niliwaandikia wakati huo, na pia nyongeza ya Mary Mgawe, Mkamiti Kibayasi, Sunday Shomari na Aida Issa.
Ninalomaanisha hapa ni kuwa LICHA ya kubadili mazingira, licha ya kuchukua muda mrefu, na licha ya kuendelea kupita njia nyingine mbalimbali, bado TUNATAKIWA KUENDELEA KUAMINI KATIKA KILE CHEMA TUAMINICHO kwani NDOTO NI KAMA HATUA.....NASI TWATAKIWA KUENDELEA KUSONGA.
Miaka 9 baadae nimekaa meza moja na kufanya kazi na wale ambao nilitamani kufanya nao kazi. Kabla HATUJAKATA TAMAA, KABLA HUJAJIAMINISHA KUWA NDOTO YAKO HAIWEZEKANI....JIPE MUDA. Kwani NDOTO NI KAMA HATUA. Hivyo......KEEP ON MOVING

Sikiliza hapa ushiriki wangu katika jumatatu ya mwisho ya awamu yangu hii ya kwanza "kazini" pale.
5 comments:
Hii Imekaa vizuri. Kila la heri mkuu. Nategemea kukusikia siku moja ukiunguruma VOA, BBC au DW kwani una kila kitu ambacho mtangazaji na mchambuzi makini anatakiwa kuwa nacho.
Ni lazima tuendelee kuota ndoto zetu hata zile ambazo zimegeuka kuwa za majinamizi. Hata hizi bado tunaweza kuzigeuza na kuwa za matumaini...Tusikate tamaa.
Inaniuma sana ninapoona makala nzuri kama hizi haziwafikii wasomaji wengi. Inabidi wanablogu tutafute njia ya kuchapicha makala makini kama haya magazetini...
Hongera mkuu, kweli tusikate tamaa na matarajio, maana mataraji ya wema yanakuja kwa wema..ipo siku ndoto zetu zitakuja kuwa za kweli, ...lakini tusipweteke, tukalala tukisubiri kuwa tutaota kufika Maraekani au ulaya, bila ya juhudi.
Sifa kwako mkuu, kwani maratajio yako na juhudi zako zimezaa ile ndoto yako..au sio?
Nakuunga mkono MMN
Safi sana kaka Bandio ipo siku watu wataelewa juhudi mnazozifanya za kutaka Afrika isimame kwa miguu yake yenyewe ijitegemee kuliko hivi sasa ambapo tumekuwa ombaomba , naomba nitoe wito kwa wana mageuzi wote wapitie kitabu cha professor Rwekaza Mukandala mkuu wa chuo UDSM kiitwacho from proud faces to baggers kinaweza kuongeza hamu ya kujitegemea miongoni mwa waafrika
kaka umenena,Ahsante sana kwani nimejifunza kitu hapa, Pamoja kaka!!!
wow. its nice one. keep it up!!!
Post a Comment