Sunday, November 6, 2011

Chonde chonde "waheshimiwa". Kabla hamjasema tena ya Cameron.......

Picha kwa hisani ya Mawasiliano Ikulu Blog
Moja kati ya habari zilizotikisa anga la TAARIFA nchini Tanzania ni suala la serikali ya Uingereza kutoa kauli kuhusiana na haki za mashoga na misaada kwa wale waipingao.
Punde baada ya kauli hiyo tukasikia kauli mbalimbali za viongozi mbalimbali wa Tanzania kuhusiana na hili hasa kwa kuwa lilihusisha SERA na MISAADA kwa nchi zetu. Kauli rasmi ya kwanza ilitolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe Bernard Membe ambaye amenukuliwa akisema “Tanzania ni nchi maskini lakini hatutakubali kuruhusu upuuzi huo eti kwa sababu ya misaada yake na fedha zao, lakini ushoga si utamaduni wetu, hata sheria zetu zinakataa,”
Na kama hukubahatika kusikia kauli ya Mhe Membe basi kuna kitu unakosa katika maandishi haya, msisitizo wa kimatamshi ama niseme "TONE".
Kwa namna alivyotamka, kwa hakika ungetambua kuwa alikuwa akipinga taarifa na kauli hizo za Mhe Waziri Mkuu wa Uingereza. Siku hiyohiyo tukaona "tweet" toka kwenye akaunti itumiayo jina la Jakaya Kikwete (na naamini ni ya mhe Rais kwani kama imekuwepo kwa muda mrefu wangeshaitoa iwapo isingekuwa yake) nayo ilieleza kama unavyoona hapa chiniOK.....WAHESHIMIWA WAMESEMA.
Nirejee nyuma kidogo. Mpaka kwenye post yangu hii ya Februari 24 2010 iliyokuwa na kichwa kisomekacho Wanasiasa wetu na sakata la Ushoga / Usagaji.
Hili bandiko lilikiwa maalum kueleza MTAZAMO WANGU kutokana na kauli ya Mbunge wa chama tawala cha NRM Mhe. David Bahati aliyewasilisha mswada katika Bunge la nchini UGANDA ambao kama ungepitishwa (wakati huo) basi ungewaadhibu MASHOGA NA WASAGAJI walio nchini Uganda na wenye asili ya Uganda kwa adhabu mbalimbali kuanzia kifungo mpaka kifo.
 Katika bandiko hil nilieleza mambo lakini mwanzo nilieleza kuwa ni lazima tujiangalie na kutambua kuwa MASHOGA NA WASAGAJI wamezaliwa katika familia ambazo nyingi ni za watu wasio mashoga wala wasagaji. Kwa hiyo kama wamezaliwa katika familia zilizo tofauti na walivyo wao, NI LAZIMA TUJIULIZE kuwa NI WAPI TULIPOJITENGA NAO NA KUWAFANYA / KUWAACHA WABADILIKE NA KUWA WALIVYO?
Sisi kama JAMII TUNA SEHEMU YA LAWAMA kwa kuwa ama hatuwasaidii kutokuwa walivyo, au tunachochea kuwa walivyo hata kama twatenda haya bila sisi kujua.
HAPA NDIPO NINAPOKUJA KWA WAHESHIMIWA HAWA WAWILI WALIOTOA KAULI.
WAHESHIMIWA...
Kama suala la mashoga na wasagaji linawakera kama ambavyo mmeonyesha kwenye kauli zenu, ni yapi ambayo mmeyafanya kulipunguza ama kuliondoa?
Mimi na ninyi na wasomaji wangu tunajua kuwa kama tungekuwa na mashoga sifuri, basi tusingehofu kuhusu hili. Lakini kwa kuwa idadi yao ni kubwa NA INAONGEZEKA KWA UHURU KILA UCHAO, mnaona athari zake. Lakini kabla hamjasema tena juu ya kauli ya Cameron, mtusaidie kutueleza ni yapi mmefanya kupunguza ama kuondoa ushoga Tanzania?
Tena nimesikia Mhe Membe akisema SHERIA INASEMA WANAWEZA KUFUNGWA MPAKA MIAKA 30 JELA.
Sina hakika ni wangapi walikuwa wakilijua hili, na sina hakika takwimu za Waziri na Rais zaonyesha ni wangapi wameshafungwa kwa hili?
Kama nilivyosema katika post yangu ya mwaka jana, hakuna kiongozi anayetaka kujishughulisha na chanzo cha tatizo. Wanakurupuka kwa namna za KUAHIRISHA tatizo na kisha kutumia uhahirisho huo kujipatia kura za kurejea madarakani. Kisha tatizo larejea.
Wakati nasikia habari za kile nilichokuja kung'amua kama matendo ya kishoga na usagaji nilikuwa mdogo, na nina imani kuwa walikuwepo mashoga na wasagaji wachache saana ukilinganisha na sasa lakini kile wanachokiita "mila za kiAfrika" ziliwazuia wazazi, walezi na viongozi kujadili ATHARI za kujikita kwenye tabia mbaya kama hizo na matokeo yake ndio tuonayo sasa ambapo tatizo hili LIMEOTA MIZIZI na twasikia harakati za KUWAFUNGA MIAKA 30. Kisha baada ya hapo?
Hivi waheshimiwa mmeshawahi kwenda magereza na kuona hali ilivyo?
Magereza zetu hazina zinachofanya kubadili tabia za wafungwa. Niliwahi kuuliza haya katika post hii ya maswali yangu kumi kwa Rais Kikwete, kisha nikauliza hapa KWANI KAZI ZA JELA ZETU NI ZIPI???, na kabla ya hapo niliuliza hapa kuwa UBORA WA JELA NI UPI NA ZETU NI NAMBA NGAPI?, na hata kuhusu "mibambiko" ya jela kama hii hapa, kuhusu Magereza zetu, lakini nani alijishughulisha kujibu? Kwa taarifa yenu, Magereza zetu zasemekana kuwa kama "maskani" za mashoga na / ama vyanzo vya ushoga. Sasa wapelekeni tuhalalishe magereza yetu kuwa "RAINBOW HEADQUARTERS".
Kama ni kweli waheshimiwa wote mmkereka na kauli ya Mhe Cameron, tuambieni mmeshafanya nini, mnafanya nini na mtafanya nini kuondoa suala la ushoga na usagaji ambalo MMEONYESHA kuwa mnalipinga kwa nguvu, ari na kasi MPYA.
Nasio Fontaine aliwahi kuonya katika wimbo wake DANGEROUS kuwa "don't worry about the pretty things you hear them say" na katika ubeti wa kwanza anaanza akisema "I heard your speeches, man and your empty promises. But now that i know, YOUR WORDS ARE DANGEROUS" Hebu msikilize kwa UKAMILIFU

Tuwekeni POLI-TRICKS pembeni na kujaribu kuisaidia TANZANIA YANGU kutoka kwenye MATATIZO yanayotatulika.

5 comments:

Mbele said...

Ninapingana na serikali yetu inaposema kuwa Tanzania ni nchi maskini. Tanzania ina utajiri mwingi.

Kila kukicha, wanafurika watu nchini mwetu wenye uchu wa kuchota utajiri huu. Wengi wa hao, ingawa wanaitwa wawekezaji, ni matapeli. Sasa tangu lini watu wenye kutafuta mali wakamvamia maskini? Kama kweli Tanzania ni nchi maskini, hao watu wote wanatafuta nini kwetu?

Kama ni umaskini Tanzania, uko kwenye vichwa vya hao wanaoitwa viongozi. Umaskini huu wa fikra, pamoja na ufisadi, ndio unachangia kukosekana kwa sera bora za kulinda rasilimali ya nchi hii yenye utajiri kuliko nchi nyingi.

Mzee wa Changamoto said...

Heshima yako Mwalimu Mbele.
SAKATA HILI LIMENIFUNZA MAMBO MAWILI MAKUBWA. Ama niseme limesisitiza katika lile ambalo mimi na wengine twalitambua ama tumekuwa tukilisema na kulisikia lakini si toka midomoni mwa watawala wetu.
Jana wakati nasikiliza Ebony FM ya Iringa, mtangazaji akawa anataja orodha na kauli za viongozi wa serikali waliopinga wazo hili. Mmoja wao alikuwa Mhe. Sofia Simba ambaye alinukuliwa akisema kuwa kama hilo ni sharti la kupata msaada, basi na wakae nayo kwani TANZANIA INAWEZA KUJIENDESHA BILA MSAADA WA NJE.
Nikakubaliana naye hakika, lakini kisha nikawaza, KAMA WANAJUA KUWA TUNAWEZA, NI KWANINI TUSUBIRI MPAKA MKWARA WA KUSITISHA MISAADA UJE NDIO TUWAAMBIE WANANCHI HIVI? Mimi nawe twajua kuwa kama ingekuwa ni hapa Marekani, basi kauli hii ingemfanya AWAJIBIKE kwa kushindwa kutekeleza kile anachojua kuwa anaweza na ambacho kingeisaidia jamii na kuondoa fedheha kwa nchi.
Pili nikasikia kauli ya Waziri Membe kuwa kosa la mahusiano ya jinsia moja linaweza kukufunga jela kwa miaka 30. Nikawaza NI WATANZANIA WANGAPI WANALIJUA HILI? Nikakumbuka post yangu niliyouliza iwapo TAARIFA NI HAKI YA MTANZANIA AMA "FAVOR"?
Tunasubiri mpaka haya yatokee ndio tuseme tuna sheria hii ilhali kuna WIZARA YA SHERIA NA MAMBO YA KATIBA?
Inasikitisha

paulina said...

Tanzania, Tanzania nakupenda kwa moyo wote, ni wimbo ninaoukumbuka wakati nikiwa vidudu na shule ya msingi tulikaririshwa ipasavyo nasi tukawa kama Kasuku kuimba tuu bilakujua maana yake. Nilipojitambua niliacha kuimba huo wimbo kwani nilliona najichora kama watoto wa mjini wanavyosema. Ni viongozi wa nchi hii hii ndio walionifanya niache kuuimba wimbo huu, kutokana na ubinafsi wao wa kujijali wao wenyewe na familia zao na kuwaacha wananchi wengine wakiogelea kwenye wimbi la umaskini wasiojua ni lini watatoka huko. Tanzania kwa mtizamo wangu sio nchi maskini hata kodogo kwa rasilimali tulizonazo tulipaswa kuwa kati ya nchi tajiri duniani lakini kinyume chake tumekuwa masikini wa kutupwa huku viongozi waliopewa jukumu la kuendesha nchi wakijineemesha vya kutosha, Hizi kauli za viongozi wetu za kupinga ushoga ni sawa na bendera fuata upepo isiyokuwa na msimamo inaangalia upepo unavumia wapi. Hivi Rais na waziri wake wanapotoa tamko la ushoga na usagaji ni leo wamelisikia? hawaoni kila siku kwenye jamii yetu? au wanaishi kwenye visiwa peke yao? embu wapeleke UNAFIKI wao huko tumewachoka. TANZANIA tunaweza tukiamua sisi sio masikini, tungekuwa masikini wasingekuja kuwekeza kwetu, WANANCHI TUCHUKUE HATUA KWANI VIONGOZI WAMESHINDWA.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

ushoga

Unknown said...

kama hawapo wasiwasi wa nini....kama kuna ulazima wa sheria manake serikali inakiri mashoga wapo...ukubaliane nao usikubaliane nao wana haki ya kulindwa kikatiba kama raia