Friday, July 30, 2010

Them, I & Them......HYPOCRITES....Nasio Fontaine

"They will smile in your face, stub you on your back,
They will smile in your face, but they wanna get you off your track.....
Their teeths are whites and smiles are brights, filled with hates and hypocrisy
Hands are stretched ready to recieve, cause they know that you're willing to give...."

Umewadia
Wakati
wa sisi waTanzania kusikiliza. Wakati wa kuongeleshwa na wakati wa kusikilizishwa.
Wakati tutakaoona tabasamu kuubwa na nyingi kuliko wakati wowote
Wakati ambao "tutapendwa" na kutoonewa kinyaa
Wakati ambao hata "waheshimiwa" watakaa nasi na kujifanya wanataka kutusikiliza
Wakati ambao watakaa chini na hata ukikaa kwenye kiti chake atasema "kaa tu maana nimekuja kukusikiliza wewe"
Wakati ambao kweli "mteja ni mfalme" (japo kwa nadharia)
Wakati ambao watacheka nasi, watagongesha viganja na ngumi kusalimiana kwa style yetu,
Wakati ambapo watatuonesha kuwa nao wanatuwaza.
Weeeelllll!!!!!!!!! Tuwe makini kwani huu ni WAKATI WATAKAODHIHIRISHA UNAFIKI ULIOMO NDANI MWAO.
Siku ya leo wala sina mengi msomaji wangu. Naomba umsikilize NASIO FONTAINE na kibao chake Hypocrites anapozungumzia hawa watu watakaokutabasamulia usoni ilhali wanatafuta namna ya kukuondoa katika mfumo wako wa maisha.
**Them, I & Them ni kipengele kikujiacho kila Ijumaa kinachoelezea kazi za wasanii (Them) kulingana na maono yangu (I) kwa ajili na manufaa ya hadhira (Them)**
Kwa nyimbo zaidi ndani ya kipengele hiki bofya hapa.
IJUMAA NJEMA

Thursday, July 29, 2010

"HAKUNA KAZI BORA KAMA UZAZI NA MALEZI"

Maneno haya yalisemwa naye Dr Ben Carson alipokuwa akimzungumzia mamake.
Tarehe 5 Aprili mwaka jana niliandika makala yenye kichwa cha habari Ni mbegu ndogo iletayo mazao makubwa (irejee hapa)
Na habari hiyo iliyomhusu Daktari bingwa wa upasuaji ulimwenguni Dr Benjamin Carson. Katika makala hiyo, nilieleza kile nilichosikia na kusoma katika toleo la kipengele cha THIS I BELIEVE kipindi cha Morning Edition kirushwacho na Radio ya jamii hapa Marekani ya NPR. Unaweza kusikiliza alichokisema katika kipindi hicho kwa ku-bofya hapa.
Lakini bado nilikuwa miezi kadhaa kabla nami sijawa mhanga wa kazi ama shughuli hii nzuri ya ulezi.
Licha ya kuwa mlelewa na kuona njia njema za malezi toka kwa wazazi na walezi wangu, haikuwa sawasawa mpaka nami nilipoingia jukumu lisilo la hiari la ulezi. Na hapo ndipo nilipoona uzuri, ugumu na ama umuhimu wa malezi bora kwa yule umleaye.
Nakumbuka katika Salaam zangu za siku ya kinamama duniani (hapa) niligusia umuhimu wa kinamama. Nimelikumbuka hili hivi majuzi wakati nawasiliana na Kakangu Kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa kumpongeza kwa kupata mwana. Na kisha nikapitia kwenye kijiwe chake kusoma toleo la ujio wa mwanawe huyo na moja kati ya sentensi alizoandika katika taarifa ya ujio wa mtoto ni ile aliyomalizia nayo akisema "nilianza kumheshimu mwanamke toka zamani ila hii inaongezea heshima kwa mwanamke" Natambua malezi si ya mwanamke pekee lakini kama Kakangu Kamala na hata mimi mwenyewe tunaweza kuongeza heshima na thamani ya wanawake kwa kile wanachotubariki nacho, ina maana tunaongeza mapenzi na msaada kwao na kujishughulisha zaidi katika malezi. Ina maana kwa kuamua kumuona mwanamke kwa namna iliyo bora zaidi, tunaongeza msaada wa malezi kwao na kuboresha malezi kwa mtoto.
Wapo waliotangulia wakasema "harder the battle, tougher the fight, sweeter the victory". Na naamini mchakato mzima wa malezi ndio UTAMU WAKE na kwa waliofanikisha suala la malezi wanaweza kuamini kuwa katika KUWEKEZA KWENYE MALEZI, TUNASAIDIA KUKUZA MWANA NA KIJANA / BINTI ALIYE MWEMA AMBAYE NDIYE ATAKAYEKUJA KUWA MSAADA KWA JAMII.
Na kwa kuwa wanajamii wote wanaanzia utotoni, basi lazima tujue kuwa UZAZI NA MALEZI ni KAZI BORA ZAIDI na ni msaada mkubwa kwa jamii ijayo.
WAKATI NAMKARIBISHA RASMI KAKA KAMALA KATIKA ULIMWENGU WA MALEZI, Naomba uungane naye kusikiliza kibao hiki mwanana cha Darius Rucker kuhusu makuzi na malezi na yanavyopita. Anaonesha ama kueleza namna ambavyo kile tunachoona ni karaha katika malezi ya sasa tutakavyokumbuka baada ya muda mfupi. Na hili ni jingine linalofanya MALEZI KUWA KAZI BORA SAANA MAISHANI

He didn't have to wake up
He'd been up all night
Layin’ there in bed listenin’
To his new born baby cry
He makes a pot of coffee
He splashes water on his face
His wife gives him a kiss and says
It gonna be OK

It won’t be like this for long
One day we'll look back laughin’
At the week we brought her home
This phase is gonna fly by
So baby just hold on
‘Cause it won't be like this for long

Four years later ‘bout 4:30
She's crawling in their bed
And when he drops her off at preschool
She's clinging to his leg
The teacher peels her off of him
He says what can I do
She says now don't you worry
This’ll only last a week or two

It won’t be like this for long
One day soon you'll drop her off
And she won’t even know you're gone
This phase is gonna fly by
If you can just hold on
It won’t be like this for long

Some day soon she'll be a teenager
And at times he'll think she hates him
Then he'll walk her down the aisle
And he'll raise her veil
But right now she's up and cryin’
And the truth is that he don't mind
As he kisses her good night
And she says her prayers

He lays down there beside her
‘Til her eyes are finally closed
And just watchin’ her it breaks his heart
Cause he already knows

It won’t be like this for long
One day soon that little girl is gonna be
All grown up and gone
Yeah, this phase is gonna fly by
So, he's tryin’ to hold on

‘Cause it won’t be like this for long

It won’t be like this for long

It won’t be like this for long

Tuesday, July 27, 2010

Miaka 9 baada ya wimbo wake........ JAMII IKO PALE PALE

Ulipotoka kwa mara ya kwanza niliufurahia kwa kuwa ulikuwa ukifurahisha. Kisha nikausikiliza tena na tena na kuangalia hali halisi ya jamii yetu. Na kwa kuwa ilikuwa ni mwaka mmoja tu baada ya uchaguzi, wengi waliuchukulia kama kibwagizo cha kusindikiza kile kilichotokea 2001. LAKINI SI KWELI.
Aliimba kile ambacho kilikuwa, kimekuwa na nategemea kuwa KITAENDELEA KUWA TATIZO katika suala zima la mchakato wa maendeleo yetu waTanzania kwa kuwa tunapuuza ilipo asili ya mchakato huo ambapo ni kwenye uchaguzi. Ikiwa ni miaka 9 sasa tangu msanii Joseph Haule atoe wimbo wake aliouita NDIO MZEE ambao ulipatikana katika albamu ya MACHOZI, JASHO NA DAMU, bado jamii ya Tanzania inaendelea kuishi katika matatizo na kupitia katika hali mbaya ya kimaisha kana kwamba hakuna ambaye ameshaliona, kulionya na kueleza namna ya kutatua jamii.
Wimbo huu ambao umeeleza kwa namna ya USAHIHI maongezi na ahadi nyingi zisizotimilika za wanasiasa na maitikio ya wananchi yasiyojali kusikia kisemwacho na mwanasiasa huyo, unaonekana kupuuzwa hata sasa ambako UONGO huu umeanza kushamiri tunapoelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba.
Wimbo wake huu kwa kiasi kikubwa umezungumzia namna ambavyo waTanzania wengi HAWAJUI KILE WAHITAJICHO na matokeo yake kupokea kila kisemwacho ama kutamkwa na "mzee" ambaye anaaminika kiasi kwamba kila asemacho wao wanakubali. Sina hakika kama mmesikia nililolisoma kwa Dadangu Subi kule fesibuku kuhusu "Mgombea mmoja wa Ubunge kwa tiketi ya CCM huko Iringa anasema akipata Ubunge atawanunulia wananchi nyavu za kuvulia samaki il hali eneo hilo ni la mwinuko na milimani kusikokuwa hata na mto, wachilia mbali ziwa au bahari!" Ninaloweza kufikiria ni namna ambavyo wananchi walivyoshangilia na kuona kama shida zao zimekwisha ilhali wanasahau kuwa hazitakwisha kwani hazipo.
Na sasa ni mwaka mwingine wa UCHAGUZI. Mwaka ambao kila mtu anakuwa muongeaji na kila mmoja ni mzalendo. Kila mtu anaipenda nchi na kuja na sera zake "disposable" na watu bila kujua wataendelea kuimba NDIO MZEE.
Natamani kama wagombea wangekuwa wanasema kile walicho na uwezo.
Natamani kama wananchi wangekuwa wanauliza na kujiuliza yale wapasayo kujiuliza./
Natamani kama waandishi wangetanguliza mbele taaluma na kuhoji kisemwacho kuliko kuripoti
Natamani kama kungekuwa na utaratibu wa kutunza rekodi ya kisemwacho na kuhakikisha mwisho wa muhula waliosema "wanarejesha hesabu"
Natamani tusingekuwa tunachagua viongozi ambao meisho wamuhula ndio wanatuambia kuwa walitumia muhula huo KUJIFUNZA WANACHOHITAJI KUFANYA na bado hakuna anayewawajibisha kwa kuahidi wasichoweza
Natamani kama safari hii wagombeao wangetueleza ambavyo wamefanya katika miaka 5 iliyopita na namna ambavyo wanaamini uwepo wao katika nafasi wanazogombea unavyoweza kuleta mabadiliko endelevu.
NATAMANI KAMA MWAKA HUU, WANANCHI WASINGEKUWA WAITIKIAJI WA KILE KITIKIO CHA NDIO MZEE
Joseph Haule ama Prof Jay akishirikiana na Lady Jay Dee, Babu Ayubu na Juma Nature wameweza kueleza kwa namna ya pekee ambavyo jamii imekuwa "waitikiaji" wasiofikiri.
Albamu hii ya MACHOZI JASHO NA DAMU (ambayo binafsi naamini kuwa moja ya albamu bora zaidi kupata kutoka katika muziki huu nchini Tanzania) imesheheni mengi, imeonesha ujuzi na utambuzi wa Prof Jay na kuiainishia jamii mengi ambayo miaka 9 baadae, hakuna mabadiliko. Ni uwezo huu ulio/ unaomfanya Prof Jay kukubalika ndani na nje ya nchi (kwa jamii zisikiazo kiSwahili) na pia kumuwezesha kupata tuzo nyingi tu.Picha kwa hisani ya Bongo Star Link Blog<>
Naomba USIKILIZE KWA MAKINI kibao hiki NDIO MZEE na tafakari kuleee jamii yetu ielekeako sasa hasa wakati huu wa uchaguzi

TUONANE "Next Ijayo"
Uchaguzi Tanzania ni "label" inayozungumzia namna niionavyo nchi yangu ya Tanzania ijiandaavyo na uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2010. Kwa maandishi mengine juu ya mada hii katika "label" hii BOFYA HAPA

Uchaguzi Tanzania ni "label" inayozungumzia namna niionavyo nchi yangu ya Tanzania ijiandaavyo na uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2010. Kwa maandishi mengine juu ya mada hii katika "label" hii BOFYA HAPA

Friday, July 23, 2010

Them, I & Them... YOUTH TODAY......Morgan Heitage

Japo si kawaida yangu kufuatisha nyimbo za msanii, bendi ama kikundi kimoja, kuna wakati ambapo uhitaji wa uoanishaji wa matukio unalazimisha hili kutokea. Na kwa wakati huu, hili la wakati kuongoza tukio ndilo lililotokea. Tunarejea tena kwa Royal Family of Reggae, The Morgan Heritage.
Nimekumbuka kurejea maelezo na mahusiani ya maudhui ya kibao hiki na maisha yetu ya sasa baada ya kuonjeshwa na kusoma kwa umakini makala makini kwenye tovuti ya VIJANAFM.COM yenye kichwa cha habari Vijana wa Tanzania tuamke!(ipitie hapa). Nimesema MAKALA MAKINI na pengine ambayo kila kijana wa kiTanzania anastahili kuisoma na pengine kuuchukia ukweli wake ili aweze kuwa sehemu ya badiliko lihitajikalo.
Ndugu watano (Nyuma L-R) Lukes, Gramps, Jah Petes (Mbele L-R) Dada yao Una na Mr Mojo Morgan wanaounda kundi zima la Morgan Heritage a.k.a ROCKAZ. Watembelee HAPA
Nimekuwa nikisema kuwa MPAKA KESHO ITAKAPOHESABIKA KUWA LEO, BASI VIJANA HATUTAENDELEA. Maana kubwa ya sentensi yangu ni kuwa mambo ya msemo wa VIJANA NI TAIFA LA KESHO hauna maana.
Hauna maana kwangu kwa kuwa wazee wanaendelea kung'ang'ania madaraka mpaka vijana wanapoelekea kuuacha ujana na wakati huo ndipo tunapojikuta tumekosa la kufanya. Hakuna ubishi kuwa wazee wengi na hasa kwenye siasa za nyumbani wana uzoefu, lakini tusisahau kuwa "The trouble with experience is that by the time you have it you are too old to take advantage of it. " — Jimmy Connors
Ndio maana twaona namna ambavyo "wazee" wetu waliojikita kwenye siasa walivyoishiwa na kuanza kutetea yasiyo na maana na yasiyo na tija kwa taifa.
Ni wakati wa VIJANA KUAMKA NA KUANZA KUNYOOSHA MAPITO ya maumivu tunayopitishwa na "waheshimiwa" hawa.
Twaona ilivyo nchini kwetu na Afrika kwa ujumla jinsi vijana wanavyohangaika kwelikweli kutaka "kuiona kesho". Katika hili, tunawasikia Morgan Heritage katika wimbo wao YOUTH TODAY wakilizungumzia hili. Mfano ni hapa mwanzo ambapo Jah Petes anaimba namna ambavyo tunashuhudia yaendeleayo kuwakumba na kuwaathiri vijana bila kutafuta suluhisho anaposema "How much more do we need to see before we realize we all need to change our lives. For the better world in this time. Now the time has come, let's not wait till it's gone. Don't wait too long". Lakini Gramps katika ubeti wa pili anazungumzia maumivu / mateso ambayo vijana wanayapata kwa maamuzi ambayo hawakushiriki kuyafanya na kisha anahimiza kuwa hakuna wa kulamu bali kuamua na kuungana kuyafanyia kazi mabadiliko. Anasema "now the youth they feel the pain, for the choices made yesterday, there's no one out to blame we all have to work towards the change"
Basi ni wakati ambao lazima VIJANA TUAMKE na kuacha kutegemea waliopitiliza kwenye nafasi ambazo hawana uwezo wa kuzishikilia. Wanatapatapa na kuhaha na sssi (bila kujijua) tunatapatapa tukiwafuata wao. Hivi unajua athari ya kumfuata asiyejua aendako? Unajua anakoweza kukufikisha kama utaendelea kumfuata ilhali yeye anaendelea kukukimbia na kutafuta pa kujificha? Tunapowaona wao kama "milima" ilhali milima inatafuta bonde la kujificha (kwa kuwa wameshaishiwa) basi ujue TUNAAIBIKA. Ndio anayofungia nayo Jah Petes anaposema
"see someone looks a hills to run to,
the youths a look somewhere to run to,
see someone looks around to run to,
the ROCKAZ looks somewhere to run to,
see someone looks a mountain top to run to, the mountain looks somewhere to run to
See someone run out of space, what a big disgrace"
Nikiwa na Gramps wakati wa Mission In Progress tour (2008)
Wasikilize Morgan Heritage hapa katika kibao chao mwanana YOUTH TODAY kipatikanacho katika albamu yao waliyoiita MISSION IN PROGRESS

**Them, I & Them ni kipengele kikujiacho kila Ijumaa kinachoelezea kazi za wasanii (Them) kulingana na maono yangu (I) kwa ajili na manufaa ya hadhira (Them)**
Kwa nyimbo zaidi ndani ya kipengele hiki bofya hapa.
IJUMAA NJEMA

Thursday, July 22, 2010

Tuwaombao wanabana, sisi je? Kuna ajifunzaye???

Novemba 26 2009 niliandika bandiko lenye kichwa cha habari Nalinganisha majengo na uchumi wetu (irejee hapa) nikionesha tofauti kati ya bunge la Uingereza na Bunge letu. Nikaangalia muonekano na KIPATO cha nchi hizi na nikaishia kujiuliza maswali hayo.
Jana na leo kumekuwa na habari nyingine iliyonifanya nirejee kujiuliza kuhusu JUHUDI ZA WAHISANI WETU ukilinganisha na za kwetu.
Hivi karibuni tumesikia kuhusu nyongeza ya mishahara huko Kenya imfanyayo Waziri Mkuu kuondoka na zaidi ya theluthi ya pesa anazopata Waziri Mkuu wa Uingereza na pia asilimia kadhaa zaidi ya mshahara wa Rais wa Marekani.
Waziri Mkuu wa Uingereza Mhe David Cameron
Waziri Mkuu wa Uingereza Mhe David Cameron ambaye aliingia madarakani na kuanza kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya serikali. Aliahidi kufanya hivyo kwa vitendo baada ya kuamrisha kutoongezwa mshahara kwa baadhi ya watumishi.
Na wiki hii, David Cameron ameushangaza ulimwengu pale alipoamua kutotumia ndege ya kukodi wakati akifanya safari yake ya kwanza kubwa kikazi kuja hapa Washington DC kuonana na Rais Barack Obama. Katika safari hiyo, Waziri Mkuu huyo alitumia ndege ya abiria ya biashara (British Airways) na hivyo kuweza kupunguza matumizi ya zaidi ya $300,000 ambazo zingegharamia usafiri wa kawaida wa kukodi. Kwa mujibu wa Gazeti la The Sun la nchini Uingereza kama ilivyonukuliwa katika bandiko la leo katika Blog ya Jack Cafferty wa CNN, afisa mmoja wa serikali ya Uingereza amesema "When we are asking the country to tighten their belts as much as we are it's very hard to justify hiring big jets to swan around the world. It may make his travel a little harder, but the Prime Minister believes it's up to him to set an example."
Nimeshuhudia baadhi ya msururu wa viongozi wa nchi za Afrika (Tanzania ikiwa mojawapo) na ninawaza kama kuna watakalojifunza sasa.
Natambua Rais mmoja barani Afrika (sina hakika kama ni Zambia) aliamua kusitisha ndege ya Rais kupunguza gharama.
Pengine na sisi Tanzania kama tutafikiria hili na pengine kuongeza utendaji kazi wa MABALOZI ambalo litakata gharama za safari za kila uchao za Rais, naamini tunaweza kubaki na vi-senti vya kuchimbisha visima kadhaa vya maji kwa wananchi wanaohitaji saana, kujenga tu-vituo twa afya na mengine mengi.
Kwa ufupi ni kuwa TUACHE KUTUMBUA KULIKO WANAOTUWEZESHA KUWA NA MATUMBUZI HAYO.

Wednesday, July 21, 2010

Uhiari wetu wa lazima....Tunautumiaje????

Image @ WalkerNews.net
Haya sasa. Huu ndio wakati muafaka wa kuelekea UWEKEZAJI wa maisha na maendeleo ya waTanzania na Tanzania kwa ujumla. Wakati wa UCHAGUZI. Wakati ambao wananchi wanaelezwa mengi kuliko wanavyoweza kuelewa na pengine kupelekwa kwingi kuliko wanakoweza kwenda.
Wanawazishwa mengi kuliko uwezo wa fikra zao na kutamanishwa meengi kuliko uwezo wao wa kupatiwa.
NI WAKATI AMBAO WANACHAGUA WALE WATAKAOCHUKUA DHAMANA YA MAISHA YAO NA NCHI YAO.
Lakini ni nani mwenye mwajibu wa kumuelimisha mTanzania wa kawaida juu ya Ukweli vs Uongo usemwao? Ni nani wa kumuamsha mTanzania kuwaza na kuuliza maswali muhimu kwa ajili ya kupata njia sahihi za kutatua matatizo yao?
Niliwahi kuuliza kuwa YAKO WAPI MAHITAJI YA WAHITAJI? (irejee hapa) na nia hasa ilikuwa kuwaamsha wale wanaoongoza vyama na mashirikisho ya WAHITAJI kuandaa maswali na mikakati mbalimbali. Mpaka sasa sijasikia lolote toka kokote kuhusu mikakati ya "kuwabana" wagombea juu ya haki za WAHITAJI.
Sasa ninashuhudia UTITIRI wa wagombea kwenye mabandiko mbalimbali, nawaza AZMA ya kuwaweka bila kuwaeleza kwa kina. Kila siku twaona "blah blah blah atangaza nia" na baada ya hapo twaona blogu na tovuti nyingi zikiishia hapo na kutoeleza nia ya huyo mgombea kufanya hivyo. Hatuelezwi historia na uzoefu wake kikazi na kiutawala na mara chache tumeelezwa undani wa nia ya mgombea na kufaulu na kufeli kwake.
Labda tuanze kuwa KUTHAMINI NA KUTAMBUA UMUHIMU WA NJIA HII YA UPASHANAJI HABARI AMBAYO NI HIARI.
Na japo ni ya hiari, bado ina ulazima katika kuitekeleza kwa ufanisi. Hatutaki kurejea yaletale niliyoandika juu ya Tanzania Yangu.. Yenye vyombo vingi vya habari visivyo na habari zaidi ya taarifa (irejee hapa). Ni wakati wa blogu na tovuti zetu kuacha KUTAARIFU JUU YA WAGOMBEA na kuanza KUTUHABARISHA JUU YAO.
Natambua na kuheshimu ukweli kwamba ku-blogu ni hiari, lakini katika kuelimisha umma juu ya maamuzi muhimu kama UCHAGUZI ujao, basi ELIMU HII INA ULAZIMA.
Tuonane Next Ijayo

Uchaguzi Tanzania ni "label" inayozungumzia namna niionavyo nchi yangu ya Tanzania ijiandaavyo na uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2010. Kwa maandishi mengine juu ya mada hii katika "label" hii BOFYA HAPA

Monday, July 19, 2010

Za Kale vs Maisha ya Sasa...TOP QUEEN

Ukianza kutafuta SIFA mbalimbali ambazo anaweza kuwa nazo mtu udhaniaye ndiye chaguo lako, unaweza kushangazwa na kile utakachogundua.
Lakini kawaida ya wengi huwa twasubiri mtu mwingine atuambie sifa ya yule tunayempenda. Ina maana hatuzioni na hata tukiambiwa hatuonekani kuzithamini. Na ndio maana hata mwenye mke ama mwenye mwenye busara na upendo wa dhati (hasa kwa mazingira ya nyumbani) anaweza kuamka na kuondoka na kurejea na kuelekea kulala bila hata kumwambia ama kudhihirisha BARAKA aliyonayo kuwa na mume ama mke mwenye busara na upendo.
Kama walivyoimba Vijana Jazz kwenye wimbo wao, wamesema "hapa ulimwenguni kila binadamu Mungu kamuumba kwa sifa zake". Na huu ndio ukweli wa mambo. Lakini pia kulingana na maisha yetu, na pengine mahitaji ya nyoyo zetu, tunajikuta tuna mahitaji tofauti. Na ni kwa wale wajao na suluhisho la mahitaji yetu wanaokuwa na nafasi ya kipekee kwetu. Vijana Jazz kwenye wimbo Top Queen wamemueleza Regina (ambaye ndiye aliyeimbwa kama Top Queen) kuwa uzuri wake "..tabia njema na busara zake......zimefanya wazazi waheshimu maamuzi yake".
Na hili la kuwa na maamuzi ya busara linazidi kujidhihirisha pale ambapo aliamua kuwaweka kando wale waliokuja na magari ya fahari, pesa nyingi, waliokuja na nguo za kuazima na wenye kujionesha na kuishia kuolewa na MFUGA BATA ambaye hali yake kimaisha (naamini kulingana na wale waliomtangulia "kurusha karata" imetajwa kama HOHEHAHE.
Yes!!! Ni mimi na TOP QUEEN wangu.
Na hawa wenye fikra na mitazamo hii myema wako wengi ulimwengu wa sasa. Well!!! Nami ni mmoja wa walionufaika na TOP QUEEN wangu. Busara nyingi zilizotajwa kuwemo ama kuwa nazo Top Queen aliyeimbwa na Vijana Jazz amekuwa nazo. Na hii ndiyo sababu inayonifanya niamini NYIMBO HIZI ZIKINGALI NA MAANA MPAKA LEO.
Sikiliza wimbo huu Top Queen toka kwao Vijana Jazz Band uburudike na kuelimika.

** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia kila Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama mtandao shirika hapa**

Friday, July 16, 2010

Them, I & Them........POLITICIAN.....Morgan Heritage

Kundi zima la Morgan Heritage liundwalo na ndugu watano.
Ni siku 5 tu zimepita tangu kumalizika kwa michuano ya soka ya Kombe la Dunia ambayo ilifanyika na kufana huko nchini Afrika ya Kusini. Na kumalizika kwa michuano hiyo kwa baadhi ya "wafaidi kuangalia" kunamaanisha kuwa ni mwisho wa mchakato mzima na sasa wanasubiri "kufaidi" mwaka 2014. Lakini kwa waliokuwa wamewekeza na kuhitaji matokeo yaliyo sahihi, WAMEFANYIA KAZI MATOKEO YOTE.
Kwa waliopoteza mechi kizembe ama kijinga wamewajibishwa. Ina maana Makocha, Wachezaji ama Viongozi vya vyama ama mashirikisho ya soka nchini mwao wamewajibishwa kwa adhabu mbalimbali. Wengine kwa hiari yao wenyewe wakaamua kumwaga manyanga.
Lengo hapa ni KUJIPANGA KWA AJILI YA MICHUANO IJAYO NA KUANGALIA UWEZEKANO WA KUKAMILISHA DHAMIRA NA MALENGO YA NCHI KULITWAA KOMBE HILO
Ninatamani saana kama uwajibishaji wa namna hii ungekuwa unatokea kwenye maisha yetu ya kila siku. Maisha ya kisiasa na kitawala nchini Tanzania. Yaani tunapoelekea mwisho wa "kombe la urais na ubunge", tuangalie ni nani na nani wamefanya nini. Kisha tuangalie kama kuna anayestahili kuwajibishwa. Tuangalie ni "timu gani" tunayohitaji kuwa nayo ili kutuwezesha kulitwaa KOMBE LA MAENDELEO kwa wananchi katika fainali zianzazo mwishoni mwa mwaka huu mpaka mwaka 2015.
Kwa wale ambao hawakuwa na msaada kwetu, walioshindwa kutumia rasilimali zilizopo, walioshindwa kuhimiza nguvukazi kuendeleza maeneo watokako, waliohamia nje ya majimbo yao na kuendekeza biashara na kujirundikia pesa, wasiotetea wananchi wao na ambao kwa namna moja ama nyingine wameshindwa kutekeleza kile walichoahidi kukifanya mwaka 2005, TUWAENGUE.
Lakini pia tukumbuke kuwa kumekuwa na mengi ya kukwamisha mambo kutimia, lakini cha kuangalia ni namna gani wamejitahidi kutimiza malengo na ni kwa kiasi gani mambo yaliyo nje ya uwezo wao (kama mtikisiko wa uchumi uliokumba dunia) vimechangia kuwakwamisha.
Kwa ujumla tuwe makini katika kuchagua. Tujiulize waliyojiuliza MORGAN HERITAGE katika wimbo wao POLITICIAN waliposema "why should we trust in politicians, and why should we vote every elections. When there's no place for we (you and me) in their secret society. They call us minorities".
Hakuna haja ya kuendelea kuchagua uozo ambao unaendelea kututafuna na kutumalizia maliasili. Wenye kuongeza gharama za malipo na posho ilhali hawana suluhisho lolote katika kutatua matatizo ambayo WAMEYAONA, WAMEYAKIRI, WAMEYATANABAISHA KUWA YANATATULIKA NA KIKUBWA ZAIDI WAMEAHIDI KUYATATUA
Nikiwa na kiongozi wa uimbaji (lead singer) wa kundi hilo Peter Morgan (2008)
Sikiliza kibao chao hiki POLITICIAN kilichomo kwenye albamu yao MISSION IN PROGRESS uburudike na kujifunza pia.

**Them, I & Them ni kipengele kikujiacho kila Ijumaa kinachoelezea kazi za wasanii (Them) kulingana na maono yangu (I) kwa ajili na manufaa ya hadhira (Them)**
Kwa nyimbo zaidi ndani ya kipengele hiki bofya hapa.
IJUMAA NJEMA

Thursday, July 15, 2010

Maalum kwa WAGOMBEA WETU 2010

"Jamaica is a paradise, but for those who were born and raised there is a struggle" Haya ni maneno yalitosemwa / yanayosemwa naye Peter Morgan wa kundi la Morgan Heritage kuhusu vile ambavyo JAMAICA huonekana machoni ama kusikika masikioni mwa watalii ukilinganisha na hali halisi ya maisha ya wazawa wa nchi hiyo. HILI HALINA TOFAUTI NA NCHI YANGU TANZANIA.
Kwa kumbukumbu tuu, ni kuwa huu ni MWAKA WA UCHAGUZI. Mwaka tuonao TABASAMU toka kwa wanasiasa kuliko wakati mwingine wowote ule. Wakati ambao hata mtoto ambaye hajabahatika kuoga kwa siku kadhaa, anapata "kumbatio na busu" toka kwa wagombea. Wakati ambao wagombea hawachoki kupunga mikono na kusalimia watu.
Kwa ufupi, ni WAKATI AMBAO WANASIASA WANAKUWA WANAFIKI KULIKO WAKATI MWINGINE WOWOTE ili kuweza kujipatia kura watakazo.
Lakini kabla hawajaingia kwenye "viwanja" na kuanza KUDANGANYA, napenda kuwakumbusha yale yaendeleayo ndani ya majimbo na nchi yao.
Yaani nawaomba watazame kile kilichopo "ndani" ya majimbo yao. Na hizi zifuatazo ni baadhi ya taswira nilizozikusanya toka katika blogu na tovuti mbalimbali ambazo zaonesha hali inayohitaji kutendewa kazi ama kuboreshwa.
TUANZE NA SEKTA YA AFYA
KISHA SEKTA YA ELIMU Hapa chini ni maliwato ya shule hukoooo Lindi. Hii shule imekuwa na maliwato ya hivi kwa miaka 35
Hili hapa chini ni jengo la bweni katika shule ya sekondari huko Tanga TUHAMIE SEKTA YA MIUNDOMBINU:
LABDA TUCHUNGULIE KWENYE UWEKEZAJI
NB: Picha zote ni mali ya blog na tovuti mbalimbali. Si mali ya Blog ya Changamotoyetu Blog

Uchaguzi Tanzania ni "label" inayozungumzia namna niionavyo nchi yangu ya Tanzania ijiandaavyo na uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2010. Kwa maandishi mengine juu ya mada hii katika "label" hii BOFYA HAPA

Wednesday, July 14, 2010

Tanzania yangu.......Isiyojua kuziba ufa, wala kujenga ukuta

Image Credit: SECURE CHANNEL
Alhamis ya Januari 14 niliandika bandiko Niangaliapo HAITI naiona TANZANIA (irejee hapa) nikihusisha niliyoyaona HAITI wakati na baada ya tetemeko na nilivyokuwa nikiichungulia nchi yangu TANZANIA. Nikaangalia MAANDALIZI ya nchi yangu katika majanga ya asili na yale tusababishayo na namna ambavyo tunajitahidi kuyazuia ama kukarabati pale tulipochelewa. Sehemu ya bandiko hilo niliandika nikisema
"Tukumbuke kuwa Tanzania (na hasa Dar Es Salaam) iko katika hatihati ya kukumbwa na athari za ongezeko la kina cha maji na ilionja athari za Tsunami japo haikuwa na madhara. Sasa nawaza................
Hivyo "vikwangua anga" ninavyosikia "vinaota" kila siku vimejengwa kuweza kuhimili matetemeko ya ardhi ama ndio mwendo wa "kitu kidogo" tusonge? Na ziliishia wapi tetesi za kupinda kwa jengo la Mafuta House? Ni kweli kuwa majengo yote yanayojengwa sasa jijini ni salama na yanafikia kiwango cha kuhimili athari kama haya?
Kwa mji kama Dar Es Salaam, kuna urahisi gani wa waokozi kuwafikia watakaokuwa matatizoni iwapo litatokea? Kama majengo ndio haya (ambayo ubora wake hatuujui) na barabara hazipanuliwi wala kuboresha mfumo wa usafiri wa ardhini, ni vipi tunajiandaa kiuokozi kwa matatizo yasiyoepukika kama hili lililotokea Haiti?
"
Japo sijasikia tamko lolote kuhusu mambo ambayo niliwahi kuzungumzia (na pengine sikutegemea kusikia lolote kwa kuwa hakuna anayejali), lakini bado nawaza kama yale tuyaonayo yakitendwa ama kupangwa na serikali yana mipango ya kuzuia ama kutatua tatizo.
Kila wakati nasikia MISAADA YA VYANDARUA IMETOLEWA kwa ajili ya kujikinga na mbu ambao wameachwa kuzaliana, na bado twajua kuwa misaada hiyo yaweza kuwa aghali kuliko gharama za kuua mazalia ya mbu. Nawaza ni kipi kilicho chema zaidi? Kukinga mbu wasizaliane ama kuzuia mbu waliozaliana wakati wa kulala ilhali wanaendelea kutuuma tunapoenda "kuchanja kuni" ama tutumiapo vyandarua hivyo kimakosa?
Tatizo nilionalo hapa ni kuwa MBU HAWAZUIWI KUZALIWA na hata juhudi za kuwazuia waliozaliana wasidhuru watu si halisi.
Niliwahi kuandika juu ya Tanzania Yangu.... Ijengayo Ghorofa ikipuuza msingi (irejee hapa) ambamo humo nilishangazwa na utaratibu wa kiutawala wa nchi yangu ambao hauoneshi kujali CHANZO CHA TATIZO zaidi ya kulipuuza na kisha kuweza hata kupuuza TATIZO LENYEWE.
Image: NYDaily News.com
Na sasa naangalia sakata la uchafuzi wa Ghuba ya Mexico hukooo kusini ya Marekani na nawaza kuhusu pwani zetu. Nawaza wenye dhamana za kuziweka salama na utendaji wao wa kazi. Nimewaza "mnuko" ninaousikia katika fukwe za nyumbani kama ni UCHAFU unaiathiri bahari ama ni nini. Na nawaza zile tetesi za "taka zimwagwazo baharini" na kisha naangalia kama kuna anayehusika kutambua MADHARA YA MUDA MREFU YA UCHAFU HUO na pia kuangalia namna ya kuzuia sasa. Nawaza kama kuna taasisi inayoshugulikia USALAMA NA UBORA WA MAJI NA FUKWE kwa manufaa ya wananchi.
Ni nini chahitajika kufanyika kuhakikisha kuwa TUNAJIFUNZA KUZUIA MAJANGA na pia pale pawezekanapo KUYATATUA?
Naiwaza Tanzania Yangu katika harakati nzima za kuzuia na kutatua.
Iwe ni kuzuia ukosefu wa ajira, RUSHWA, UFISADI na hata USALAMA WA WATU KUTOKANA NA UWEKEZAJI KAMA HUU na hata malipo kwa waathirika. Na licha ya hayo yote, hatuoni HARAKATI ZA KUREKEBISHA MAKOSA YALIYOTOKEA.
Hivi majuzi SERIKALI IMETANGAZA KUWA MAJI YA KWENYE MTO ULIOATHIRI WATU YAKO SALAMA KWA MATUMIZI YA BINADAMU (bofya hapa kujisomea)

Na hili lanifanya niiwaze TANZANIA YANGU..... ISIYOJUA KUZIBA UFA, WALA KUJENGA UKUTA

Tanzania Yangu ni kipengele kinachozungumzia ytale yaendeleayo nchini Tanzania na namna ambavyo "ndivyo sivyo" inavyozidi kupamba moto nchini. Kwa matoleo yaliyotangulia BOFYA HAPA


Tuonane "Next Ijayo"

Sunday, July 11, 2010

REKODI ZAVUNJWA.........

Lakini uvunjwaji wake wanifanya niwaze kama kuna ulazima wa kujaribu?
Wazivunjao WANAWAZA NINI?
Labda tuanze INDONESIA ambapo kumekuwa na habari ya huyu "MTOTO" ambaye aonekana kuwa mdogo zaidi kumudu uvutaji wa sigara.
Nawaza kinachomfanya avute, alivyoanza, anayemuwezesha kuzipata na hata uvutaji wake unapofanyika kama hakuna waonao haya. Na nawaza kuwa kama anaweza kuvuta kwa "ufundi" kwa namna hii, amekuwa akivuta kwa muda gani? Na kama ana miaka miwili, na aligunduliwa na wazazi wake akiwa na miezi 11, alianza lini na alianzishwaje na nani??
Nawaza tuu kuwa kwa kufikia hivi waliomzunguka WANAWAZA NINI?

Na pia niangaliapo HAWA walioingia kwenye kitabu cha MAAJABU ya dunia, WANAWAZA NINI?

Tuhamie huko uCHINA aliyeamua kuvunja rekodi ya KUVUKA NA KAMBA. Nawaza ALIWAZA NINI na waliomuacha ajaribu waliamini vipi kwamba atamaliza na kuvunja rekodi na sio "kifo kitarajiwa?
Itazame hii HAPA
NAWAZA KAMA REKODI NI LAZIMA ZIVUNJWE NA KAMA KILA IVUNJWAYO YAVUNJWA BILA "UTATA" NA "HATARI?
***"Waliwaza nini ni kipengele cha kuelimishana tukifurahia. Hiki kitakuwa kikikuletea habari za kweli na kushangaza kuhusu watu ambao wamefanya yale ambayo unaweza kujiuliza kuwa WALIWAZA NINI? wakati wanatenda haya.
Kitakuwa na habari fupifupi kutoka ulimwenguni kote. Kwa habari zaidi kuhusu kipengele hiki
BOFYA HAPA"***

Friday, July 9, 2010

Them, I & Them....CRY NO MORE.....Beres Hammond

Hali ya maisha ilivyo sasa ULIMWENGUNI imemuathiri takribani kila mmoja. Wengi wamepoteza kazi, wengi wamepoteza ndugu ambao kwa msongo wa mawazo na kukata tamaa wameamua kukatisha maisha yao (na wengine ya wenzi na familia zao) na wengine kuteteresha afya zao kwa kuwaza kuliko wanavyoweza kuwa suluhisho.
Nami kama wengine niliwaza na kuwazua lakini nikagundua kuwa kuna baadhi ya mambo ambayo kuwaza na kufikiri hakutayabadili, bali cha kufanya ni kubadili mfumo wa maisha ulio tegemezi kwayo na kuishi bila kutegemea saaana uwepo wa hayo. Mfumo huu mpya wa maisha una msaada sana kwa sasa hasa kwa yeyote ambaye hana lolote analoweza kufanya kubadili uhalisia wa maisha ya sasa. Baadhi ya mambo hata ukiwaza na kujikwaza hayatabadilika kwa sasa, mfano kuwaza kazi / ajira wakati hakuna anayeajiri, kuwaza nyongeza ya mshahara wakati waajiri wanapunguza watu kazi, kuwaza kuongeza wateja katika biashara wakati wanunuzi wanaishi kwa kuomba na kwa msaada wa serikali, kuwaza pesa mara mbili ya mshahara ilhali unajua halitakoea. Jawabu nililopata naamini ni muafaka kuwa TWAHITAJI KUISHI KAMA TULIVYO NA KUJITAHIDI KUTENGENEZA NAFASI NJEMA YA MAISHA TULIYOPO KULIKO KUENDELEA KUOTA YASIYOWEZEKANA KUTENDEKA SASA. Kwa kifupi twatakiwa kuishi kwa namna tulivyo na si tutakavyo. Kama alivyosema "mwana mpotevu" kuwa Pa kuanzia ni pale ulipo (Bofya hapa kumsoma)
Niungane naye Beres Hammond katika kibao hiki NO MORE ambapo naye ameeleza alivyoamua kuishi bila hesabu za kile asichonacho.
Sote twaweza na itatupunguzia hali ya kujiona kama walioshindwa kuyakabili maisha kwani tutakuwa tukiishi kwa uhalisia wa maisha ya sasa.
Msikilize hapa Beres Hammond anapoanza kwa kusema
"Am gonna cry no more, i've shed my last tear,
No more worrying about what tommorow bring.I'm gonna live today the best way the best way i will have, and from now on that's how is gonna be...."
pia anaendelea kuimba kuwa
" i'm wont set myself for the worry about what i can't have
i'll have to live without......"


**Them, I & Them ni kipengele kikujiacho kila Ijumaa kinachoelezea kazi za wasanii (Them) kulingana na maono yangu (I) kwa ajili na manufaa ya hadhira (Them)**
Kwa nyimbo zaidi ndani ya kipengele hiki bofya hapa.
IJUMAA NJEMA

Wednesday, July 7, 2010

NI SISI WENYE SULUHISHO LA AFRICA

Mara nyingi tumekuwa tukisaka suluhisho la matatizo ya bara letu ilhali tunasahau wajibu wetu katika kusaka suluhisho hilo. Hapa aktika video hii hapa chini, mwanadada huyu Ory Okolloh anayeendesha blog ya Mzalendo anaeleza namna Afrika tuonwavyo na wengine na uhalali wa kuonwa ama kuonekana hivyo na hata namna tunavyonyanyasana na mwisho ni ni nani wa kusukuma mabadiliko tuyatakayo.
Shukrani kwa Da Mija "aliyenionjesha" hii nilipokuwa adimikoni na sasa naamini ni wakati muafaka wa kushirikiana nanyi video hii.
TAZAMA, SIKILIZA, JIFUNZE



JICHO LA NDANI ni kipengele kinachozungumzia mambo mepesi na yaliyo ndani mwetu, ambayo yakiangaliwa vema na kwa tafsiri ama tafakari njema yanaweza ama ndio suluhisho kwa matatizo yetu. Kwa matoleo yaliyopita katika kipengele hiki, BOFYA HAPA

Tuesday, July 6, 2010

Sajna... Anapomuwaza machinga wa Tanzania ndani ya dk 4:32


Sajna a.k.a Mzee wa Iveta ktk pozi.
"Nilipoungwa" kuutazama wimbo huu na Kaka Sandu George "Kidbway" mtangazaji mahiri wa a Radio Free Africa na mdau mkuu wa Tetemesha Recordz iliyozalisha wimbo huu, niliamua kutulia kutazama na kusikiliza. Kama kawaida, kuhusianisha nionacho na nisikiacho ilikuwa ni sehemu kubwa ya muda wangu huo.
Na kilichonivutia si mpangilio wa ala ama sauti pekee, bali kilichozungumzwa, kilivyozungumzwa na hata kilivyooneshwa.
NI HALI HALISI YA MAISHA YA WAHANGAIKAJI WENGI NCHINI TANZANIA.
Katika wimbo huu aliouita IVETA, Sajna anamuimbia mpenziwe ambaye amemuacha kijijini kwenda mjini kusaka maisha. Ni mfumo wa maisha ambao unawakumba wengi wanaohangaika kuinua hali ya maisha nyumbani watokako. Lakini maisha hayawaendei kama ambavyo huamini yataenda huko mjini. Anakumbana na magumu ya kusaka maisha na bado anamuomba mpenziwe kumsubiri wakati huu anapotafuta yatoshayo kubadili maisha yake na wake mpenzi. Na katika msako huo huo, anapoanza kujisakia maisha kwa mtaji wake mdogo na kuijali familia yake, anakumbana na "askari wa jiji" ambao (kama ilivyo kwa wachuuzi wengi) wanaonekana kumpa wakati mgumu.
Akiwa mjini, Sajna anaeleza namna anavyokumbuka maisha ya kijijini japo hali halisi ya maisha inamlazimu kukaa mjini "kumtafutia dear" wake ambaye anaendelea kumuomba kuwa mwaminifu na mvumilivu ili waje waje kuishi pamoja.
Mbio zake ambazo zilionekana kufanikiwa kumkimbia askari lakini baadae aliishia kunyang'anywa mali na mporaji. Na swali la kujiuliza hapa ni kuwa ni vipi anaweza kumrejea askari (ambaye alitaka kumdhulumu ama kumnyanyasa) ili kuomba msaada wa kurejeshewa mali.

Na yamkutayo SAJNA ndiyo yawakutayo wajasiriamali wengi saana nchini. Na ndani ya dk 4:32 analiangalia tatizo hili na kulionesha kwa undani zaidi.
Jiunge naye hapa chini kwa kumtazama na kumsikiliza katika wimbo wake huu IVETA

Picha kutoka ukurasa wa "ufokitabu" wa SAJNA

Monday, July 5, 2010

Old School Tanzania.......Mwanzo mzuri kuenzi sanaa na wasanii wetu

Kikosi kamili cha Old Skul Tanzania
Februari 18 niliandika kuwa NATAMANI KUONA (bofya hapa kuirejea) na kama naweza kunukuu sehemu kubwa ya toleo hilo niliposema "Nikiwa mpenzi mkubwa wa muziki wa kiTanzania, NATAMANI KUONA kitu ambacho kitakuwa kikitoa mjumuisho wa muziki huo na KUENZI KAZI NA WASANII wa muziki wa Dansi nchini.
Natamani kuona SIKU YA DANSI NCHINI ambayo bendi zitajumuika kuimba nyimbo za wasanii mbalimbali waliochangia kwa kiasi kikuuubwa kuufanya muziki wa Tanzania kuheshimika. Waliotumika kuelimisha, kuburudisha na pia kukamilisha harakati mbalimbali katika jamii.
Natamani kuona tamasha litakalowaenzi nyota wengi wanaoendelea kutuelimisha kwa miaka nenda rudi na pia waliotangulia mbele ya haki...."

Na leo ikiwa ni Jumatatu ya mwisho kabla ya Jula 7, napenda kujumuika na wanaChangamoto wote kuwapongeza wanamuziki wote waliofanikisha kwa namna yoyote uwepo wa onesho hili kubwa la muziki wa dansi liwakutanishalo wasanii wengi wakongwe waliojiita Old School Tanzania mablao lategemewa kufanyika ukumbi wa Karimjee.
Japi sitaweza kuhudhuria, bado nashukuru kuwa KILE AMBACHO NILIKIONA KAMA TAMAA NA AMBACHO NDUGU ZANGU WATOA MAONI WALINIFARIJI KUWA NAWEZA KUONA KIKITOKEA, leo kinamaliziwa.
Shukrani saana kwa washiriki woote waliofanikisha hili na siku ya leo ya Jumatatu ambayo mara nyingi huwa twaweka miziki ya kale, tunajiunga na wapenda burudani woote kupongeza juhudi hizi.
Kwanza pata ufafanuzi wake Waziri Ally kuhusu Old Skul Tanzania.

Na kisha kutazama na kusikiliza mazoezi ya kundi hili hapa chini

PICHA NA VIDEO KWA HISANI YA Michuzi Blog
** Zilipendwa ni kipengele kinachokujia kila Jumatatu kukuletea muziki wa kale kuhusisha na maisha, muziki ama sanaa ya sasa katika nyanja mbalimbali. Unaweza kusikiliza nyimbo nyingine ndani ya kipengele hiki kwa kubofya hapa, ama mitandao shirika hapa** . Ama ili kuweza kujua tasnia nzima ya muziki na wanamuziki wa Tanzania BOFYA HAPA

Friday, July 2, 2010

Them, I & Them......UNITED STATES OF AFRICA.....Innocent Galinoma

The flag of the African Union. 54 stars for each country on the continent, it looks like a flag for the United States of Africa.
"If all Africa should unite, we'll be strong than any nation..... There will be no more WAR, there we'll be no more apartheid....."
Haya ni maneno aliyoanza nayo Innocent Galinoma katika wimbo wake mwanana UNITED STATES OF AMERICA ambao ndio zungumzo letu la leo kuhusisha fikra za msanii na maisha yetu ya sasa.
Mara nyingi katika kipengele hiki huwa naelezea mtazamo ama fikra ama uchambuzi wa nyimbo za wasanii wa Reggae nikihusisha na maisha ya sasa. Lakini wakati huu niliwaza na kuona ni vema nikampa nafasi msanii husika aeleze kwa undani kilichomsukuma kuandika wimbo huu wa UNITED STATES OF AFRICA ambao kila nikiusikiliza naona kama una suluhisho la matatizo mengi japo wenye kustahili kuyaona wanazidi kupuuza ili wanufaike. Kumbuka alivyosema Bob Marley kuwa "see they want to be the star, so they faight the tribal war". Kwa hiyo naamini watawala wanajua chenye uwezo wa kuleta amani, bali wanataka kunufaika na VITA.
Maswali yangu kwa Inno Galinoma ni kuwa
CHANGAMOTO YETU: "Katika Albamu yako KILIMANJARO umeimba nyimbo zenye maswali mengi kwa Afrika na waAfrika (mfano Africans, Kilimanjaro na hata Running). Na katika albamu hiyohiyo umetoa baadhi ya suluhisho ambazo zingeweza kuwa msaada mwema kwa bara letu na waAfrika kwa ujumla kama katika wimbo huu United States of Africa.
Unapoangalia maisha yalivyo sasa ikiwa ni zaidi ya miaka 18 tangu utoe wimbo huo na matatizo uliyoyazungumzia yakingalipo na suluhu ulizoshauri hazionekani kufuatwa japo twajua zingekuwa msaada ama mwisho wa matatizo, UNAJISIKIAJE na hii inaweza kuathiri vipi kuendelea na fani hii?"
Na bila hiyana, Inno alikuwa mwepesi na wa haraka tena mwenye ukarimu kunijibu maswali yangu haya na hii ni sehemu ya majibu yake.
INNOCENT GALINOMA: "nilipotunga na kuimba United States Of Africa ilikuwa ni kama ndoto tu ambayo nilikuwa nayo, na nilidhani labda baada ya ukoloni kwisha na nchi zote za Afrika kuwa huru, ingekua ni rahisi na bora kuungana na kuliita taifa letu moja, kubwa ambalo litajumuisha nchi zote za Afrka. United States Of Afrika ingewezekana kama wote tungekuwa na mawazo sawasawa, lakini unaelewa kuwa hiyo ni ndoto, hata ndugu wa Baba mmoja mara nyingine hawaelewani. Mfano, wakati wa enzi za Mwalimu (Julius Nyerere), (Jommo) Kenyatta, na (Milton) Obote, ilikuwa ni kama mwanzo mzuri, umoja wa East Afrika ungeendelea kukua kwa kuongeza nchi moja moja ambazo zilikuwa na fikra sawa, kwa mfano Zambia, uhusiano wetu nao ulikuwa ni mwema, pamoja na Msumbiji, pamoja na nchi ambazo Tanzania ilijitoa kwa hali na mali na pia damu kwa ajili ya ukombozi wa hizi nchi. Lakini matokeo yake tunayaona leo, nchi nyingine zinajigawa, mfano Eritrea na Ethiopia. Somalia hata serikali inayoeleweka haipo, na hata kwetu Tanzania, nyumbani, Zanzibr wakati mwingine inaonekana kama inataka kujitenga na bara kwa sababu zisizoeleweka. Suluhu haitapatikana iwapo matabaka ya watu yananza kujitokeza nchini, kuna wale walio nacho, na wanacho kwelikweli, na wale wasio nacho wanakanyagwa na wenye nacho. Miaka imeenda sana na Afrika imebadilika kwa mema na kwa mabaya. Ukoloni bado upo na wakati huu mkandamizaji sio mzungu tena, bali ni WaAfirika we nzetu.
La mwisho, najisikia vibaya sana kuona jinsi baadhi ya wananchi hali yao ya maisha ilivo, I mean, People suffer so much just to live little life or just to survive in Africa, and That is a shame beacause Africa is rich. Unapoangalia mbele utaona wazi ya kuwa Africa inanunuliwa kimpangompango bila ya wanachi kujua kinachoendelea, japo mara moja moja utasikia kiongozi fulani amebakwa yuko mahakamani na magazeti na TV zikitangaza..... Almasi, Dhahabu, Tanzanite zitakuwa zinondolewa Afrika kwenda kwenye masoko ya nje bila ya wananchi kufaidika na chochote.
Nina Dada, shangazi, na mashemeji kibao, lakini sija wahi kumwona hata mmoja wao, amejiremba na Tanzanite."
KUHUSU HAYA YOTE KUATHIRI KAZI ZAKE AMA ZA AINA YAKE:
"ni kweli hii imeathiri sana utunzi na uimbaji wa nyimbo za aina yangu, la kwanza, ni kawaida kwa wasikilizaji hasa wenye umri mdogo na ambao ndio wengi, kutosikiliza nyimbo ambazo zinabeba ujumbe unaogusia maisha au matatizo,au kero za kisiasa ama magonjwa kama ukimwi na kadhalika. Wengi wanataka kusikia nyimbo zinazoburudisha na kuchekesha, kama wote tulivokuwa vijana. Wanataka kusikia na kucheza nyimbo ambazo zinazungumzia mabinti wa jirani, au bling bling, ama migari mikubwa mikubwa ama nyumba kubwa na "usafiri" wa mabinti na zaidi.... iko haja ya kuwahusisha vijana wajao, wenye vipaji na mawazo au fikra za kuburudisha na kuelimisha na kutangaza amani upendo na majambo yanajo husu jamii na mazingira na Tanzania na Africa kwa ujumla."
Sina ninaloweza kuongeza hapa. Blogu ya Changamoto yetu yamshukuru saana Kaka Inno kwa kutushirikisha kilichomsukuma kutunga, kinachoendelea kuumiza moyo wake kutokana na kutotatuliwa kwa matatizo na kile aonacho chaja siku zijazo.
Usikilize wimbo huu kiukamilifu hapa chini.

**Them, I & Them ni kipengele kikujiacho kila Ijumaa kinachoelezea kazi za wasanii (Them) kulingana na maono yangu (I) kwa ajili na manufaa ya hadhira (Them)**
Kwa nyimbo zaidi ndani ya kipengele hiki bofya hapa.
IJUMAA NJEMA

Thursday, July 1, 2010

"Watawala" hawa wanahitaji "SOMO LA AWALI LA URAIA"

Kama nakumbuka vema, basi URAIA NI ELIMU IHUSUYO HAKI NA WAJIBU WA RAIA KWA NCHI YAKE. Na kwenye haki na wajibu pia huwa laja suala la uongozi. Na kwenye UONGOZI kuna wajibu pia kwa wale uwaongozao.
Lakini mbali na uraia ufunzwao darasani, sote twatambua kuwa ili kuweza kuwa na suluhisho kwa tatizo, ni vema ukawa unalitambua fika tatizo hilo. Na katika mambo ya uongozi wa nchi ambayo yanahitaji mipango na ushauri wa watu zaidi ya "aliye juu" ina maana kunahitajika MUDA WA KUTOSHA KUWEZA KUJADILI NA KUWEKA KIPAUMBELE KWENYE MATATIZO MBALIMBALI.
Hivi majuzi (nikiwa huko nilikojichimbia nikikariri hili na lile) nikaona HARAKATI ZA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2010 zikishika kasi kwa wagombea wa vyama vya CUF na kisha CCM kuchukua fomu za kugombea nafasi ya Urais. Achilia mbali utitiri unaotangaza kugombea ubunge, udiwani nk. Na tena hawa wanachukua fomu kwa ajili ya kura za maoni / uchaguzi wa chama kumpata mgombea.
Rais Jakaya Kikwete akikabidhiwa fomu ya kugombea Urais na Katibu Mkuu wa CCM Yusuph Makamba makao makuu ya chama Dodoma.
Picha:
Dina Marios' Blog
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahimu Lipumba akichukua fomu za kugombea nafasiya Urais kutoka kwa Katibu wa Chama hicho Wilaya ya Kinondoni, Mh. Kassim Chogamawano
Picha:
Michuzi Blog Mwanachama wa chama cha siasa cha TLP Bwn Macmillan Lyimo (kushoto) akirejesha fomu ya kuomba kugombea uraisi kwa tiketi ya chama hicho kwa katibu mkuu wa chama hicho Meja Jesse Makundi huku katibu msaidizi wa TLP Bwn Hamad Tao akishuhudia.
Picha: Robert Oganda / DAILY NEWS
Ninalowaza ni kuwa kati ya siku hii mpaka Oktoba 31, watakuwa wameweza kutembelea majimbo ama sehemu ngapi kuweza kujionea kwa macho yao matatizo yaliyoko huko kisha kupanga mikakati ya kuyatatua kama watapewa ridhaa ya kuingia madarakani?
Labda kuna anayeweza kusema kuwa "kuna watendaji huko vijijini" lakini nani asiyejua UONGO WA KUTUPWA waufanyao watendaji hawa kumfurahisha "mgeni rasmi"? Haya tumeyasoma kwingi mpaka baadhi ya wananchi kufikia hatua ya kuwazomea viongozi na wengine kuchoka na ahadi zisizotekelezeka na kuanza kuwapiga mawe. Unakumbika yaliyotokea kwa Mheshimiwa Rais kule Mbeya? Kuna mengine yaliyotokea kabla ya hayo japo hakuna aliyenena kitu. Jikumbushe aliyoandika Dadangu Happy Katabazi kwenye makala yake HAPA. Na kama hiyo haitoshi, Rais Kikwete akaenda Morogoro mwaka huohuo akapewa takwimu za miaka 12 iliyopita REJEA HAPA. Unadhani kuna mtendaji atampeleka Rais ama Mwenyekiti wa chama chake kwenye "zahanati" kama hii? Ili aulizwe maswali ama? Sina hakika kama wagombea wanajua kuwa maisha ya hivi yapo duniani (achilia mbali ndani ya nchi yetu)
Picha: Beda Msimbe

Sasa nirejee kwenye suala la hawa WATAWALA wanaojiita viongozi.
Ni lini wagombea hawa watapata muda wa kuzungukia nchi, kuangalia na kukusanya mahitaji na matatizo yawakabilio wananchi, wayajadili, wayatengenezee mipango ya kuyatatua ama kuyatimiza (Ilani za uchaguzi) kisha warejee kwenye sehemu hizo na kuwaeleza wananchi namna watakavyowatatulia matatizo yao?
Kwani wenzetu hawa hawajui kuwa wajibu wao kama viongozi ni KUSAIDIANA NA WANANCHI KUTIMIZA YALE YAHITAJIWAYO NA WANANCHI WANAOWAONGOZA?
Ni kweli kuwa wagombea hawa wanalijua hili? Ama wako kwenye kukariri elimu ya uraia iliyo kubwa na kupuuza hii ya awali?
Na kwa kuwa kutakuwa na kambi mbili za chama tawala na vyama vya upinzani, bado wote wana majukumu na LAWAMA za kubeba. Niliwahi kuandika juu ya MASWALI YANGU 10 KWA RAIS JAKAYA KIKWETE (hapa) na kisha nikawa bayana juu ya yale YATAKAYOWAANGUSHA WAPINZANI KWENYE UCHAGUZI MKUU (hapa) na bado naamini hivyo.
Kuona wananchi wanateseka watesekavyo inasikitisha.
Kuona wapigao kampeni wanawafanya wananchi waamini kuwa WAO NDIO SULUHISHO NA SIO SEHEMU YA SULUHISHO INATIA KINYAA.
Na yote haya yanatokea kwa kuwa kila mpiga kampeni anasahau TAFSIRI YA URAIA ambayo ingemfanya yeye azungumzaye na wale wazungumziwao wajue kuwa wana WAJIBU NA HAKI ya kuhakikisha kuwa wanapata mahitaji yao kwa kushirikiana.
Hili lanifanya niamini kuwa WATAWALA HAWA WAGOMBEAO NAFASI ZA URAIS, WANAHITAJI SOMO LA AWALI LA URAIA.
Kwa wenzetu wangeweza sema "Civics 101 ama Introduction to Civics" ama...
Nawaza kwa sauti tuuu

Uchaguzi Tanzania ni "label" inayozungumzia namna niionavyo nchi yangu ya Tanzania ijiandaavyo na uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2010. Kwa maandishi mengine juu ya mada hii katika "label" hii BOFYA HAPA