Saturday, December 3, 2011

Nawaombea viongozi wapate ajali kama zetu, wahisi maumivu yetu, watatue tatizo letu na kuokoa maisha yetu.

Photo Credits:Orlando Grace Church
Mafunzo ya imani yanatufundisha ama kutuelekeza kuwa BINADAMU WOTE NI SAWA.
Ni kuwa licha ya tofauti zetu za mali, rangi, imani, pesa, kimo, kabila nk bado tu-sawa na TUNA UHAI ULIO SAWA.
Lakini HILI SI KWA WATAWALA wetu. Tumejengewa TOFAUTI KUBWA SANA KATI YA UHAI WA MTAWALA WETU NA MWANANCHI WA KAWAIDA. Uhai wa hawa wajiitao VIONGOZI umeonekana kuwa na thamani sawa na makumi, mamia na ama maelfu ya wananchi wanaowaongoza. KIFO CHA KIONGOZI NI KIFO, LAKINI CHA MWANANCHI NI TAKWIMU (hata kama wote wamekufa kwa sababu inayofanana). Ndio maana awapo kiongozi hata shughuli za nchi zitasimama, japo ili zisimame kwa mwananchi, lazima liwe JANGA LA KITAIFA.
Na ndio maana thamani ya mwananchi wa kawaida haionekani katika mikakati ya serikali kujali uwepo wao. Kwa maana nyingine ni kuwa VIONGOZI WETU HAWATUJALI.
Tumeshuhudia namna ambavyo watawala wa nchi mbalimbali wanavyotumia maelfu ya maisha ya wananchi wao KUKINGA NAFASI NA MAISHA YAO.
TATIZO la ajali kwa TANZANIA si tatizo la jana wala juzi. Si tatizo ambalo tunaona likipata unafuu wowote na hasa siku ama nyakati hizi za mwisho wa mwaka ambapo wasafiri huongezeka, wenye magari KUTAMANI PESA ZAIDI na wenye mamlaka ya kusimamia sheria za barabarani "KUCHUMA" ZAIDI. Wananchi KUTAMANI ZAIDI KUFIKA ilhali wakipuuza njia sahii za kuwafikisha huko nk. YOTE JUU YA YOTE, NYAKATI HIZI USALAMA HUPUUZWA NA AKILI KUWEKWA KWENYE PESA.
Na KAMA KAWAIDA ya serikali yetu, haionyeshi kuwa na mikakati madhubuti ya kupunguza na pengine kufuta ajali za kizembe, bali kitakachofuata ni SALAMU za rambirambi toka kwa viongozi. Nilisema hapa kuwa TUMECHOSHWA NA SALAAM ZENU ZA RAMBIRAMBI NA SASA HATUZITAKI. Kila salaam ya rambirambi inaambatana na ONYO KALI KWA WATENDAJI kuhakikisha kuwa ajali zinapungua ama kushughulikiwa, lakini hakuna tofauti. Kwenye salaam zake za mwanzoni mwa mwaka 2009, Rais Kikwete alisema "hatuwezi kuvumilia kutokea kwa ajali hizi wakati mamlaka zenye dhamana ya kusimamia sheria za usalama barabarani zipo. Tufanye jitihada zote zilizo ndani ya uwezo wetu kupunguza kwa kiwangi kikubwa na ikiwezekana kukomesha kabisa ajali hizi za barabarani ambazo zimeshapoteza maisha ya wenzetu wengi"
KUNA MABADILIKO GANI YA DHATI YALIYOFANYWA?
Kwa mujibu wa ripoti hii ya kwanza kutolewa na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) kuhusu hali ya dunia katika usalama wa barabarani, watu milioni 1.3 hufa kila mwaka na kati ya milioni 20 na 50 hupata majeraha makubwa katika ajali. Na kwa mujibu wa TAKWIMU HIZI KAMILI juu ya ajali hizo, Tanzania inayokadiriwa kuwa na watu takriban milioni 40.4 inapoteza watu (wanaoripotiwa) 34.3 katika kila watu 100,000 kutokana na ajali za barabarani. Hii si idadi ndogo hata kidogo na hasa ikizingatiwa kuwa asilimia kubwa ya ajali hizi zingeweza kuepukika kama serikali ingeweka mkakati mzuri wa kukabiliana na tatizo hili.
Baraza la mawaziri lililotangazwa Novemba 2010 lilikuja na utata wa nani atakayekabiliana na suala la ajali, na kwa kuwa HAKUNA aliyekubali kutekeleza OMBI HILI lililowataka MAWAZIRI WAORODHESHE WATATENDA NINI, VIPI NA KUFIKIA LINI, bado swali linabaki palepale kuwa "Ni nani atakayechukua jukumu la kushughulikia kuzuia ajali na kuratibu usalama wa wananchi? Je! Ni Wizara ya Ujenzi (Barabara na Uwanja wa Ndege), Wizara ya Uchukuzi (Reli, Bandari, Usafiri Majini) ama Wizara ya Usalama wa Raia (ambayo hata sijui imekuwa "faded" ndani ya wizara ipi? Ama ni wizara gani?)"
Leo hii bado tunasikia vifo vingi vitokeavyo kutokana na ajali ambazo bado twaamini nyingi zingeweza kuzuilika.
Tumezoea kusema AISIFIAYE MVUA IMEMNYEA. Kweli, na mimi MVUA YA AJALI ILININYEA. Lakini tusisahau kuwa si kila aina ya mvua ikunyesheayo hukupa nafasi ya pili ya kukauka na kuwa kama ambaye hakuguswa nayo. Kuna masimulizi ambayo huwakuta watu walionyeshewa na mvua hizo ambayo wanatamani wasingekuwa wasimuliaji wa habari ama hali hizo na licha ya juhudi zao za hali na mali katika kuhakikisha hatupitii yale wapitiayo wao, bado twapuuza na matokeo yake ni sisi kuteketea.
TUSISUBIRI MVUA YA AJALI ITUNYESHEE KWANI HATA TUKIPONA, HATUTAKUWA KAMA TULIVYOKUWA AWALI.
Kwa kumbukumbu niliyonayo, mara ya mwisho niliposikia serikali ikionekana kuamka na kuzungumzia tatizo la ajali kwa namna ya suluhisho ni pale lilipohusisha WAHESHIMIWA. Na kwa hakika tuliona mabadiliko kidogo mpaka walipoonekana kuwa salama TUMEREJEA KWENYE KULIPUUZIA.
Hili linanifanya niamini kuwa serikali haioni tatizo la ajali kwa waTanzania mpaka pale litakapowahusisha viongozi, na ndio maana sasa natamka wazi kuwa NAWAOMBEA VIONGOZI WAPATE AJALI KAMA ZETU, WAHISI MAUMIVU YETU, WATATUE TATIZO LETU NA KUOKOA MAISHA YETU.

No comments: