Monday, February 18, 2013

Matokeo MABAYA ya kidato cha nne.....NI AKISI YA JAMII INAYOMOMONYOKA.


Photo credit:WAVUTI.COM
Kwenye matokeo haya ya kidato cha nne, nahofia zaidi waliofaulu kuliko waliofeli.
Kwa kuwa nahofia uongo kuliko ukweli.
Na nahisi wapo wafaulishwao mitihani wakifelishwa maisha.
TATIZO langu si nani kafeli na nani kafaulu.
Tatizo ni NINI KUFELI NA NINI KUFAULU?
TAFAKARI NAMI....
1: Unafahamu kuwa nchi yetu ipo ilivyo kwa kuwa imekuwa ikiongozwa na WATAWALA WALIOFAULU tena saana (kwa mujibu wa vyeti vyao)?
2: Unafahamu kuwa ni viongozi haohao waliofaulu ndio wanaopanga mitaala na vipimo vya ufaulu na ufeli wetu?
3: Unafahamu kuwa MITAALA YETU HAIMFANYI AFAULUYE AWEZE KUITUMIKIA JAMII IPASAVYO?
Na kuwa....
Wapo wanaofeli kwa kuwa wana majukumu ya kijamii yanayowakabili hata wawapo shuleni?
Na kuwa....
Wapo wafauluo kwa kuwa wanapuuza chochote katika jamii ili watumie muda wote KUKARIRI majibu ya mitihani yasiyoisaidia jamii?
Ndio maana kuna wakati ninaohisi waliofeli wanaweza kuwa msaada kwa jamii kwa kuwa kiwafelishacho ni USHIRIKA WAO KWA JAMII.
Ukweli ni kuwa MITAALA YA ELIMU YETU HAIMFUNZI MWANAFUNZI KUWA SEHEMU YA MAENDELEO YA JAMII.
Ni kweli kuwa waliofaulu sasa hawajui namna ya kukabiliana na mazingira ya maisha ya nyumbani.
Na ndio maana kuna baadhi ya mambo yanayohusisha WALIOFAULU yanatia shaka.
UNATAKA MIFANO?
Inapatikana kwenye POST HII ambayo ndani mwake nilitoa mifano ya namna ambavyo Tanzania Yangu iko na mikakati thabiti ya KUUA KILICHO CHAKE.
Niliuliza.....
Hivi kama serikali (ambayo naamini ina magari mengi sana) ingeweka ulazima wa magari yote kununua matairi kwenye viwanda vya ndani kama General Tyre, VINGEKUFA? Ama watasema matairi yaliyokuwa yakitengenezwa Arusha hayakukidhi ubora wa barabara na hali ya Tanzania?
Hivi kama serikali ingeweka mkakati madhubuti na kuamua kutumia magari yanayotengenezwa na kiwanda cha jeshi cha NYUMBU katika idara na ofisi zake zooote nchini, tusingepunguza uagizaji wa magari? Ama watasema MAGARI YA NYUMBU HAYAKO KATIKA KIWANGO CHA TANZANIA ukilinganisha na magari yatokayo Marekani / Japan / China?
Hivi serikali ingeamua kutumia (japo asilimia kubwa ya) saruji ya nyumbani, nondo za nyumbani na mafundi wa nyumbani kujenga "vikwangua anga" vyote vya nyumbani, ajira ingekuwa katika kiwangi ilichopo?
TUNAO "WASOMI" WALIOFAULU (kama vyeti vyao ni sahihi) WANAOFANYA MAAMUZI HAYA YASIYOTHAMINI VILIVYO VYETU.
Ni vipi tutaendeleza VAZI LA TAIFA iwapo mBunge asiyevaa SUTI haonekani kuvaa kiheshima ndani ya Bunge la Tanzania? Hata suti tunasikia kuwa wazivaazo wanazitoa nje ya nchi (kama WIKILEAKS ilikuwa sahihi).
Tutawezaje kuendeleza uzalishaji wa magari ya nyumbu ikiwa yale waliyotengeneza miaka hiyo hayajapata mteja na wala kupata nafasi ya kuonyeshwa na kunadiwa (zaidi ya siku ya maigizo ya uhuru)?
Ni vipi kiwanda kama General Tyre kingeshindana na viwanda vya nje iwapo maelfu ama malaki ya magari ya serikali yanatumia matairi yaliyoagizwa nje?
NIKUMBUSHE NILICHOWAHI KUANDIKA HAPA KWENYE POST HII ILIVYOSEMA "TUNAPOFELISHA KIZAZI KWA KUFAULISHA MITIHANI.
Sehemu ya post hiyo niliandika
"Lakini mifumo iliyojengwa na waalimu wetu (ambao yawezekana wamejengewa na waalimu wao) ni kuwa unastahili kupata daraja fulani ili uonekane umefaulu. Na ndio maana msisitizo hauko kwenye kuelewa na kuweza kutumia elimu katika maisha na kutatua matatizo ya jamii, bali ni katika kufaulu mtihani kwa kupata maksi kadhaa.
Tusemeje kuhusu WASOMI wetu wa IDARA YA MAWASILIANO IKULU? Unadhani hawakufaulu? Unadhani kuna sehemu yahitaji watu "waliofaulu" vema kama sehemu nyeti kama hizo? Umeshajiuliza wafanyalo huko? Basi SOMA HAPA ama HAPA uone WAFAULU MITIHANI HAWA WANAVYOLIFELISHA TAIFA KWENYE MAMBO NYETI KAMA MAWASILIANO HUKO IKULU
Na pia nimekuwa nikiona maswali meengi kuwa "kwanini wahandisi wa Tanzania hawabuni vitu vya kuisaidia jamii wakiwa nyumbani" na nahisi hili ndilo jibu lake. Kuwa waandisi ambao wamekuwa na alama nzuri darasani na kutunukiwa vyeti mbalimbali kuonesha UFANISI DARASANI lakini wanapoingia kwenye "ulimwengu wa kazi" inakuwa ni shughuli nyingine kabisa kwani wafunzwacho kwa nadharia hakionekani kuwa halisi kwenye utendaji wao. Ni hapo waajiri wanapoanza kusaka kama waajiriwa wao wana vyeti visivyo halali ama walipata matokeo hayo isivyo halali. Lakini mwisho wa siku ni kuwa WALIFUNZWA KUFAULU MITIHANI NA SIO KUFANIKISHA KAZI WASOMEAZO.
Yaani kwa wabunge ndio yaleyaleee. Kuonekana anafaulu kwa kupigiwa makofi katika kila asemacho hata kama hakina utekelezaji. Yaani twaifelisha jamii yetu kwa kufaulisha kile tunachoamini kuwa mtihani japokuwa kitu hicho si suluhisho la matatizo tuliyonayo."
Ukweli wa mambo ni kuwa MATOKEO MABAYA yameonyesha namna ambavyo JAMII YETU IMEFELI.
Hili si TATIZO....NI MATATIZO.
Hapa ni matatizo mengi.
Hili ni la kijamii zaidi.
Ni malezi kwenye jamii.
Ni maandalizi ya wanajamii.
Ni "utumwa wa kiakili" kwa jamii yetu.
Ni mitaala na vitendea kazi.
Ni moyo wa kazi na wito.
Ni mishahara na maisha ya walimu.
Ni majukumu na mazingira ya wanafunzi

Tazama takwimu hizi zilizobandikwa kwenye UKURASA HUU WA Mhe. Zitto Kabwe
2012 Form 4 results

DIV 1: 1,641 (0.4%)
DIV 2: 6,453 (1.6%)
DIV 3: 15,426 (3.9%)
DIV 4: 103,327 (26.0%)
DIV 0: 240,903 (60.1%)

2011 Form 4 results

DIV 1: 3,671 (1.09%)
DIV 2: 8,112 (2.41%)
DIV 3: 21,794 (6.84%)
DIV 4: 146,639 (43.60%)
DIV 0: 156,085 (46.41%)

2010 Form 4 results

DIV 1: 5,363 (1.53%)
DIV 2: 9,944 (2.83%)
DIV 3: 25,107 (7.14%)
DIV 4: 136,777 (38.9%)
DIV 0: 174,407 (49.60%)

2009 Form 4 results

DIV 1: 4,419 (1.78%)
DIV 2: 10,493 (4.21%)
DIV 3: 27,310 (11.2%)
DIV 4: 130,651 (52.61%)
DIV 0: 65,708 (26.46%)

DHIHIRISHO LA AKISI YA JAMII INAYOMOMONYOKA NA ILIYO NA VIONGOZI WASIOJALI JAMII HUSIKA LITAKUJA  KUDHIHIRIKA PALE ATAKAPOKOSEKANA WA KUWAJIBIKA, KUWAJIBISHWA NA / AMA KUWAJIBISHANA KWA HILI.


Tanzania Yangu ni kipengele kinachozungumzia ytale yaendeleayo nchini Tanzania na namna ambavyo "ndivyo sivyo" inavyozidi kupamba moto nchini. Kwa matoleo yaliyotangulia BOFYA HAPA
Tuonane "Next Ijayo"

1 comment:

Unknown said...

WHAT YOU SAY IS TRUE BUT THE PROBLEM IS HEA IN TANZANIA WE USE TO SOLVE THE EFFECT OF THE PROBLEM BT NOT FINDIND THE SOURCE PF IT AS TO RESOLVE FROM THE ORIGN